Monday, December 26, 2011

Chama chabaki matawi

Matawi yamebakia, mizizi wameing'oa,
Swali linanivamia, kuwepo kitaendelea?
Na wanaoning'inia, ni hao wa kulipiwa,
Chama chabaki matawi, mizizi wamesanzua!

Chama juu chaanzia, kura kujitafutia,
Mizizi haikukua, kwani haikujiotea,
Wajanja walishang'oa, walokuwa haramia,
Chama chabaki matawi, mizizi wamesanzua!

Chama kimechukuliwa, na wasokuwa wazawa,
Kwa malengo fisadia, watu na nchi kuvia,
Wakaneemeka wazoa, na wanaowapigania,
Chama chabaki matawi, mizizi wamesanzua!

Wakubwa wamepokea, hicho walichokipewa,
Pembeni wakasogea, vyao kwao kuanzia,
Mengi wamejijgengea, kama sio kukupua,
Chama chabaki matawi, mizizi wamesanzua!

Chini wameachiwa, vidogo kuvitumia
Hakuna kinachoingia, chama kikakitumia
Vyote watu hujilia, na juu kuongezewa,
Chama chabaki matawi, mizizi wamesanzua!

Kikichwa kinachokua, ni nani anakitoa,
Nini anajipatia, na vipi asaidia,
Au tumeishanunuliwa, jina tu linabakia?
Chama chabaki matawi, mizizi wamesanzua!

Na macho tusipokua, wallahi tutaumia,
Kifo hatutakijia, saa kitakapotokea,
Hugeukwa na wategemewa, tukabaki tunalia,
Chama chabaki matawi, mizizi wamesanzua!

No comments: