Wednesday, December 28, 2011

Mji kukosa gazeti

Redio isipokua, vigumu kuendelea,
Hapatazungumziwa, matatizo yalokua,
Na jinsi ya kutatua, mkoa kuendelea,
Mji kukosa gazeti, utatawala ujinga!

Wapi watazungumzia, muhimu yaliyokua,
Hoja wakazisikia, na aula kuchagua,
Kisha kujajipangia, na bajeti kuandaa,
Mji kukosa gazeti, utatawala ujinga!

Mikakati kuamua, mkoa unaofaa,
Mbinu wakazichambua, kazi rahisi ikawa,
Miaka ikapungua, afueni kutokea,
Mji kukosa gazeti, utatawala ujinga!

Gazeti lisipokua, wajinga wanachanua,
Hoja hawatazijua, ndiyo wataitikia,
Viongozi huchagua, wale wasiowafaa,
Mji kukosa gazeti, utatawala ujinga!

Wananchi wataibiwa, kila chao kilokua,
Rasilimali hupaa, na mali asili pia,
Na fedha hukwapuliwa, mchana wajionea,
Mji kukosa gazeti, utatawala ujinga!

Tovuti isipokuwa, ni mji uliovia,
Watalii hukimbia, hapo tena hawatakaa,
Kwingine huelekea, mawasiliano yakawa,
Mji kukosa gazeti, utatawala ujinga!

Televisheni kupwaya, mji huja kudumaa,
Katu hautaendelea, utazidi kusinyaa,
Na vijana husanzua, jijini kukimbilia,
Mji kukosa gazeti, utatawala ujinga!

Simu zisipoenea, mawasiliano huvia,
Vijana hupakimbia, kwingine wakaingia,
Kamwe hawatasalia, hata ukiwafungia,
Mji kukosa gazeti, utatawala ujinga!

Wakati tumefikia, maamuzi kuamua,
Redio za umma kua, kila mji Tanzania,
Ya mji kuzungumzia, na yanayotarajiwa,
Mji kukosa gazeti, utatawala ujinga!

Magazeti nayo pia, kila mji yatakiwa,
Habari zao kujua, mambo kuchangamkia,
Ya wengine kusikia, kurasa zinazofatia,
Mji kukosa gazeti, utatawala ujinga!

Tovuti tunatakiwa, kila kona kuchanua,
Ukienda kutembea, Google wajipatia,
Migawaha maridhawa, huduma ikazitoa,
Mji kukosa gazeti, utatawala ujinga!

Televisheni mbia, picha inatupatia,
Ni mengi tunayojua, papo hapo kujionea,
Ziara kujifanzia, hali chumbani twakaa,
Mji kukosa gazeti, utatawala ujinga!

Wakale hawakujua, umuhimu ulokua,
Uongo walichelea, gizani tukabakia,
Alamu katujalia, sasa zaangazia,
Mji kukosa gazeti, utatawala ujinga!

Ila kinachotokea, uchafu zinachukua,
Bado hatujajitambua, wenyewe twajiumbua,
Viongozi watakiwa, hili kuliangalia,
Mji kukosa gazeti, utatawala ujinga!

Zingekuwa za mkoa, vyemja zingedhibitiwa,
Kumoja kutolemea, na kwingine kuonea,
Na wanaosimamia, umiliki kuchukua,
Mji kukosa gazeti, utatawala ujinga!

Muhimu yangelikuwa, yanayozungumziwa,
Miji ije kuchanua, kama Ulaya ikawa,
Ikang'ara Tanzania, hadi huko Malaysia,
Mji kukosa gazeti, utatawala ujinga!

© 2011 Sammy Makilla

No comments: