Wednesday, December 14, 2011

Kwa kukosa uunngwana

Kwa kukosa uungwana, tutakuja kuuana,
Njiani kuvamiana, majumbani kwingiliana,
Amani itajanuna, paishe kuaminiana,
Tutakuja kuuana, kwa kukosa uungwana!

Mbona akili hatuna, twashindwa kuambiana,
Vituko twafanyiana, hata njiani mchana,
Uhuni ninaouona, amani sioni tena,
Tutakuja kuuana, kwa kukosa uungwana!

Misikitini kupona ninayo mashaka sana,
Na kanisani watuna, waanza kuburuzana,
Na nje wanaopangana, hakuna la muamana,
Tutakuja kuuana, kwa kukosa uungwana!

Na nje wanaopangana, hakuna la muamana,
Makelele twapigiana, hata kusali twabanwa,
Imani twafua sana, makali tutayaona,
Tutakuja kuuana, kwa kukosa uungwana!

Magari yanapishana, kelele kujibizana,
Promosheni zinafana, wanyonga uungwana,
Pongezi wapeana, majambia si mbali sana,
Tutakuja kuuana, kwa kukosa uungwana!

No comments: