Friday, December 16, 2011

Wawashikao wakubwa

Mbeleko walofungiwa, mgongoni wakakaa,
Budi kujishikilia, kifua kutoachia,
Matuta huja fikiwa, na mashimo kuvamiwa,
Wawashikaowakubwa, huondoka na wakubwa!

Bahari kweli hujaa, na kupwa kunafatia,
Kutoka na kuingia, huwa hiyohiyo njia,
Na neema na balaa, ni hiyohiyo jamaa,
Wawashikao wakubwa, huondoka na wakubwa!

Mbebwapo shikilia, na sio kuning'inia,
Ukila unavyopewa, vichungu hutochukia,
Na juu ukishapaa, si vibaya kutambaa,
Wawashikao wakubwa, huondoka na wakubwa!

Ukibebwa zingatia, kushushwa itafikia,
Salama utagundua, taratibu kujiachia,
Na kujenga mazoea, hali kutokukataa,
Wawashikaowakubwa, huondoka na wakubwa!

No comments: