Wednesday, December 28, 2011

Ya wezi kaziye wizi

ZIMEFIKA zama hizi, hadhi wawe nayo wezi,
Na wakubwa majambazi, inshallah viongozi,
Walinzi wawe mijizi, wenye sheria hifadhi,
Mamlaka kama jizi, ya wezi kaziye wizi !

Na wa dini viongozi, kugeuka walanguzi,
Dini ziwe uchuuzi, bidhaa na matanuzi,
Busara iwe masinzi, na hekima kuwa nazi,
Mamlaka kama jizi, ya wezi kaziye wizi !

Malaya wawe wajuzi, wa kazi sio mapenzi,
Vyeo viwe fumanizi, wanone kimaangamizi,
Watajileta mabuzi, kuchinjwa kwenye makazi,
Mamlaka kama jizi, ya wezi kaziye wizi !

Ujaji huwa ni vazi, si utenzi bali hadhi,
Haki wawe wachuuzi, na wa chini dumuzi,
Yakaenea maradhi, pasiwe nayo hifadhi,
Mamlaka kama jizi, ya wezi kaziye wizi !

Wajinga wapewe kazi, na pengine uongozi,
Kazini kupanda ngazi, iwe kama utelezi,
Ufanisi jinamizi, kuzama isiwe kazi,
Mamlaka kma jizi, ya wezi kaziye wizi !

Waandishi na watunzi, wawe kwao waigizi,
Uongo waudarizi, liwe lao kuu vazi,
Keki likawa andazi, fumanizi, ugunduzi,
Mamlaka kama jizi, ya wezi kaziye wizi !

Urongo uwe ujuzi, wautaka viongozi,
Na umma kuwa zoezi, hadaa kuzimaizi,
Nchi isiwe majazi, bali shari na ajizi,
Mamlaka kama jizi, ya wezi kaziye wizi !

Kipendwacho kukabidhi, nusu yake maamuzi,
Ikafanza matanuzi, pato lenye ubaguzi,
Walewe utandawazi, na wa nje majambazi,
Mamlaka kma jizi, ya wezi kaziye wizi !

Huchaguliwa viazi, vikapika maandazi,
Na wasioenda kozi, wakawa ni wakufunzi,
Viatu kuwa kubadhi, wakavaa wanawenzi,
Mamlaka kama jizi, ya wezi kaziye wizi !

Wenye hoja kuwa mbuzi, waheshimiwa kwa ngozi,
Yakakwama mageuzi, uchama kushika uzi,
Tozo hili hatutozi, wajao watamaizi,
Mamlaka kama jizi, ya wezi kaziye wizi !

© 2011 Sammy Makilla

No comments: