Friday, December 16, 2011

Huja yakasimuliwa

Maamuzi twayatoa, hatma tunaijua,
Huja yakasimuliwa, wakati tushajifia!

Mazuri yaliyokuwa,watu watayasifia,
Na mabaya yalokua, tutajakulaumiwa.

Akili tukijitia, wengine zimezidia,
Ni hali yawazuia, wangeweza tuumbua.

Faraghani huingia, tukayazungumzia,
Wazi yaliyotakiwa, maamuzi kufanyiwa.

Na kila mwenye kujua, uchuro anaujua,
Na kisa cha siri kua, si siri kwa wanaojua.

Ikiwa chama chajua, viongozi waridhia,
Dhambi mnayojaliwa, ya jumla itakuwa.

Na serikali ikiwa, yatenda inayojua,
Na dhuluma waijua, basi nayo hulaaniwa.

Viongozi wangejua, motoni wataingia,
Na hili wakahofia, pepo 'ngekuwa dunia.

Ila wengi waamua, ni pepo yao dunia,
Hakuna wa kusikia, kumbikumbi akipaa.

Dunia yaendelea, na nchi yazidi kua,
Huja yakasimuliwa, yote tunayoamua!

Tungo mpya 2011
Aina: Mbilia
© 2011 Sammy Makilla

No comments: