Wednesday, December 28, 2011

Mzungu twampa dhahabu

Pu nguani wadhania, viongozi walokua,
Dhahabu tunaitoa, peremende twachukua,
Kusoma tumefulia, uchumi tunaogea,
Mzungu twampa dhahabu, sisi twakubali pipi!

Mababu hawakujua, sisi mbona tunajua,
Bado tunaendelea, na ileile tabia,
Hakika ninashangaa, viranja sijawajua,
Mzungu twampa dhahabu, sisi twakubali pipi!

Ni njaa yawasumbua, au wajinga majuha,
Mchele watoa gunia, wapokea kitumbua?
Hii laana imekua, mkono wa mtu nahofia,
Mzungu twampa dhahabu, sisi twakubali pipi!

Pamba bure unagawa, mtumba unanunua,
Miwa unaiachia, sukari nyeupe wapewa?
Sumu iliyokwishajaa, kifo hujakihofia,
Mzungu twampa dhahabu, sisi twakubali pipi!

Magurudumu bidhaa, mpira twajiuzia,
Madini twawaachia, wengine kujichimbia,
Wasomi tuliotoa, nje wameshahamia,
Mzungu twampa dhahabu, sisi twakubali pipi!

Wazungu sasa wajaa, tarafu wasiokua,
Amerika na Ulaya, utazoa kwa gunia,
Twabaki twashangaa, badala kuwachukua,
Mzungu twampa dhahabu, sisi twakubali pipi!

Reli kuja kufufua, na ndege zetu nazo pia,
Bandari kujijengea, watu wetu kutumia,
Akili ikilemaa, bofra mwili kulemaa,
Mzungu twampa dhahabu, sisi twakubali pipi!

Wasomi nje wajaa, kazi wanazililia,
Ukienda wachkua, viwanda utainua,
Na nchi juu ikawa, ya pili kwenye dunia,
Mzungu twampa dhahabu, sisi twakubali pipi!

Matatizo wangeondoa, na nchi kujitanua,
Akili wangezinoa, uburu ukajifia,
Tuanze kujichongea, mengi yenye kutufaa,
Mzungu twampa dhahabu, sisi twakubali pipi!

Uongozi twahofia, kulogwa uliokua,
Huna unalolijua, ila siasa kugwaya,
Nchi inadidimia, na wao washindilia,
Mzungu twampa dhahabu, sisi twakubali pipi!

© 2011 Sammy Makilla

No comments: