Sunday, December 25, 2011

Usije ukala moto

Kaizari anunua, kwa kodi anayopewa,
Wote wasiojijua, na rahisi kununua,
Dini walioingia, kushibisha zao njaa,
Usije uakala moto, kwa fedha za Kaizari!

Dini wamezivamia, ibilisi walokua,
Na ushehe wamepewa, hata tusiowajua,
Kumbe wote watumiwa, imani kuichafua,
Usije uakala moto, kwa fedha za Kaizari!

Elimu wasiokuwa, wala kufahamu dua,
Maimamu wamekua, wafuasi wapotea,
Giza nene laingia, kweusi tunakoelekea,
Usije uakala moto, kwa fedha za Kaizari!

Mola anayewachukia, hawa wanaonunuliwa,
Na wakubwa walokua, siasa wameingia,
Kama maboi wamekuwa, utumwa wa kununua,
Usije uakala moto, kwa fedha za Kaizari!

Wameacha mhofia, mletaji wa dunia,
Sasa wawatumikia, binadamu walokua,
Magoti wawapigia, wengine kuabudiwa,
Usije uakala moto, kwa fedha za Kaizari!

Laana zatunyemelea, tumgeukie Alaa,
Mabaya kuyakimbia, Sodomu yaliyovaa,
Na Gomorrah kutokea, nchi akazipindua,
Usije uakala moto, kwa fedha za Kaizari!

Serikali isokua, utoto ikabakia,
Kila mwaka yarudia, kule ilikotokea,
Weye ukiisifia, hakika umelaaniwa,
Usije uakala moto, kwa fedha za Kaizari!

Miaka ninaringia, nchi yangu kutetea,
Uhaini kutuhumiwa, ya rada nilipoyazua,
kazi yao kusingizia, mashetani walivyokua,
Usije uakala moto, kwa fedha za Kaizari!

Njia ningelizijua, ningeidai fidia,
Ila Mungu namwachia, mengine kunipatia,
Watu wakishaujua ukweli yangu ni sawa,
Usije uakala moto, kwa fedha za Kaizari!

No comments: