Friday, December 30, 2011

Babangu hajulikani

Hivi kazi nitapata, babangu hajulikani,
Barua nikizileta, kitu zitaaidia ?
Kitu gani nitaleta, hakika nayo nikawa,
Babangu hajulikani, hivi kazi nitapata ?

Ubavuni nikijata, kwa baba wa kufikia,
Hawawezi kunisuta, sio walionizaa,
Jina langu wakafuta, mitaani kutupiwa?
Babangu hajulikani, kazi naweza kupata?

Ubunge hakuupata, baba alipogombea,
Ufakiri kapakata, siwezi mtegemea,
Budi kazi kutafuta, pengine nitamsaidia,
Babangu hajulikani, kazi naweza kupata?

Uwaziri kaudata, kabaki kuusikia,
Na wakubwa hakuitwa, sio wa kuchagulia,
Umaskini anata, nani kumuangalia,
Babangu hajulikani, kazi naweza kupata?

Utajiri hakupata, ndugu kawasaidia,
Nyumbani tunachachata, mengi twabangaizia,
Walopata watusuta, nini tutawaambia?
Babangu hajulikani, kazi naweza kupata?

Najuta shemu Mjata, hali niliyofikia,
Nasaha naitafuta, waniachie na saa,
Twala wali wa mafuta, na nazi nilizoea?
Babangu hajulikani, kazi naweza kupata?


© 2011 Sammy Makilla

No comments: