Sunday, December 25, 2011

Historia inaishi

Haifutiki historia, japo huchakachuliwa,
Mkoloni katugawa, wenzetu naye wakawa,
Uhuru kupigania, wenyewe tukabakia,
Historia inaishi, yaja wengi kuumbua!

Manasra wanajua, vita walivikimbia,
Mwingereza kumvaa, hawakuwa nayo nia,
Dini moja walikua, kwalo hilo wakagwaya,
Historia inaishi, yaja wengi kuumbua!

Lakini walishajua, mzungu kamwandaa,
Msomi mwenye kujua, ndiye watamwachia,
Sisi mkenge kwingia, ukubwa tukamwachia,
Historia inaishi, yaja wengi kuumbua!

Nyerere kaanzia, udikteta kujua,
Tulipomfikiria, mwislamu atakua,
Kumbe sio yake nia, ukubwa auwania,
Historia inaishi, yaja wengi kuumbua!

Wenzie sisi tukawa, manasra wakimbia,
Hadi nchi kuchukua, wote wakamrudia,
Ndivyo walivyomhadaa, nchi wakaichukua,
Historia inaishi, yaja wengi kuumbua!

Wale walioumia, kitu hawakuambulia,
Taasisi kaziua, hakuna kilichobakia,
Umoja akatumia, BAKWATA kutuhadaa,
Historia inaishi, yaja wengi kuumbua!

Hadi leo tunalia, waumini twapotea,
Umoja umesinyaa, na mambo yetu yavia,
Ilitujua dunia, sasa tumefukiwa,
Historia inaishi, yaja wengi kuumbua!

Welfeya twaililia, hapa tusingelikua,
ICO wazuia, kuingia wakataa,
Fedha wanauibiya, kila tunapotumiwa,
Historia inaishi, yaja wengi kuumbua!

Kazi iliyobakia, kuamka Tanzania,
Islamu kukataa, kugawanywa na wabia,
Na elimu kufukua, watoto kujipatia,
Historia inaishi, yaja wengi kuumbua!

Mitaji kuichipua, kisha tukaigawa,
Zaka yetu kutumia, Mola keshatwandikia,
Wote tukawanyanyua, nchi kuja kuchukua,
Historia inaishi, yaja wengi kuumbua!

Hii iwe yetu nia, toka tunapozaliwa,
Umaskini kukataa, ni ufakiri balaa,
Motoni utatutia, Mungu hatutamjua,
Historia inaishi, yaja wengi kuumbua!

No comments: