Friday, December 16, 2011

Mnywaji akishakunywa

Kwa kiu ukizidiwa, mnywaji hukutambua ?
Nani kukusaidia, wao wajisaidia,
Mnywaji hatokunyanyua, ataka wake wale pia,
Mnywaji akishakunywa, humjuaje mwenye kitu?

Waongoza wenye njaa, kula mnategemea?
Matumbo yamewajaa, hewa tupu kumbe yawa?
Mioyo ganzi yeshakua, huruma watasikiya?
Mnywaji akishakunywa, humjuaje mwenye kitu?

Hawa wajilimbikia, nini watawaachia,
Kazi yao kuopoa, mwadhani ni wa kuvua,
Nyavu kujawapatia, hiyo kweli ruiya,
Mnywaji akishakunywa, humjuaje mwenye kitu?

Nchi itaendelea, bila mtu kuendelea,
Hii ni kubwa sanaa, mwanzo wake sijajua,
Lakini inapoishia, tayari ninapajua,
Mnywaji akishakunywa, humjuaje mwenye kitu?

Ustawi motokaa, na njia zinafatia,
Sijapata kusikia, ila sasa naambiwa,
Kwa mguu natembea, najua nitapofikia,
Mnywaji akishakunywa, humjuaje mwenye kitu?

Nyumba wanazikataa, si msingi wa kufaa,
Fedha wanajirushia, vigumu chini kutua,
Kile kisichotufaa, kwao dili imekua,
Mnywaji akishakunywa, humjuaje mwenye kitu?

Kazi watuimbia, maneno usiokua,
Ala hazijatimia, burudani yazubaa,
Na kula anayejua, huhofu kuzinguliwa,
Mnywaji akishakunywa, humjuaje mwenye kitu?

Fumbo wawafumbia, wajanja wasiokua,
Mjinga aking'anua, ataondoa udhia,
Na juu kinachokua, lazima chini kutua,
Mnywaji akishakunywa, humjuaje mwenye kitu?

© 2011 Sammy Makilla

No comments: