Monday, December 26, 2011

Wapi Bunge la mkoa ?

Itazame Estonia, angalia Lithuania,
Nako pia Georgia, Urussi iliyokua,
Ilikuwa ni mikoa, sasa nchi zimekua,
Mikoa haitochanua, hadi huru kuja kuwa,
Wakubwa kutembelea, hilo halitasaidia,
Wapi bunge la mkoa, mikoa kuendelea?

Hofu iliyowajaa, chama wanakihofia,
Kwingi kitafagiliwa, hakinayo manufaa,
Waamka Watanzania, vipya watachagua,
Pembeni wakisogea, itaamka mikoa
Na ukubwa kurudia, si rahisi itakua,
Wapi bunge la mkoa, mikoa kuendelea?

Mikoa haitaibiwa, uhuru ikipatiwa,
Waziri Mkuu akiwa, bora atayaamua,
Mikoa haitachezewa, dhahabu wakagawa,
Misitu itaokolewa, na wanyama nao pia,
Vyanzo vya maji kua, salama kwa mamia,
Wapi bunge la mkoa, mikoa kuendelea?

Budi bunge la mkoa, mkoa kuzungumzia,
Sio kwa kututania, bali kwa kuazimia,
Maamzi kuamua, mbele yanayotufaa,
Kisha nasi kusogea, tusiwe wa kusinzia,
Uchumi kuunyanyua, hali bora tukajua
Wapi bunge la mkoa, mikoa kuendelea?

Jamii kusimamia, hadi ikajikomboa,
Nyumba kuasisia, kila mji zikajaa,
Vijiji kuwa vipya, watu wakajahamia,
Maendeleo kuzua, wageni kufurahia,
Wapi bunge la mkoa, mikoa kuendelea?

Nchi jirani zikawa, ni wake mkoa ubia,
Kuuza na kununua, bila ya kuzuiliwa,
Walanguzi kuwangoa, na kodi zenye udhia,
Unyonyaji kukataa, huria sote tukawa,
Wapi bunge la mkoa, mikoa kuendelea?

Wanaochelea tambua, hofu imewaingia,
Walichofanya wajua, vigumu kuvumiliwa,
Ukubwa walipopewa, nchi kama wameuziwa,
Wavuna wasikotia, na haramu kuchukua,
Siku itakapowadia, redioni kuvisikia,
Wapi bunge la mkoa, mikoa kuendelea?

Nchi zote za dunia, ushirika utakua,
Kuunyanyua mkoa, kwa biashara huria,
Na misaada kuingia, mkoa ikasaidia,
Mawaziri wakapewa, shughuli kuzifanyia,
Dar hazitoshia, wala tena kujaliwa,
Wapi bunge la mkoa, mikoa kuendelea?

Mikoa shule itakuwa, viongozi kufunziwa,
Uwaziri watajua, kwenye ngazi ya mkoa,
Miaka watakayokaa, nayo itahesabiwa,
Mazuri watakayotoa, kitaifa kutumiwa,
Nchi ikiwachagua, hawatajifunza jipya,
Wapi bunge la mkoa, mikoa kuendelea?

No comments: