Wednesday, December 28, 2011

Mnaanza kudarizi

Mnaanza mashauzi, kuchuma hatujachuma,
Nchi mwageuza mbuzi, kuchuna bila huruma,
Mwajifanya ni wawazi, kumbe yenu yako nyuma,
Mnaanza kudarizi, kufuma hatujafuma?

Yalazimu bumbuwazi, kwa kila mwenye hekima,
Msitufanye viazi, Mbozi wanavyovilima,
Macho yetu yako wazi, na masikio yasema,
Mnaanza kudarizi, kufuma hatujafuma?

Midomo ni mapinduzi, kuikataa dhuluma,
Na sura ni machukizi, mtendayo siyo mema,
Tungelikuwa bazazi, basi nasi tusingesema,
Mnaanza kudarizi, kufuma hatujafuma?

Ucheshi na matanuzi, hayajaleta neema,
Mmetufanya ushuzi, wanuka ila lazima,
Lini nchi yake majenzi, yategemea wagema?
Mnaanza kudarizi, kufuma hatujafuma?

Zinachosha simulizi, kulima tulishalima,
Bidii haina hadhi, faida isipochuma.
Na juhudi ni ushenzi, kama yarudisha nyuma,
Mnaanza kudarizi, kufuma hatujafuma?

Utenzi na uteuzi, mambo yataka hekima,
Udugu hauna enzi, kwenye kazi utazama,
Na kazi bila ujuzi, hugeuka ni ujima,
Mnaanza kudarizi, kufuma hatujafuma?

Mshairi sina kazi, kazi yangu ni kupema,
Na pasipo pema mjuzi, kutangaza ni lazima,
Baa wanaodarizi, na walipo ni kuhama,
Mnaanza kudarizi, kufuma hatujafuma?

Namshukuru Mwenyezi, kuniwezesha kalima,
Pekee ndiye mwenye enzi, napanda akinituma,
Habari ziso ajizi, nimejuza maamuma,
Mnaanza kudarizi, kufuma hatujafuma?


© 2011 Sammy Makilla

No comments: