Wednesday, December 14, 2011

Mazuri yachukueni

Dhahabu mazuriye, nayo yote ondokeni,
Ila pia mikosiye, kwenu nayo enendeni,
Na nyuma msirejee, mbali sana kafieni,
Mazuriye chukueni, na mikosi yake pia!

Na awapatiliziye, mwenye kisasi Manani,
Pabaya mtumbikiye, pasipotokeka shimoni,
Sauti tusisikiye, tuliopo midomoni,
Mazuriye chukueni, na mikosi yake pia!

Makuwadi muwagee, muwe nao abadani,
Na wote mtuondokee, kama vile nuksani,
Kivulini mjilie, mliokosa hisani,
Mazuriye chukueni, na mikosi yake pia!'

Heri yenu myatwae, zishibe zenu imani,
Ndani msiingilie, kuharibu ya nyumbani,
Muopoayo mwopoe, si wetu utamaduni,
Mazuriye chukueni, na mikosi yake pia!'

Tuachieni utufae, mashimo tukibaini,
Na wenetu waelewe, waroho ni kina nani,
Na kizazi kitambue, nani wa kumuamini,
Mazuriye chukueni, na mikosi yake pia!'

No comments: