Sunday, March 3, 2013

WATAKA KUNIUNGUZA ?



MKONO sintanyanyua, kukufanyia ubaya,
Ila moyo nafungua, dua nikajisomea,
Ukinitakia baya, zuri nitakuombea,
Wataka kuniangusha, usijeanguka wewe!

Ku'ngua waniombea, moto sintokuombea,
Maji unanimwagiwa, kutozama nakwombea,
Ila ulimi zuia, laana kutoitoa,
Wataka kuniunguza, utajiunguza wewe!

Wanitakia balaa, mie nipate umia?
Mwili ninakuachia, ila roho nakataa,
Hayo yako mazoea, siwezi kukuzuia,
Wataka kuniumiza, utaumia mwenyewe!

Wapuliza kwa ghasia, kuzimwa wanitakia,
Pumzi nakuachia, utambi najishushia,
Kwa tufani na mvua, kuzimwa nikakataa,
Wataka kunizimisha, usijezimika wewe!

Kuzama waniombea, chombo ninakuachia,
Mashimo ungefukua, bahari kuongezea,
Chewa ataniokoa, nchi kavu kurejea,
Wataka kunizamisha, usijekuzama wewe!

Kama mti wanivaa, na shoka kushambulia,
Kisa unaniombea, kuanguka natembea,
Nyayo sijashadidia, mlio hutosikia,
Wataka kuniangusha, usijeanguka wewe!

Wataka nikaaangiza, na upate niunguza,
Na masinzi kunitunza, mkaa kunieneza,
Kisha ukanipakiza, na majivu kunikwaza,
Wataka kuniunguza, utajiunguza wewe!

Kila ukikusudia, majidi akuumbua,
Sio njema yako nia, na yeye ameshaijua,
Mwenyewe namuachia, zawadi kukupatia,
Wataka kuniumiza, utaumia mwenyewe!

Kwani yeye ni mtoa, tena ndio mchukuwa,
Mgawaji maridhia, daima anayebakia,
Kila mwenye kujitia, mwishowe anaujua,
Wataka kunizimisha, usijezimika wewe!

Miye nimemridhia, yangu kan

Thursday, February 21, 2013

u s i t u p e v i o n g o z i

KAMA wapo waondoe, safu zikasafishika,
Tena usitujalie, mamlakani kuwaweka,
Nasi utuhurumie, tusiwe wa kuteseka,
Usitupe viongozi, waliokuwa fisadi!

Marafiki na mashoga, jamaa hao dhihaka,
Kaumu Lutu kubwaga, yakini kusalimika,
Wageuze ni maboga, na tembo kukanyagika,
Usitupe viongozi, marafiki na mashoga!

Wazungu waabuduo, na wengineo nao pia,
Tuwe tuwatapikao, yakwao tukayazoa,
Wawe wabakiao, ni rafiki wa kukaa,
Usitupe viongozi, waabuduo Wazungu!

Vijiji vinaugua, nani kuviangalia,
Hata maji wachimbua, badala ya kufungulia,
Huu mkubwa ukiwa, na viongozi waridhia,
Usitupe viongozi, vijiji wasiojali!

Wenyewe wajipendelea, wao na zao jamaa,
Wazee wawatezea, uzeeni kuumia,
Ahadi wakazitoa, hamsini zisokuwa,
Usitupe viongozi, wazee wasiotunza!

Huwatumia vijana, kufata yao mapenzi,
Ila kutenda ya maana, kwalo hawana ujuzi,
Maisha duni waona, vijana kukosa kazi,
Usitupe viongozi, vijana wasiothamini!

Waliojaa hadaa, kuwazaini raia,
Mola kutotujalia, na kama wapo ondoa,
Hii ni ya umma dua, Muumba wetu sikia,
Usitupe viongozi, wadanganyao wananchi!

Wala rushwa ni balaa, hasa chama kupitia,
Hawaoni ni udhia, nchi watajiuzia,
Watumwa raia kuwa, upya wakatawaliwa,
Usitupe viongozi, ambao ni wala rushwa!

Tuepushe na balaa, kwa kuwadi kujaliwa,
Na wezi wenye ubia, vya nchi wakachomoa,
Ni vibaka walokuwa, hadhi wanaitumia,
Usitupe viongozi, wanaokula na wezi!

Ubabe wanaotumia, huja kuzusha ghasia,
Hasira ikipasua, hakuna wa kutuokoa,
Kila mtu kukimbia, kwenye moto tukatua,
Usitupe viongozi, ubabe wanaonunua!

Saini wanazitia, wakubwa waliokuwa,
Fedha wakazidokoa, benkini zilizokaa,
Na dhahabu kuitwaa, binafsi ikawafaa,
Usitupe viongozi, benki kuu waibao!

Wazungu kuwasikia, ya kwao wanayozua,
Wa kwetu kuwaonea, Pasina kuwa na hya,
Vyao vikachukuliwa, Kimya kimya vikaliwa,
Usitupe viongozi, waabuduo wazungu!

Nasi tukashingilia, dini zetu kuchukia,
Na ugaidi kuridhia, sera yetu na ikawa,
Upofu tukajitia, kuridhi tusichojua,
Usitupe viongozi, imani wanaochezea!

Fata upepo tukawa, sio wa kujitambua,
Lao tukaitikia, pasipo kuliulizia,
Ukweli tukaujua, kwa akili kuamua,
Usitupe viongozi, yetu wasiofikiria!

Kuna walevi wajaa, irabu ni kutumia,
Shilingi wakiijua, huko watachokonoa,
Na akiba kuitoa, ikaenda kupotea,
Usitupe viongozi, walevi wa kutumia!

Wasiokuwa na haya, nao sasa wamejaa,
Aibu imeshawagwaya, na soni yawakimbia,
Waweza kujifanyia, hata usofikiria,
Usitupe viongozi, hayawani walokuwa!

Raia wanaoibia, uwaangaze Jalia,
Katu kutokuwaachia, ovyo wakatutendea,
Ufakiri kututia, na nusura kutojua,
Usitupe viongozi, raia wanaoua!

Dhuluma tunazijua, hai walotufanzia,
Na marehemu kadhia, hata nao waijua,
Hawa kiwaangazia, utaijua hidaya,
Usitupe viongozi, dhuluma waliojaa!

Wanaabudu dunia, vichaa waliokuwa,
Wao wakajidhania, milele wataikaa,
Na kufa kutoridhia, wengine wakawaua,
Usitupe viongozi, waabuduo dunia!

Ving'ang'anizi balaa, hawafai Tanzania,
Nafasi waliotwaa, watake tena rudia,
Hao ni kuwafagia, pembeni wakazolewa,
Usitupe viongozi, ving'ang'anizi wakubwa!

Mabomu wanaotumia, kupiga ovyo raia,
Na dola kuitumia, vibaya isivyokuwa,
Mkoloni bora kuwa, hao ni wa kuwaondoa,
Usitupe viongozi, raia waumizao!

Akili waliofubaa, kuzua wasiojua,
Mirija wakaachia, vya kwetu ikajinywea,
Sisi kutojipatia, chungu chetu kikajaa,
Usitupe viongozi, wasojua kutafuta!

Wafuliao kuchuma, hawafai uongozi,
Mengi sana watasema, ila hawawezi kazi,
Nje hawa kuwatoma, tupate wenye ujuzi,
Usitupe viongozi, wasioweza kuchuma!

Migodi wanaouza, badala ya sisi kuchimba,
Sawa na bure kuuza, hao lazima kuchamba,
Nchi tukaigeuza, kwa nje tukawasomba,
Usitupe viongozi, vito bure wauzao!

Nchi wanaoikwaza, kwa kila kitu kuwa upya,
Mipango kuichakaza, kabla haijatumiwa,
Kila siku kuanzia, nyuma ya tulipoishia,
Usitupe viongozi, upya mambo waanzao!

Waficha fedha Uswizi, hawa sio maswezi,
Ya kwao hatuyawezi, miili hufa kwa ganzi,
Ni mikubwa midokozi, wanazidi majambazi,
Usitupe viongozi, fedha waficha Uswizi!

Watumiao uchama, watufanzia zahama,
Nchi inaikosa kalima, demokrasia kukwama,
Sasa tunarudi nyuma, kwa kujenga uhasama,
Usitupe viongozi, watumiao uchama!

Vitisho wavipikao, hawajui kupakua,
Ni moto wauwashao, na chuki kujipandia,
Wapo roho watoao, yao kuyapigania,
Usitupe viongozi, kutawala kwa vitisho!

Dinichini wawekao, wao juu kujiona,
Hawa kama malimao, kazi wisha kikamua,
Inani haiko kwao, dunia yawahadaa,
Usitupe viongozi, dini waicheza shere!

Waongo waliokuwa,imani huiondoa,
Kukesha kuaminiwa, ovyo kusikitikiwa,
Hakuna wa kuwasikia, kila kitu hufulia,
Usitupe viongozi, waliokuwa waongo!

Waizi na haramia, mbali kutuepushia,
Nchi najisi watia, tohara haitakuwa,
Huyazusha mabalaa, nchi yote kuenea,
Usitupe viongozi, waliokuwa waizi!

Waipendao zinaa, ni haramu kutwachia,
Nchi laana yakaa, malaika kukimbia,
Mioto twajiwashia, ya kushoto na kulia,
Usitupe viongozi, ambao ni wazinifu!

Nchi wanayoiuza, twaomba kuangamiza,
Dakika kutowatunza, mabaya wakafanyiza,
Ya kwao ukayakwaza, Tanzania kutopoteza,
Usitupe viongozi, taifa wanaouza!

Kisasi waliojaa, Muntakimu umbua,
Wewe ndiwe muamua, wengine wanajitia,
Kisasi unakijua, wao kuwageukia,
Usitupe viongozi, waliojaa kisasi!

Dikteta ni balaa, ya Amini twayajua,
Joka tunamtambua, ndani kwake kumvaa,
Kisha tukamuondoa, na nje kumtupilia,
Usitupe viongozi, ambao ni dikteta!

Wataniao raia, kwa katiba kuwaibia,
Kisha wao kujitia, ndio juu walokuwa,
Hukumu ukiitoa, twajua yakutarajia,
Usitupe viongozi, katiba wapinduao!

Muamuzi kiamua, hakuna cha kubakia,
Na watu huwajalia, wakautoa udhia,
Hata kwa zao hadaa, bado tu wakafulia,
Usitupe viongozi, waliojaa hadaa!

Ambao kama bidhaa, dukani kununuliwa,
Yakini hao nazaa, isiwe tukajaliwa,
Mbali kutuepushia, na waliopo ondoa,
Usitupe viongozi, bidhaa waliokuwa!

Wote wanaoteuliwa, ni wenyewe wajifaa,
Na bwana kutumikia, wala si raia kufaa,
Uchungu hawajajua, mwana hawajamzaa,
Usitupe viongozi, ambao huteuliwa

Manyang'ayu karaha, kama Kenya ilivyokuwa,
Sasa kwetu waingia, vipi twawavumilia?
Mbepari mjamaa, kiongozi Tanzania?
Usitupe viongozi, ambao ni manyang'au!

Ubepari waingia, wazaini ujamaa,
Mizizi wajichimbia, juu waliokuwa,
Ardhi kujiuzia, cha mbele wakapatiwa,
Usitupe viongozi, waenzio ubepari!

Ubora wanaojitia, yao kuonea haya,
Imani kuwapotea, utumwa wakajitia,
Hawa si wa kutufaa, ni watu wa kutumiwa,
Usitupe viongozi, wanaojiona ni bora!

Pesa wanaotumia, watu kujinunulia,
Kisha wakachaguliwa, kwa hila kuitumia,
Ni dhuluma na nazaa, kutokuivumilia,
Usitupe viongozi, watu wanaonunua!

Wajanja wanaojitia, kumbe wajinga wajua,
Kamba ni kuwaachia, wenyewe kujinyongea,
Hauwezi kushangaa, maana yao wajua,
Usitupe viongozi, wajifnayao wajanja!

Wasiopenda kusoma, na daima maamuma,
Maamuzi kujitoma, bila kujua kalima,
Hawa meli yao kuzama, ni kitu kilo adhama,
Usitupe viongozi, wasiopenda kusoma!

Wenye chuki na husuda, huroga kuneemeka,
Ni la kwao kwa kaida, hawawezi chukulika,
Hata wakiwa makada, hai bora kuwazika,
Usitupe viongozi, wenye chuki na husuda!

Uungu wanaotaka, na riziki kuitoa,
Wamalize kwa hakika, kama hawatakujua,
Jambo lako la hakika, na wahaka haijawa,
Usitupe viongozi, miungu wajifanyao!

Majibari na jeuri, njia yao waijua,
Firauni ni amiri, aliyekukutezea,
Ukamtia kabari, na yake kupotezea,
Usitupe viongozi, jeuri waliojaa!

Dharau waliojaa, na kiburi kujitia,
Yao yapate sinyaa, na maradhi kutwaa,
Heri kutoifungua, na shari kuwagawia,
Usitupe viongozi, dharau waliojaa!

Wenye njaa Tanznia, viongozi walokuwa,
Ni maradhi waugua, hebu kuwapatilizia,
Mbali waende ishilia, nchi hawawezi kuifaa,
Usitupe viongozi, wenye njaa isoisha!

Utajiri waabuduo, kuwaacha ni radhia,
Mitaji tutafutayo, mashaka sije kutiwa,
Uhai tukiwa nao, hata nasi hujichumia,
Usitupe viongozi, waabuduo utajiri!
Usitupe viongozi, wasiosema ukweli!

Kutunza wasiojua, hawafai Tanzania,
Ubadhirifu wajaa, uchungu hawajatiwa,
Vya kwetu wavitumia, na akiba waing'oa,
Usitupe viongozi, iktisadi wasojua!

Kukopa wamezoea, deni watuongezea,
Tunalibeba jamaa, vijukuu kuachia,
Si haki inavyokuwa, wengine twawaonea,
Usitupe viongozi, waishio kwa kukopa!

Kodi wanaotafuna, hawafai Tanzania,
Yafaa nao kwachana, haki tukajitendea,
Huu si wetu muamana, tunaibeba balaa,
Usitupe viongozi, kodi wanaoitafuna!

Elimu wasioenzi, nyuma wanaturudisha,
Sio wetu wanagenzi, wanaizaya nasema,
Linatakiwa zowezi, pembeni kuwasukuma,
Usitupe viongozi, elimu wasioenzi!

Michezo wasiojali, ila maneno kuzidi,
Hao si marijali, kadari waikaidi,
Hawataki afadhali, vijana homa kuzidi,
Usitupe viongozi, michezo wasiojali!

Afya wanaokwaza, watu kuzidi ugua,
Si watu wa kuweza, ni lazima kuondoa,
Tasnia waitatiza, ukubwa kung'ang'ania,
Usitupe viongozi, afya wasiojali!

Wala wao wakashiba, sisi makombo watwachia,
Chajaa chao kibaba, chetu chazidi pungua,
Na ni wao mrahaba, sisi twazidi ugua,
Usitupe viongozi, wala, tukala makombo!

Keki wakiipakua, kubwa wanajigawia,
Sababu wakizitoa, vigumu kutuingia,
Uongozi kujifaa, wala sio kutufaa!
Usitupe viongozi, kubwa wala,chache yetu!

Masikini waumia, hali kwao sasa mbaya,
Mikakati watumia, wenye nacho kuwafaa,
Fakiri aliyekuwa, azidi kupotezewa,
Usitupe viongozi, wasiofaa maskini!

Wanakula ya fakiri, wao wanaochagua,
Mnyonge kweli kafiri, nani wa kumfaa,
Maisha yake ni shari, na majuto kujutia,
Usitupe viongozi, walao vya mafakiri!

Wengine tukichagua, aibu wajionea,
Imani yao kufaa, ubaya wakaamua,
Mbegu bora kichipua, wao wanazichimbua,
Usitupe viongozi, imani wanaokejeli!

Mapagani wanakuwa, hofu hawana moyoni,
Shetani kawachagua, yake yawe ni ubani,
Na wao wameamua, wadhani wa salamani,
Usitupe viongozi, ambao ni mapagani!

Walimu wanaokwaza, dira wanaipoteza,
Maumivu twayakuza, na nchi twailemaza,
Kitu gani tutaweza, labda iwe miujiza,
Usitupe viongozi, wanaokwaza walimu!

Wadharau daktari, wao bora kujiona,
Hili hawajalihariri, ni kosa tena kubwa sana,
Haujengi ufahari, mengi tutapotezana,
Usitupe viongozi, daktari wasothamini!

Na wenye njaa ya sifa, watengezee kashfa,
Uwe wa bure wadhifa, kila pembe una nyufa,
Na kukosa maarifa, iwe ni yao masafa,
Usitupe viongozi, wapendao kusifiwa!

Watakao abudiwa, shiriki wanaizua,
Nawe dawa waijua, dozi ungewapatia,
Ndiwe mwenye kuamua,tuepushie Tanzania,
Usitupe viongozi, watakao abudiwa!

Imani ninailea, nawapatia usia,
Mko huru kuamua, kupu'za au kusikia,
Mola namshuhudia, mmoja aliyekuwa,
Usitupe viongozi, watenga dini na siasa!

Magharibi yatuvaa, na upofu kututia,
Yao kufuatilia, yetu tukayaachia,
Utamani Afrika, ni imani kutangulia,
Usitupe viongozi, watenga dini na siasa!

Wenye heri huamua, imani kuichangia,
Wala si kuitumia, mwenyewe kujifagilia,
Na kisha uakdhania, salama utabakia,
Usitupe viongozi, watenga dini na siasa!


Uranium wachezeao, mabahau kutufanza,
Ili wachume wao, mbali wanaojitunza,
Hakika kina mfamao, hawafai maliwaza,
Usitupe viongozi, uranium wachezeao!

Sensa wanaochezea, na takwimu kuzipika,
Hila wanayoitia, na uongo kuzagaa,
Na vitisho kuvitia, Muumba akaona haya!
Usitupe viongozi, sensa wanaochezea!


Tunu kuombea uwazi, uwajibikaji, haki za binadamu,
usawa, demokrasia na utawala na menejimenti bora Tanzania na Afrika!
-Mwandishi.



Saturday, December 29, 2012

Maneno tumeshashiba



KUSHIBA hamkuchelewa, ukubwa mlipopewa,
Vipit mwatutarajia, sisi tuwe twangojea ?
Mwenye shibe nimejua, hamjui  mwenye njaa,
Maneno tumeshashiba, tuna njaa ya vitendo.

Watu wamevumilia, sasa wajitapikia,
Nusura wakingojea, miaka ikaishia,
Uzee wakaingia, na wengine kujifia,
Maneno tumeshashiba, tuna njaa ya vitendo.

Wachoka Watanzania, wachche kujishibia,
Kisha wao kuambiwa, watakiwa kungojea,
Kingine kupakuliwa, mwaka ukisharejea,
Maneno tumeshashiba, tuna njaa ya vitendo.

Dhihaka wajionea, mingine kuingojea,
Leo leo vyatakiwa, uhaini kuwafaa,
Sio kuwangojea, maiti wameshakuwa,
Maneno tumeshashiba, tuna njaa ya vitendo.

Kitu hawatasikia, subira kutambuliwa,
Neno wanalingojea, kazi ikishatimia,
Miliki kuichukua, kufaidi manufaa,
Maneno tumeshashiba, tuna njaa ya vitendo.

Tena hawatangojea, kaya kujahadithiwa,
Wanataka kutumiwa, funguo za kufungua,
 Makasha yameshajaa, wenyewe wakachagua,
Maneno tumeshashiba, tuna njaa ya vitendo.

Vingine wataamua, vingine kuviondoa,
Usafi wakajitia, hadi mwaji kujimwagia,
Manukato wakatia, harufu kuziondoa,
Maneno tumeshashiba, tuna njaa ya vitendo.

Ubani kufukuzia, uoza ukafukiwa,
Pale wakijitambua, na dhamana kuitwaa,
Wawe wanajivunia, nchi yao imekuwa,
Maneno tumeshashiba, tuna njaa ya vitendo.




Kweli mwalimu dunia



Ukweli akikwambia, kujali unatakiwa,
Somo ameliandaa, na dunia aijua,
Wewe ukalikataa, mwenyewe utaumia,
Kweli mwalimu dunia, kazi yake anajua!

Uongo akikwambia, fupi huwa yake njia,
Wewe ukauchagua, maisha kukusaidia,
Hatua itafikia, ukweli ukatambua,
Kweli mwalimu dunia, kazi yake anajua!

Wizi akihofia, huja ukakuumbua,
Wewe ukajichekea, na kazi kwendelea,
Siku ya kushtukiwa, moto unaweza tiwa,
Kweli mwalimu dunia, kazi yake anajua!

Haki akikuambia, vibaya kujiuzia,
Wewe ukamtania, na lako kuendelea,
Huja siku kweli kuwa, haya ukajionea,
Kweli mwalimu dunia, kazi yaek anajua!

Zinaaa akihofia, pabaya hukuchukua,
Wewe ukamnunia, na batili kuingia,
Yanapokujatokea, mbali nawe atakuwa,
Kweli mwalimu dunia, kazi yake anajua!

Tamaa akikumbia, hukuingiza pabaya,
Wewe ukajichekea, na kuilea tabia,
Itakuja kuumbua, naye kajiondokea,
Kweli mwalimu dunia, kazi yake anajua!
Uroho akikuambia, waweza kugeukia,
Wewe usiposikia, yanakujakutokea,
Kisha ukajililia, ujinga uliokuwa,
Kweli mwalimu dunia, kazi yake anajua!

Uchu akikuambia, athari kuangamia,
Wewe ukapuuzia, na yako kuendelea,
Siku yakijajizoa, na wewe hutojijua,
Kweli mwalimu dunia, kazi yake anajua!

Watu akikuambia, kuheshimiwa wafaa,
Na thamani kuijua, masihani kiingia,
Wewe ukalikataa, utakuja lijutia,
Kweli mwalimu dunia, kazi yake anajua!

Wazazi wakifulia, itakufunza dunia,
Bila fimbo kuchukua, yakabidi kuingia,
Tena laivu yakawa, mwenyewe wajionea,
Kweli mwalimu dunia, kazi yake anajua!'

Alimu namuachia, njia anayeijua,
Kizazi kuangalia, kisiwe kinapotea,
Njia usiyoijua, haifai kuingia,
Kweli mwalimu dunia, kazi yake anajua!

Mpenda vya ukoloni




Sheria za jalalani, zisibaki vitabuni,
Uhuru tulishawini, twafhifadhi ukoloni ?
Nani ataliami, atokaye Ulayani ?
Mpenda vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Kama hapana uhuni, basi sisi majinuni,
Au tunayo moyoni, haki yasiyoamini,
Raia twawazaini, hali nasi wakoloni ?
Muenzi vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Misingi hatuamini, usawa inayowini,
Tunaufanya utani, ustawi kuzaini,
Huu sio uhaini, ukiwemo katibani ?
Mpenda vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Viongozi duniani, raia wanazaini,
Watwaa ya ukoloni, kuhodhi madarakani,
KIlichokuwa uhuni, sasa chapewa thamani,
Muenzi vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Kuna mabomu yakini, ya machozi na hewani,
Hayachagui ni nani, atupiwa uwanjani,
Wazee na afkani, wote watiwa kundini,
Mpenda vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Sheria za uhaini, zawaficha watu ndani,
Dhamana ikawa guni, japo iko katibani,
Ya mtu wayathamini, sio yalo sheriani,
Mpenda vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Mikutano na maoni, yakatolewa uzani,
Wakaingia vitani, kodi inayoauni,
Mlipa akawa duni, kama damu na mumiani,
Muenzi vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Kuna nyingi za kihuni, waziachia nchini,
Haki haziithamini, ila kulinda fulani,
Zisizotiwa ubani, wala usawa kuwini,
Mpenda vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Uhuru wetu ni chini, viwango haujawini,
Katiba zungumzeni, uhuru kuuthamini,
Kisha kutathmini, chapungua kitu gani,
Muenzi vya ukoloni, na yeye ni mkoloni!

Uchochezi ndio nini



Uhaini ndio nini, pakiwepo ushindani,
Wanasheria watani, naomba lizungumzeni,
Latutia matatani, sisi tusiobaini,
Uchochezi ndio nini, dunia ya ushindani?

Niandike kitu gani,  uchochezi kutoghani,
Kama maji siyaoni, niseme yako njiani,
kama twaishi gizani, niige niko nuruni ?
Uchochezi ndio nini, dunia ya ushindani?

Kama shibe siioni, niseme niko makini,
Njaa iko hatarini, kuilaza kaburini,
Nitamdanganya mtu gani, kati ya walioko ndani ?
Uchochezi ndio nini, dunia ya ushindani?

Hata kichanga sidhani, baba kitaniamini,
Kitaniona ni mhuni, kama sio mamluni,
Akishanitathmini, akanitoa hisabuni,
Uchochezi ndio nini, dunia ya ushindani?

Nitakuwa hayawani, wengi wasiniamini,
Au kuwa utumwani, shaka watia moyoni,
Jamani niambieni, uchochezi kitu gani ?
Uchochezi ndio nini, dunia ya ushindani?

Haki zetu kubaini, nisiseme hadharani,
Katiba nisiamini, uhuru kunipa thani ?
Nizungumze kwa yakini, haki hata kwa maskini,
Uchochezi ndio nini, dunia ya ushindani?

Zama zenye ushindani, yote naona ilani,
Yategemea maoni, we, uko upande gani,
Hili ukitathmini, uhaini, uzaini,
Uchochezi ndio nini, dunia ya ushindani?

Mawakili elezeni, mna msimamo gani,
Na sisi tujiamini, pasina kuwa haini,
Itengezeni mizani, pande zote kuauni,
Uchochezi ndio nini, dunia ya ushindani?

SI UKUU HUU



KATIKA hii miaka, ya ujanja na hadaa,
Jambo ninalolijua, uchaguzi watakiwa,
Watu wakamchagua, kiongozi wa mkoa,
Si ukuu wa mkoa, nchi utakaojenga!

Kwenye mwaka wa fadhaa, ukweli tutapojua,
Uongo tukifaragua, na ukweli kuenea,
Nchi umoja kulea, lazima huru mikoa,
Si ukuu wa mkoa, nchi utakaojenga!

Nchi tuanjionea, vidogo vilivyokuwa,
Guinea Equatorial, milioni hawajawa,
Chumo wanajichumia, mkuu akachezea,
Si ukuu wa mkoa, nchi utakaojenga!

Dubai haijafikia, ya kwetu mingi mikoa,
Mauritius nayo pia, na Seychelles nakwambia,
Ila wanazitungua, hazinani kuingia,
Si ukuu wa mkoa, nchi utakaojenga!

Bahrain angalia, na Brunei nako pia,
Ka-Qatar ukijua, hautoyaridhia,
Ya kati kutawaliwa, watu wasikofikiwa,
Si ukuu wa mkoa, nchi utakaojenga!

Ili uchumi kukua, njia ni huru mikoa,
Yao wakayaamua, kupanga na kupangua,
Rasilimali zikawa, zinaufaa mkoa,
Si ukuu wa mkoa, nchi utakaojenga!

Wengine wakatambua, umuhimu watakiwa,
Za kwao kuzichumbua, pia nao kuwafaa,
Kubebana sio dawa, pua tutaangukia,
Si ukuu wa mkoa, nchi utakaojenga!

Mtu huru atakiwa, maamuzi kuyatoa,
Kisha akazingatia, utaifa kuufaa,
Mkoa kama nyumba huwa, kwanza kutolala njaa,
Si ukuu wa mkoa, nchi utakaojenga!

Yote kuichukulia, kama sawa imekua,
Ni siasa zenye njaa, katu hazitatufaa,
Mikoa kujitambua, hatuwezi likataa,
Si ukuu wa mkoa, nchi utakaojenga!

Mikoa kujitambua, fursa zilizokuwa,
Njia wakazichagua, za wao kuendelea,
Sawa haitatokea, tofauti itakuwa,
Si ukuu wa mkoa, nchi utakaojenga!

Haya tukiyaelewa, nchi tutaiimua,
Hamira tukaitia, ikaanza jifutua,
Kuoka rahisi kuwa, na vitamu kuzaliwa,
Si ukuu wa mkoa, nchi utakaojenga!

Umoja kuendelea, wala lhautajifia,
Ujerumani ni njia, hii waliyopitia,
Mtai anaijua, huko tulitembelea,
Si ukuu wa mkoa, nchi utakaojenga!

UJimbo sio balaa, bali sasa ndio njia,
Kenya wameshaamua, kwa ukabila twajua,
Sisi tumeendelea, bado tunalihofia ?
Si ukuu wa mkoa, nchi utakaojenga!

Ninaona ni hadaa, uchama kuendelea,
Wanachohofia, kuipoteza mikoa,
Upinzani kuitwaa, haraka ikajapaa,
Si ukuu wa mkoa, nchi utakaojenga!

Naanika si kuanua, wenyewe mtalijua,
Uchama kwetu tanzia, kifo unatuletea,
Ustawi unavia, hali wanajisifia,
Si ukuu wa mkoa, nchi utakaojenga!

Njaa yazidi kolea, shibe wanasimulia,
Kisha wanatushangaa, njaa kuitangazia,
Kwao sasa ni sanaa, mchezo wa kugiziwa,
Si ukuu wa mkoa, nchi utakaojenga!