Friday, December 16, 2011

Usinihini wajihi

Jioni na asubuhi, ninaloomba daima,
Usininyime wajihi, jua litakapoinama,
Niepushe makuruhi, mwezi utakapoinama,
Usinihini wajihi, Baqi siku ya kiyama!

Niikose staftahi, na kula iwe zahama,
Ila naomba yaillahi, usiache nitazama,
Ibilisi nimuwahi, sikuzote awe nyuma,
Usinihini wajihi, Baqi siku ya kiyama!

Nawaomba manabii, na mlio waadhama,
Kesho yangu siijui, mnisomee dua njema,
Nikiacha ardhi hii, nijikute ni salama,
Usinihini wajihi, Baqi siku ya kiyama!

Ni maombi si madai, nakusihi Yakarima,
Ibrahim natwii, kwayo uliyonituma,
Heri yako sikinai, hadi siku ya kiyama,
Usinihini wajihi, Baqi siku ya kiyama!


© 2011 Sammy Makilla

No comments: