Friday, December 23, 2011

Kuku hawezi pigana

Wagonjwa Watanzania, wabunge wao wazima,
Kisha njaa imeingia, raia tukawatuma,
Kwenda kutupigania, iongezeke neema,
Kuku hawezi pigana, na kuku anayeumwa.

Ghafla wameamua, kujipa wao heshima,
Nafsi kuzifutua, kama sawaka wavuma,
Ulaji wapigania, hali wengine twazama,
Kuku hawezi pigana, na kuku anayeumwa.

Hicho wanachochangia, kibaba sio kizima,
Chazidi tena pungua, kwa balaa na unyama,
Watu wakiwaambia, huwatoroka huruma,
Kuku hawezi pigana, na kuku anayeumwa.

Kuku ninashuhudia, amezidi kwa huruma,
Mwenzie akiugua, hamfanzii hasama,
Naye kimya huugua, akamtakia uzima,
Kuku hawezi pigana, na kuku anayeumwa.

Wabunge wetu balaa, ya mamba yao huruma,
Nafsi zimewajaa, hawaangalii nyuma,
Sasa ni kama kinyaa, walivyo nchi nzima,
Kuku hawezi pigana, na kuku anayeumwa.

Wanazidi kubugia, sahani mbili nzima,
Wengi tonge twalilia, hatujaliona sima,
Hakika wanatugawa, tena kwa kubwa dhuluma,
Kuku hawezi pigana, na kuku anayeumwa.

Huchakura kuchagua, mgonjwa akimtazama,
Hulia na kumwambia, kula kitu cha lazima,
Jikaze na kumegea, upate tena uzima,
Kuku hawezi pigana, na kuku anayeumwa.

Wabunge wetu balaa, roho zetu wasakama,
Wenyewe wajiangalia, hakuna mtazama nyuma,
Tunazidi didimia, wao wazidi kuchuma,
Kuku hawezi pigana, na kuku anayeumwa.

Hawa kuwanyanyapaa, iwe ni yetu azma,
Si wa kuwategemea, hawa watu wa nakama,
Na tena tukichagua, tuogope chao chama,
Kuku hawezi pigana, na kuku anayeumwa.

© 2011 Sammy Makilla

No comments: