Friday, December 23, 2011

Mali pasipo elimu

Bora wanaojitia, kwa mali kulimbikia,
Heshima wakajitia, kwa waliyotunukiwa,
Wenyewe wakidhania, ukwasi wamechangia,
Mali pasipo elimu, wengine huitafuna.

Shule hawakuijua, nasibu imewajia,
Mtaji walipopewa, gia ya kuondokea,
Kasi inapozidia, hudharau na jamaa,
Mali pasipo elimu, wengine huitafuna.

Wengi huwadhulumu, kwa maarifa kuvua,
Wakajitia adhimu, kila kitu wanajua,
Hujikuta na zakumu, wanyeshwa kama maziwa,
Mali pasipo elimu, wengine huitafuna.

Wao wote umuhimu, mali itawasumbua,
Hujaa wana haramu, vibaba wakachukua,
Na hata ndugu wa damu, nuwa ni maharamia,
Mali pasipo elimu, wengine huitafuna.

Mali huiona tamu, na uchungu imejaa,
Wao huwa ni madumu, kata ndani zikatoa,
Hutaka kuwapa sumu, wanazigwaya sheria,
Mali pasipo elimu, wengine huitafuna.

Hata na wao hirimu, kisima hukigundua,
Huchoteana kwa zamu, bila kitu kubakia,
Na hawaishi hamu, mara tena hurudia,
Mali pasipo elimu, wengine huitafuna.

Hukufanza ni muhimu, tena ni mwenye kujua,
Wakusanii adhimu, busara zilizoloa,
Na kujifanya karimu, kuvuna kwa magunia,
Mali pasipo elimu, wengine huitafuna.

Mabinti wenye wazimu, malaika hujakua,
Wakavutia gidamu, farasi kutokimbia,
Hunyonya kichakaramu, hali nawe watulia,
Mali pasipo elimu, wengine huitafuna.

Mjini wanaharamu, sana watakusifia,
Hujipanga kwa nidhamu, wazidi kushangilia,
Waifuata nujumu, ya ulaji majaliwa,
Mali pasipo elimu, wengine huitafuna.

Waheshimiwa muhimu, na hao wake zao pia,
Watakuona beramu, njiani kukutumia,
Wafanye yao haramu, wenyewe wanaojua,
Mali pasipo elimu, wengine huitafuna.

Sala huwa ni adimu, na ibada kupotea,
Hayo tena si muhimu, cheo hupewa dunia,
Na mali kuwa sanamu, kuanza kuabudiwa,
Mali pasipo elimu, wengine huitafuna.

© 2011 Sammy Makilla

1 comment:

Makiya said...

Safi sana nimelipendaa