Monday, December 26, 2011

Mti usio na shina

Shina limeondolewa, ni matawi yabakia,
Hivi mti utakua, na matunda kuyatoa,
Ningali ninahofia, hatima mbaya yajia,
Mti usio na shina, matawi kuuokoa?

Dharuba naisikia, juu inakotgokea,
Gharika nalihofia, chini lajititimua,
Mti umening'inia, vipi utajiokoa?
Mti usio na shina, matawi kuuokoa?

Tumaini sijaona, wasiwasi umejaa,
Hapana pa kujibana, wala pa kushikilia,
Labda nguvu ya Rabana, mti ukauokoa,
Mti usio na shina, matawi kuuokoa?

Wenyewe ulijiona, pekee uliokua,
Na haukushirikiana, na jirani walokua,
Hapakuwa muamana, kila kitu kuchukua,
Mti usio na shina, matawi kuuokoa?

Kimzani ulituna, kama sio kunona,
Ukiritimba hiyana, ukawa wake mwamana,
Na yanaposhindikana, sasa ni kutafutana,
Mti usio na shina, matawi kuuokoa?

Watu wanamalizana, ngawira kuja gawana,
Huku wajifanya wana, na baba hawakumuona,
Na majina wapeana, ukoo kujulikana,
Mti usio na shinda, matawi kuuokoa?

Ila haijajulikana, tufani inavyokazana,
Kama kuna kuokoana, au chini kutupana,
Nani kuangalizana, salamawaje iona,
Mti usio na shinda, matawi kuuokoa?

Siwezi zaidi nena, mimi siye ninayejua
Nahofia mame wana, chakula kutoungua,
Bei kimepanda sana, twaweza lala lna njaa,
Mti usio na shinda, matawi kuuokoa?

No comments: