Thursday, December 29, 2011

Kesi vyombo vya habari, kuunyonga ushairi.

Jaji:

Wasimama mtuhumiwa, mshairi ashtakia,
Unainyonga sanaa, ushairi Tanzania,
Kila unachoamua, ushairi wapungua,
Ni kweli una hatia, au wanakuzulia?

Mshairi shtakia, wote tupate sikia,
Kilio unacholia, na wao wapate jua,
Hukumu kusaidiwa, nitapokuja kutoa,
Ni kweli watuambia, au unamzulia ?


Mshairi:

Asante mheshimiwa, shtaka kulichukua,
Kilio nitakitoa, wote wapate sikia,
Sina sababu kuzua, ukweli mwajionea,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Gazeti ukiangalia, hakuna wanachotoa,
Mengineyo yamejaa, hata yasiyotufaa,
Kila ukiulizia, ujinga unajibiwa,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Nafasi wasingizia, ila huo ni umbeya,
Wengine wajisemea, udini yaliyojaa,
Fani ni Muhamadia, pekee inawafaa,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Kuua wamenuia, ushairi Tanzania,
Kiswahili nacho pia, kukinyonga wapania,
Ili nchi yote kuwa, Kiingereza yatumia,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Redio zinachanua, pembe zote Tanzania,
Karibu kila mkoa, redio utasikia,
Ila wanatukataa, wachache isipokua,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Michezo waparamia, msukule wadhania,
Uhai kisichokua, ndio kinapaliliwa,
Ni mitini wamekaa, juha tawi wakalia,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Televisheni mpya, ndio kwanza zaingia,
Nani anafikiria, ushairi kuulea?
Picha mbaya watatoa, ushairi wataua,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Intaneti yabakia, sasa inasadiaia,
Ila waliojaliwa, ni wachache walokua,
Vijijini wazubaa, wahofu wabaguliwa,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Nchi imeshalemaa, yasota teknolojai,
Rwanda yatutangulia, nyuma sisi twabakia,
Labda tukizinduliwa, zaidi itatutaa,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Mashuleni waduwaa, vitabu vilivyochakaa,
Hakuna kazi mpya, za zamani watumia,
Watoto zawachefua, darasani wajitoa,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Pasipo kuzungumzia, yale wanayoyajua,
Tungo zikasimuliwa, wote zinazosisimua,
Ushairi utapwaya, na mwisho uje jifia,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Walimu wanaojua, hii feruzi sanaa,
Wachache wamebakia, wengi wameshajifia,
Kazi wanaopanvgiwa, bongo fleva watia,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

UKUTA wamebomoa, wakubwa waliokuwa,
Miaka yasahauliwa, hakuna wa kusaidia,
Wazeeka waliokuwa, damu mpya yatakiwa,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Baraza lilibuniwa, leo ladharauliwa,
Ofisi zimefubaa, kisirani imekua,
Hata kompyuta pia, hakuna ilobakia,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Ni wote tunachangia, ushairi kuua,
Ilo wanaoshindilia, wahariri walokua,
Watu wangejisomea, mbali wangekumbukia,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Watu wangeusikia, roho ingesisimua,
Mapya kufikira, tukaacha kudumaa,
Kiuweli tukakua, na sio kuongopea,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Jaji umenisikia, japo kwikwi yanivamia,
Ni ukweli nimetoa, mtu sikumsingizia,
Naomba kufikiria, hukumu ya kuamua,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Shahidi:
Hakika mheshimiwa, hivyo ndivyo ilivyokua,
Kweli tupu kaitoa, sinalo la kukataa,
Tafakari kuamua, kitakachotusaidia,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!


Wakili:


Na mimi Mtanzania, uongo ninachelea,
Nini nitakuambia, Jaji unayesimamia,
Kweli mwenzetu katoa, chembe haikupungua,
Wahariri wauaji, ushairi na mshairi!

Jaji:


Ni nini nitaongea, bila ya mimi kulia,
Hata na zetu sheria, bado zimeelemewa,
Kiswahili hazijawa, kila mtu akajua,
Ila ninawaachia, Watanzania kuamua!

Tumelogwa nadhania, bahati kutoijua,
Ya watu twashikilia, yetu tunayaachia,
Uchumi ungelikua, Kiswahili kutumia,
Ila ninawaachia, Watanzania kuamua!

No comments: