Wednesday, December 28, 2011

Kumbukumbu ya Malenga

Ningekujawachukua, minghairi sikujua,
Akheri kufikiria, ritadi nikahofia,
Nchi mngeikimbia, kwa jinsi ilivyokua,
Kumbukumbu ya malenga, kilichobaki ukiwa!

Sanaa wanyanyapaa, hata serikali pia,
Bajeti waizuia, au inapanguliwa,
Baraza hoi jamaa, budi kuwahurumia,
Kumbukumbu ya malenga, kilichobaki uk

Ushairi wachukia, wahariri Tanzania,
Waandishi nao pia, kung'ong'a waamriwa,
Hapajawa Tanzania, mhariri mashairi,
Kumbukumbu ya malenga, kilichobaki ukiwa!

Ushairi wadhaniwa, ni ibada au dua,
Islamu unafaa, sio dini za judea,
Kiswahili nacho pia, ndio kisa chauawa,
Kumbukumbu ya malenga, kilichobaki ukiwa!

Shaaban Robert, kweli nakusimulia,
Kama ungelifufuliwa, kuishi ungekataa,
Lugha ulivyoshikilia, wangekukatisha nia,
Kumbukumbu ya malenga, kilichobaki ukiwa!

Amri Abeid pia, Mnyapala mngelia,
Kandoro mwenye kujua, ngonjera kuhadithia,
Hata nawe ungevia, kuishi kutorishia,
Kumbukumbu ya malenga, kilichobaki ukiwa!

Mbovu metuachia, kwa kuondoka Mochiwa,
Ushairi wateketea, hakuna wa kuokoa,
Maprofesa waduwaa, na walimu nao pia,
Kumbukumbu ya malenga, kilichobaki ukiwa!

Andanenga alijua, amebakia kulia,
UKUTA wabomoa, hapana pa kushikia,
Taasisi zinaliwa, hakuna zinachotoa,
Kumbukumbu ya malenga, kilichobaki ukiwa!

Ugenini chahamia, Kiswahili cha wazawa,
Ksnya wasbangilia, ufalme kuchukua,
Marekani nayo pia, nyuma haijachelewa,
Kumbukumbu ya malenga, kilichobaki ukiwa!

Japani wajivunia, Ujerumani wang'aa,
Uchina wakisikia, na Kusini wafundishia,
Uganda watangulia, nyuma yao twafatia,
Kumbukumbu ya malenga, kilichobaki ukiwa!

Burundi wajenga paa, Rwanda wameshapaua,
Ndiko watakakotokea, mabingwa watakaokuwa,
Kizazi cha kufatia, sisi tukiangalia,
Kumbukumbu ya malenga, kilichobaki ukiwa!

Kiswahili kinafia, hapa kilikozaliwa,
Hii yetu Tanzania, kizuri kisichojua,
Vya watu wang'ang'ania, hata kuzama nao pia,
Kumbukumbu ya malenga, kilichobaki ukiwa!

Majonzi yatabakia, msiba watangulia,
Kaburi kulichimbua, Kiswahili kuzikia,
Nendeni mkifurahia, mimi nimeshajitoa,
Kumbukumbu ya malenga, kilichobaki ukiwa!

Laana ninaikimbia, kizazi kitachojia,
Yenu ninawaachia, yangu ninayachukua,
Dunia kushuhudia, neno niliwaambia,
Kumbukumbu ya malenga, kilichobaki ukiwa!

© 2011 Sammy Makilla

No comments: