Wednesday, December 28, 2011

Hayuko uongozini

Ni watoto wa mtaani, waongozao jahazi,
Kutanua yao fani, kelele na mashauzi,
Siamini yumkini, yumo mwenye utambuzi,
Hayuko uongozini, mtoto wa mkulima.

Kungelikuwa tauni, mwana kuwa kiongozi,
Tungeishi vijijini, afya isiwe ajizi,
Wangefurika wageni, kuja kuvuta pumzi,
Hayuko uongozini, mtoto wa mkulima.

Yangetiririka ndani, maji yaso uchafuzi,
Wanawake vijiini, isingelikuwa kazi,
Ngozi ziwe ni laini, wakaongeza mapenzi,
Hayuko uongozini, mtoto wa mkulima.

Kisegerema si shani, kingeliikosa kazi,
Mashine zije auni, mashambani na makazi,
Maisha yasiwe duni, wana wapate hifadhi,
Hayuko uongozini, mtoto wa mkulima.

Sanaa ninaamini, haya ni masimulizi,
Hayumo uongozini, mtoto wake mkwezi,
Ni watotowa mjini, vijiji kwao ushuzi,
Hayuko uongozini, mtoto wa mkulima.

Azuke aliamini, huko afanye makazi,
Apakimbie mjini, hadi watu kuwaenzi,
Kupambike vijijini, kwa kufuma na darizi,
Hayuko uongozini, mtoto wa mkulima.

Huduma ziwe amini, yatokee mapinduzi,
Wapendeze vijinini, mwnzo huu kuuenzi,
Tusifike duniani, kwa kutofanya ajizi,
Hayuko uongozini, mtoto wa mkulima.

© 2011 Sammy Makilla

No comments: