Monday, December 26, 2011

Harusi-2

1.
Msigeuze harusi, zikawa ni kivumbasi,
Isirafu damisi, kwa shehe na makasisi,
Mjukuu Ibilisi, kisirani na nuksi,
Harusi kama hadithi, huishia muflisi.
2.
Ndoa ibada halisi, walisema waasisi,
Jambo lataka kiasi, si kushibisha nafusi,
Haliafiki Qudusi, mwingi wa kutanafusi,
Harusi kama hadithi, huishia muflisi.
3.
Nikahi ni fahirisi, utangulizi hukisi,
Lakudumu majilisi, pasiwe na wasiwasi,
Kaskazi au kusi, vyote kupata nemsi,
Harusi kama hadithi, huishia muflisi.
4.
Ikifanywa kwayo kasi, ya riha na anisi,
Hutia doa jeusi, katika moyo mkwasi,
Na kuleta uyabisi, kila kiungo kuhisi,
Harusi kama hadithi, huishia muflisi.
5.
Harusi kama libasi, wawili ni mahsusi,
Huleta hawa fususi, ya woto na utesi,
Hawapendwi maharusi, kipendwancho ni harusi,
Harusi kama hadithi, huishia muflisi.
6.
Hili lataka kiasi, hakika si wasiwasi,
Isirafu si nemsi, muulize Abunuwasi,
Na vitabu kadurusi, uone yake nakisi,
Harusi kama hadithi, huishia muflisi.
7.
Harusi si kiharusi, jasho na wingi kamasi,
Lataka bora ususi, mambo yenu kuasisi,
Yasiyoleta nuksi, balaa nayo mikosi,
Harusi kama hadithi, huishia muflisi.
8.
Harusi kitu halisi, hakichanganywi najisi,
Haumo kwenye kamusi, uchafu nao utesi,
Vinginevyo wasiwasi, na mgeni Ibilisi,
Harusi kama hadithi, huishia muflisi.
9.
Haitaki kandarasi, kuufanya uhandisi,
Huumeza ubinafsi, jumuiya kuasisi,
Ikawa yenye wepesi, umoja na urahisi,
Harusi kama hadithi, huishia muflisi.
10.
Humkataa chunusi, anayezusha mikosi,
Huyakimbia maasi, kwa mbio zake farasi,
Ili kutunza asasi, na kumkana ibilisi,
Harusi kama hadithi, huishia muflisi.
11.
Huchongwa moja libasi, ya kukaa maharusi,
Hawa zikatanafusi, huba ikawa msosi,
Pendo kuwa ni hadithi, simulizi kila mosi,
Harusi kama hadithi, huishia muflisi.
12.
Ila ikiwa najisi, haitokwisha mikosi,
Yatazidi na maasi, kusambaratika nafusi,
Ndoa ikawa nuksi, na familia kuhasi,
Harusi kama hadithi, huishia muflisi.

No comments: