Sunday, December 25, 2011

Umoja wa nguvu tope

Wanasiasa nazaa, wazidi kutuchezea,
Vipi tunawaachia, mamlaka kuyatwaa,
Nao wanatuambia, serikali pagania,
Umoja wa nguvu tope, haukawii katika.

Nani anayeamua, nani awe wetu mbia,
Hivi kweli ni sheria, au imani murua,
Mbona mwatuchanganyia, hata tusivyovijua?
Umoja wa nguvu tope, haukawii katika.

Umoja huu bandia, juu ulioazimiwa,
Dini yetu unauua, kwa waovu kubakia,
Nanyi mwachekelea, kwa tunavyoteketea ?
Umoja wa nguvu tope, haukawii katika.

Katiba yazingatia, kila mtu anajua,
Ila ajabu sheria, mbaya zinazinduliwa,
Kielimu tumepoa, yabidi kuchemkia,
Umoja wa nguvu tope, haukawii katika.

Umoja unaofaa, wa kwetu kuuamua,
Viongozi kuchagua, madhehebu zilokua,
Kama bara na Zanzibar, dini nchi huru kua,
Umoja wa nguvu tope, haukawii katika.

Ndivyo wanavyoamua, manasara na ubia,
Ya peke wanachambua, na ya pamoja kuzua,
Sisi twashindiliwa, kwenye limoja gunia,
Umoja wa nguvu tope, haukawii katika.

Itakuja adilia, hili italiondoa,
Maovu kuyakataa, na haki kung'ang;ania,
Marufuku kutumiwa, kama cha pua kitambaa,
Umoja wa nguvu tope, haukawii katika.

No comments: