Sunday, December 25, 2011

Unafiki haulipi

Haulipi unafiki, katika hii dunia,
Mola atakutalikia, ikawa fupi yako njia,
Ukija kutaharuki, umekwishaangamia,
Unafiki haulipi, duniani na akhera.

Ninakuomba Maliki, hili kutuepushia,
Tusiwe ni wanafiki, kisha kukutegemea,
Ya kwetu uyabariki, hadi utapotuchukua,
Unafiki haulipi, duniani na akhera.

Utupe yetu riziki, halali iliyokua,
Tusijefanya mikiki, vya wengine kuchukua,
Tusiwe haturidhiki, kwa kidogo kinapokua,
Unafiki haulipi, duniani na akhera.

Dunia tusimiliki, Uungu kuugombea,
Tugee yako ashiki, wewe kukung'ang'ania,
Inshallah mabruki, kwa ahaadi zilokua,
Unafiki haulipi, duniani na akhera.

Tusiichezee haki, hatiani kututia,
Tusikubali malaki, milioni kupotea,
Tuwatambue rafiki, ibilisi kumwambaa,
Unafiki haulipi, duniani na akhera.

Na wanaotudhihaki, wakweli tunaokua,
Tunakuomba Maliki, iwaaibishe dunia,
Hata tutakapofariki, wajukuu kushuhudia,
Unafiki haulipi, duniani na akhera.

Wa hariri si kaniki, huyo ni mwanaizaya,
Vizuri hatajiriki, ila kufuru kutia,
Nawe huwezi afiki, hukumu unaijua,
Unafiki haulipi, duniani na akhera.

No comments: