Monday, December 26, 2011

Huchelea la wokovu

Binadamu kumjua, bahati tunatumia,
Mgumju kumuelewa, moyoni yanayojaa,
Na unavyomdhania, ndivyo sivyo mara hua,
La wokofu huchelea, kila muogopa kifo!

Na ndivyo wanavyokua, unaotaka wafaa,
Iwe ni kuwaokoa, na dhiki unazojua,
Au balaa kuvaa, watakayoijutia,
La wokofu huchelea, kila muogopa kifo!

Wengi watakuhofia, wataka kuwachezea,
Husikiza ukajua, tayari wamesikia,
Kumbe hawakusikia, bado wanafikiria,
La wokofu huchelea, kila muogopa kifo!

Huchelea ya kufaa, tena ya kuwaongoa,
Mengine kuvamia, yatakayowaumbua,
Wakabaki washangaa, nusura kutoijua,
La wokofu huchelea, kila muogopa kifo!

Roho nimesharidhia, nasaha nitaitoa,
Na watakaosikia, sudi yao kusikia,
Wakiweza kutumia, watu huja kuwafaa,
La wokofu huchelea, kila muogopa kifo!

Waliokwishalaaniwa, jangwa ninawaachia,
Bure watanichukia, mengine wakidhania,
Ukweli wakiujua, watakuja nililia,
La wokofu huchelea, kila muogopa kifo!

Heri ninawatakia, kwa ukweli kuutoa,
Wao wanajihadaa, uongo kuutumia,
Blanketi la baa, maafa linaozua,
La wokofu huchelea, kila muogopa kifo!

Bure nisingejisumbua, ubaya ninaujua,
Nyuma ningeshaingia, na sifakuwasifia,
Na wao wakadhania, haki wanashikilia,
La wokofu huchelea, kila muogopa kifo!

Ila riha nakataa, na uongo kuzua,
Hata akiwa adawa, adili naangalia,
Na hao wasiojua, shetani awachezea,
La wokofu huchelea, kila muogopa kifo!

No comments: