Monday, December 26, 2011

Kiongozi mbaya heri

Kwa wasiojitambua, hudhani wamelaniwa,
Mbaya wanapopewa, kiongozi alokua,
Kisirani kikakua, na nia zikawa mbaya,
Kiongozi mbaya heri, mzuri ndipo hutafutwa!

Kiongozi mkipewa, kama Sauli akawa,
Kwa wanaojua biblia, torati kujisomea,
Zaburi haikukawia, maneno nayo yatia,
Kiongozi mbaya heri, mzuri ndipo hutafutwa!

Daudi alipokuwa, ngazi hakupigania,
Moyo ulimtulia, ya bwana akingojea,
Ila ilipofikia, mawili yote kapewa,
Kiongozi mbaya heri, mzuri ndipo hutafutwa!

Sauli alizidia, kwa dhuluma na ubaya,
Mola akamsanzua, Daudi kumchagua,
Ufalme akatwaa, na unabii kupewa,
Kiongozi mbaya heri, mzuri ndipo hutafutwa!

Kiongozi mbaya heri, mzuri ndipo hutafutwa!

Nchi ikatengemaa, na uovu kupungua,
Heri haikumbia, bali kuwakimbilia,
Uyahudi ikakua, na mipaka kupanua,
Kiongozi mbaya heri, mzuri ndipo hutafutwa!

Nchi ikijaliwa, kiongozi asofaa,
Ukubwa nayo tamaa, ikawa ni yake nia,
Asifanye cha kufaa, na watu kudidimia,
Kiongozi mbaya heri, mzuri ndipo hutafutwa!

Watu wakijitambua, na Mola kumgeukia,
Dini zikidhamiria, ibada zikachanua,
Mola atawasikia, na majibu kuyatoa,
Kiongozi mbaya heri, mzuri ndipo hutafutwa!

Yarabi twakulilia, kuangalia wasaa,
Ni wewe unayejua, si wafanzao kujua,
Huruma twaingojea, afu kuonyesha njia,
Kiongozi mbaya heri, mzuri ndipo hutafutwa!

No comments: