Sunday, September 26, 2010

Kiongozi hamjui mwenye dhiki

Unaishi kwenye nyumba ya fahari,
Ewe kiongozi mwema wa wanadamu,
Wananchi wako ijapo ni hodari,
nyumba bora kwao bado ni kitu adimu,
Stima yakupa kila akheri na bukheri,
watu wako hawaishi kulaumu,
Uhuru zama uliwapa kiasi jeuri,
leo nyuso zakunjika kama ndimu,
Hawasikilizi la kheri wala la shari,
Bei kila leo zinawahasimu,
Husikilizi kabisa wao ushauri,
ila ule tu wa wataalamu,
Wanaotaka aghalabu ughaibu,
na wasiotofautisha sifuri na dhahiri,
Ndio hao sasa wanaotakadamu,
na bora kwako ni wa kwao ushauri,
Wengine wameanza kuwatuhumu,
magari, safari na nyumba ndogo utitiri,
Badala sasa ya nyie kuombewa heri,
watu kulia na kushoto wawaombea shari,
Naomba wakubwa wangu msinilaumu,
Ujumbe huu nimetumwa nami si mtabiri!

Siasa zetu nyang'anyi

Siasa zetu nyan'anyi, zinatupora uwezo,
Watawala sio nyinyi, mmefanya pandikizo,
Mmejipa na umwinyi, na kuviweka vikwazo,
Siasa zetu nyang'anyi, zinatupora imani !

Wananchi hamnyang'anyi, ilokuwa yenu tunzo,
Mwawaachia wanyonyi, wapita mfululizo,
Na wala hamuwakanyi, waona kama mchezo,
Siasa zetu nyang'anyi, zinatupora imani !
Eti hawatudanganyi, wakati nyie igizo,
Na wala hamuwasunyi, mnawapa madekezo,
Ugonjwa hamuuponyi, mnaongeza mizozo,
Siasa zetu nyang'anyi, zinatupora imani !

Wananchi ndio mamwinyi, wengineo mikwaruzo,
Ukubwa hawakusanyi, ila kama ni tangaZO,
Na kitu hawakifanyi, kuondoa matatizo,
Siasa zetu nyang'anyi, zinatupora imani !

Nguvu hatuzigawanyi, waziiba mzomzo,
Na nchi haichanganyi, kwa kukosa shinikizo
Maduhuli hatukusanyi, utapiamlo wa mawazo,
Siasa zetu nyang'anyi, zinatupora imani !

Tuache unyang'anyi, watu wawe na uwezo,
Chenu hatuwapokonyi, wala hapana mabezo,
Nchi ni usisi si unyinyi, liote kwenye mawazo,
Siasa zetu nyang'anyi, zinatupora imani !

Hii bado Afrika

Wazungu wanayopika, kwetu vigumu kulika,
Ila njaa imetushika, sasa tunalazimika,
Na mwishowe tutatapika, na hapa hapatakalika,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Dini sisi tumeshika, twaogopa kulanika,
Hicho wanachokitaka, Ulaya na Amerika,
Yafaa kueleweka, kisiivuke mipaka,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Paspoti ya kuvuka, isiwe kwa yao sadaka,
Utamaduni hakika, wetu umeshajengeka,
Ukija kuporomoka, mabaya yatatufika,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Mwanamme hajaposeka, achia kuoleweka
Na dini zinatutaka, hili kutokubalika,
Huo wao ufuska, tusije shawishika,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Mwanamme Afrika, yake yanaeleweka,
Kisha hali kadhalika, mwanamke aitika,
Na ndani kuna mipaka, majukumu kuyashika,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Biblia yasomeka, na haya yatambulika,
Kurani yanatajika, muumini waridhika,
Ila wanaohangaika, wa wazungu vibaraka,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Mapinduzi twayataka, sio ya nguo kuzuka,
Ustawi twautaka, sio wa kuvurugika,
Usawa una mipaka, kwingine huwezi fika,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Mke wangu namshika, na wote tunanyanyuka,
Mipaka hajaivuka, na kwangu aheshimika,
Na simba hajawa paka, mwisho panya kugeuka,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Hii bado Afrika, Wazungu ninatamka,
Yenu yasiyoeleweka, huko huko mgeshika,
Hamnayo madaraka, kutuuzia talaka,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Ulaya mlisifika, kwa wake kunyanyasika,
Mkawata kwa mashoka, mashgoa waliozuka.
Na sio mingi miaka, hili linatambulika
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Nafasi tunaitaka, na ya kwetu kupangika,
Mwajua tunayoyataka, unyonyaji kufutika,
Na malengo ya kuvuka, ufukara kufutika,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Mengine yatafikika, taratibu tukitaka,
Hatua zitavukika, hadi malengo kufika,
Iamue Afrika, si nyie kuamulika,
Hii bado Afrika, msiivuke mipaka !

Sijakuelewa

Kuna kitu wanambia, nashindwa soma ishara,
Sauti hujaitoa, ninakuona kwa sura,
Kila nikikuangalia, ninahisi taathira,
Mbona sijakuelewa, siwezi soma ishara !

Mboni nimeyafungua, ninaiona taswira,
Ila bado kulijua, mwenzi linalokukera,
Macho yananambia, masikio yadorora,
Mbona sijakuelewa, siwezi soma ishara !

Ningekuwa natambua, anga ningeisakura,
Ulilo nalo kulijua, usiipate hasara,
Namii ningekusaidia, tena bila ya papara,
Mbona sijakuelewa, siwezi soma ishara !

Sauti ingeitoa, ningelitafuta dira,
Alama ungezitoa, maana ningeichora,
Jicho lingelibonyea, nisingefanya papara,
Mbona sijakuelewa, siwezi soma ishara !

Ishara yako ya kimya, naona kama ibura,
Na nikahi waivaa, sijaona yako sura,
Laiti ungeliivua, nje ya hii hadhira....
Mbona sijakuelewa, siwezi soma ishara !

Kucheza ninazurura, mgumu huu mpira,
Wapi kuupelekeza, kulipata goli bora?
Nimebaki nazubaa, wengine watanipora,
Mbona sijakuelewa, siwezi soma ishara !

Mnaoenzi Kiswahili

Ni redio duniani, vinara utandawazi,
Na kote ulimwenguni,wanahabari azizi,
Watupasha kwa yakini, katika utandawazi,
Tunawapeni pongezi, mnaoenzi Kiswahili!

BBC Ulimwenguni, mwastahili pongezi,
Aidha Ujerumani, mfanyayo si ajizi,
Na Wahindi kwa yakini, wanalfanya zoezi,
Tunawapeni pongezi, mnaoenzi Kiswahili!

Twaisifu Marekani, wanaongeza ujuzi,
Mchina twamthamini, japoe amekuja juzi,
Kiswahili ni auni, habari mnanukuzi,
Tunawapeni pongezi, mnaoenzi Kiswahili!

Afrika ya Kusini, hili nalo mwamaizi,
Nguvu zenu ongezeni, Kiswahili kukienzi,
Afrika itawini, uondoke ubaguzi,
Tunawapeni pongezi, mnaoenzi Kiswahili!

TBC amkeni, idhaa ziote mizizi,
Mwepo ulimwenguni, mwasikika waziwazi,
Kutangaza kila fani, lugha mfanye azizi,
Tunawapeni pongezi, mnaoenzi Kiswahili!

Nne na ishirini, habari mzidarizi,
Na michezo iwekeni, chaneli ya simulizi,
Filamu zionesheni, Afrika imaizi,
Tunawapeni pongezi, mnaoenzi Kiswahili!

Muziki uwe makini, chaneli ya matanuzi,
Kwa nyimbo kamateni, chote Afrika kizazi,
Tuwe kama Marekani, kwa Afrika kutuenzi,
Tunawapeni pongezi, mnaoenzi Kiswahili!

Mnaoenzi Kiswahili

Ni redio duniani, vinara utandawazi,
Na kote ulimwenguni,wanahabari azizi,
Watupasha kwa yakini, katika utandawazi,
Tunawapeni pongezi, mnaoenzi Kiswahili!

BBC Ulimwenguni, mwastahili pongezi,
Aidha Ujerumani, mfanyayo si ajizi,
Na Wahindi kwa yakini, wanalfanya zoezi,
Tunawapeni pongezi, mnaoenzi Kiswahili!

Twaisifu Marekani, wanaongeza ujuzi,
Mchina twamthamini, japoe amekuja juzi,
Kiswahili ni auni, habari mnanukuzi,
Tunawapeni pongezi, mnaoenzi Kiswahili!

Afrika ya Kusini, hili nalo mwamaizi,
Nguvu zenu ongezeni, Kiswahili kukienzi,
Afrika itawini, uondoke ubaguzi,
Tunawapeni pongezi, mnaoenzi Kiswahili!

TBC amkeni, idhaa ziote mizizi,
Mwepo ulimwenguni, mwasikika waziwazi,
Kutangaza kila fani, lugha mfanye azizi,
Tunawapeni pongezi, mnaoenzi Kiswahili!

Nne na ishirini, habari mzidarizi,
Na michezo iwekeni, chaneli ya simulizi,
Filamu zionesheni, Afrika imaizi,
Tunawapeni pongezi, mnaoenzi Kiswahili!

Muziki uwe makini, chaneli ya matanuzi,
Kwa nyimbo kamateni, chote Afrika kizazi,
Tuwe kama Marekani, kwa Afrika kutuenzi,
Tunawapeni pongezi, mnaoenzi Kiswahili!

Mtunukiwa Nobeli

Yangu lugha Kiswahili, nataka niipepete,
Hadi nipate Nobeli, wenye nasibu nifwate,
Waliokwishatawakali, nikae nao nitete,
Ninakumezea mate, mtunukiwa Nobeli!

Naitamani Nobeli, hakika kimeremete,
Kipanuke kiswahili, Afrika wakipate,
Tuzinoe na akili, teknolojia tulete,
Ninakumezea mate, mtunukiwa Nobeli!

Ni elimu Kiswahili, hazina kwa dhana zote,
Chekechea chahimili, muhibu kwa fani zote,
Hadi kwenye Uzamili, hata kwa shahada tete,
Ninakumezea mate, mtunukiwa Nobeli!

Hauwezi kunakili, lugha ya chuma ulete,
Hao sasa mabahili, wataka tuwe viwete,
Wakishatumaliza mwili, akili zite tekete,
Ninakumezea mate, mtunukiwa Nobeli!

Japani wastahili, siri yao tupakate,
Ni kikwao kwa asili, si Kiingereza watete,
China nao ni muhali, lugha nyingine ipete,
Ninakumezea mate, mtunukiwa Nobeli!

Norwei ama kweli, milioni nne wote,
Wana chao Kiswahili, lingine usiwasute,
Na sasa sio dhalili, nani juu awakute,
Ninakumezea mate, mtunukiwa Nobeli!

Lugha hii mwanamwali, wanaume watafute,
Itatupa afadhali, mengi sana tuyalete,
Kwa kutumia akili, si kwa kuiga tuvute,
Ninakumezea mate, mtunukiwa Nobeli!

Ninaiona amali, Kiswahili kitakate,
Ila dhoofu wa hali, legelege saa zote,
Wanangoja ufadhili, mapya mhali walete,
Ninakumezea mate, mtunukiwa Nobeli!

Nitafanza kulhali, lugha yetu ivukute,
Kinamama na rijali, elimu wote wapate,
Kwa lugha ya Kiswahili, na zingine wazitete,
Ninakumezea mate, mtunukiwa Nobeli!

Hakika ubaradhuli, lugha za watu tufate,
Tunakuwa madalali, kuwapa wengine kete,
Mchina keshawasili, je, ni Kichina tukitete ?
Ninakumezea mate, mtunukiwa Nobeli!

Mhindi anahimili, je, ni kIhindi tukivute ?
Mtashindwa pilipili, mbaki mwatema mate,
Sura mkazibadili, wajihi muukung'ute,
Ninakumezea mate, mtunukiwa Nobeli!

KWETU KUPENDWE KWANZA

NCHI kuiendeleza, ni watu kuwanyanyua,
Kwanza ukawatanguliza, vingine vikafuatia,
Huwezi haya kufanza, mzawa nyuma akiwa,
Wakwetu wapendwe kwanza, ndiyo mbegu ya ustawi.

Kiongozi mjikweza, yeye akatangulia,
Hata angelihimiza,hawezi kufanikiwa,
Nchi ataipoteza,jangwani ikabakia,
Wakwetu wapendwe kwanza, ndiyo mbegu ya ustawi.

Wageni ukiwakuza, wao wakatangulia,
Nchi utaidumaza,na mwishowe kudidimia,
Hao si watu wa kukwazwa,mwishowe hujiondokea,
Wakwetu wapendwe kwanza, ndiyo mbegu ya ustawi.

Uzawa wanaobeza, dunia hawajaijua,
Huwezi kujiegemeza,kwa huyu mpita njia,
Nendeni mkichunguza,popote kwenye dunia,
Wakwetu wapendwe kwanza, ndiyo mbegu ya ustawi.

Watu anayepuuza, kuwadharau wazawa,
Ni kiongozi wa giza,kapewa bahati mbaya,
Ni chakula cha mafunza, jina lake litaliwa,
Wakwetu wapendwe kwanza, ndiyo mbegu ya ustawi.

Mzungu si mwanawenza, bure kumtumainia,
Na wengine wachuuza, Uchina pia India,
Mzawa akiwa kwanza, huna kinachopotea,
Wakwetu wapendwe kwanza, ndiyo mbegu ya ustawi.

Mteza kwao hutunzwa, wahenga watwambia,
Hili kaa waliwaza, akilini kuingia,
Nchi bora hufanyiza, watu wakaifurahia,
Wakwetu wapendwe kwanza, ndiyo mbegu ya ustawi.

Mkaa na mjibanza, hawajatufanania,
Na chungwa haliwi chenza,na utamu sio sawa,
Na asiyemjua pweza,kitoweo hukataa,
Wakwetu wapendwe kwanza, ndiyo mbegu ya ustawi.

Nyenzo tunayoiwaza, si mtu kumchukua,
Ni akili kufyonza,wajualo tukajua,
Ganda ukishamenyeza,mbali utalitupilia,
Wakwetu wapendwe kwanza, ndiyo mbegu ya ustawi.

Ustawi utaanza, wetu tukiwatambua,
Wakawa wanaoongoza, na wageni waajiriwa,
Hawawezi kuongoza, wasiokuwa wazawa,
Wakwetu wapendwe kwanza, ndiyo mbegu ya ustawi.

Kama nchi kuongoza, lazima awe raia,
Ajabu tunaifanza, uchumi nje kugawa,
Kama tumepatilizwa,hatujui cha kutoa,
Wakwetu wapendwe kwanza, ndiyo mbegu ya ustawi.

Mabingwa wanajiuza, kazi wanaozijua,
Hata wa Uingereza, twaweza kuwachukua,
Urussi huwezi saza,pamwe nako Romania,
Wakwetu wapendwe kwanza, ndiyo mbegu ya ustawi.

Rejeeni Afrika

Sasa hamthaminiki, wao wameshatosheka,
Ukwasi si yao miliki, hata sisi tunajengeka,
Wazungu muwataliki, ndoa mpya kufungika,
Ikiwa hawawataki, rejeeni Afrika !

Uchumi wamehiliki, vigumu wataokoka,
Sasa wawa wazandiki, wageni wadhulumika,
Yakini hawawataki, chanzo hawajakishika,
Ikiwa hawawataki, rejeeni Afrika !

Kazi zinawadhihaki, masoko yanatoweka,
Bei zinawashtaki, mali ghafi imeruka,
Mishahara haishikiki, mambo yanaharibika,
Ikiwa hawawataki, rejeeni Afrika !

Uzalishaji mikiki, hakuna kinachotoka,
Wachina watamalaki, Mzungu anatishika,
Azidi uza bunduki, Mhindi anamcheka,
Ikiwa hawawataki, rejeeni Afrika !

Makaburi ya Hilaki, Ulaya yanachibika,
Ni kweupe Mashariki, Magharibi yashtuka,
Chai isiyoiliki, itaanza kunyweeka,
Ikiwa hawawataki, rejeeni Afrika !

Nduguze hawawataki, sembuse Waafrika,
Ufaransa tahamaki, Gipsi yalowafika,
Mwingereza hamtaki, Mpolishi kamchoka,
Ikiwa hawawataki, rejeeni Afrika !

Haya msiyadhihaki, yatakuja kuwafika,
Mzungu haaminiki, hali ikiwa mashaka,
Unakwisha urafiki, uadui kujengeka,
Ikiwa hawawataki, rejeeni Afrika !

Sasa hakieleweki, Ulaya imechafuka,
Mungu bara libariki, warudi waliotoka,
Tujenge mpya milki, kote ikatambulika,

Weupe ukiupenda

Binadamu kama nunda, kazi kustaarabika,
Mwenyewe anajiponda, hawezi kustahika,
Ni mwepesi kwa kuvunda, pasiwwe anayemtaka,
Weupe ukiupenda, weusi hudhalilika.

Weupe ukijisunda, weusi hautaushika,
Ukikutoka udenda,ving'aravyo kupendeka,
Weusi utakushinda,katu hautathaminika,
Weupe ukiupenda, weusi hudhalilika.

Na mkubwa kwa kutenda, viongozi Afrika,
Uti umeshawapinda,vyao kutokuthaminika,
Zimwi wanayemuunda,ndiye huja kuwazika,
Weupe ukiupenda, weusi hudhalilika.

Akili hazijasarenda,mtunzi bado nakoka,
Si wote kuheshimika,wengine hao wavunda,
Mzima havai sanda, ila aliyelaanika,
Weupe ukiupenda, weusi hudhalilika.

Weupe mnaopenda,ndo kamba ina kiraka,
Na pale ulipopinda,ndipo utapokatika,
Sio kazi yake randa,kabati kuunganika,
Weupe ukiupenda, weusi hudhalilika.

Umesheheni vidonda,weupe hutofumbatika,
Haujakivika chanda,pete isochukulika,
Na hawa sio ya kutanda,pasipo kuthaminka,
Weupe ukiupenda, weusi hudhalilika.

Hilo tisa bado kenda, okota cha kupukutika,
Haushikiki mlenda,bila ya kubwabwajika,
Nchi bora hujaunda,pasipo ya Mwafrika,
Weupe ukiupenda, weusi hudhalilika.

Chetu lazima kupenda, na kwetu kukapendeka,
Kama hili hamkufundwa, taifa litaanguka,
Hakuna wa kutupenda, wenyewe tusipojitaka,
Weupe ukiupenda, weusi hudhalilika.

Hata ukiwa tajiri

Hili nimetafakari, nakuiona shajara,
Wengi limewaadhiri,wanapokwenda zurura,
Wote wakatahayari,waonapo taathira,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.


Ni wa ovyo ufahari, mtu wa nchi fukara,
Wewe ni mtu wa shari,katika yao hadhira,
Huwa hawafanyi siri,kila kona hukuchora,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Rais au waziri, nyie nyote mafukara,
Lala hoteli mashuhuri,ni mwizi zao fikira,
Panda gari la fahari,trafiki hulipora,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Helikopta safiri, na ndege iwe tiara,
Bado hawakustiri, kwao ungali fukara,
Fanya uwezayo kheri,wewe mtu wa hasara,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Wapo wetu matajiri, nje huenda ziara,
Waulize kwa urari, huikunja yao sura,
Wazungu huwaadhiri,wakajiona majura,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Fukara wewe tajiri, nchi yako yasakura,
Kokote ukiabiri,hilo halina stara,
Katika zako safari,jua hili si bishara,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Huonekana ghururi,mtu asothaminika,
Thamani yake sifuri, tena hajakamilika,
Mustakabaliwe shari, na hafai kwa ushirika,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Mmoja mmoja kiri, si ukwasi ni ufukara,
Kujionesha ghairi, kwa nyimbo nazo bendera,
Ili uyatafakari,watu wako wote bara,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Uchumi uwe mzuri, tubadili yetu dira,
Wote tukiwa kwenye heri, twaweza kuuza sura,
Vinginevyo minghairi,yakini kwenye ubora,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Ulaya sina safari, wanihini ufukara,
Pia sinayo habari,Marekani kuzurura,
Sijaona alfajiri,nachelea ufukara,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Ninamuomba Bashiri, kutupatia nusura,
Waache kutuhadhiri, sisi tunaodorora,
Tupate wenye akheri, kuwa ni wetu vinara,
Hata ukiwa tajiri, kwa nchi tajiri, fukara.

Wednesday, September 22, 2010

Paka ameshiba mno

Keshashiba sana paka, kuwala panya hataki,
Na nyama kafaidika, vya kuwinda havitaki,
Sharubu zimekunjika, kuruka tena haruki,
Paka ameshiba mno, hataki kuwala panya !

Kakaa hana mashaka, na wala hapapatiki,
Mwenzetu kesharidhika, visivyopikwa hataki,
Msafi anajiweka, kujilambalamba hachoki,
Paka ameshiba mno, hataki kuwala panya !

Paka amekwishafika, masikani habanduki,
Sasa keshazoeleka, ndani ya nyumba hatoki,
Wengine wanamtaka, kitandani hudiriki,
Paka ameshiba mno, hataki kuwala panya !

Hajali anayemweka, anachojali riziki,
Hawezi akatoroka, kwani ametamalaki,
Wenyeji wanamtaka, kwanini awadhihaki?
Paka ameshiba mno, hataki kuwala panya !

Paka ametajirika, ikulu ni mstahiki,
Ukubwa kajipachika, wadogo tena hataki,
Milki ameishika, uongozi ashiriki,
Paka ameshiba mno, hataki kuwala panya !

Sio pusi huyu paka, walal jina nyau hataki,
Kaacha kuhangaika, inamfuata riziki,
Kazisusa patashika, kasri keshaiteka,
Paka ameshiba mno, hataki kuwala panya !

Hajui yanayozuka, mapanya wazua baa,
Wazaliana hakika, ndani kote wameshajaa,
Ni nani wa kuwashika, na paka amekataa?
Paka ameshiba mno, hataki kuwala panya !

Unaweza neemeka, kwa nyota yake twariki,
Kumbe ndio waanguka,u chini kitahamaki,
Yasiyemfika paka, huko alikokwishajaa,
Paka ameshiba mno, hataki kuwala panya !

Ndoa zingine kunyonywa

Ndoa zingine maziwa, huishi wewe kunyonywa,
Miaka inavyozidia, wazidi kuanganywa,
Hata kile kilojaa, huishia kumumunywa,
Ndoa zingine kunyonywa, na huku unadanganywa.

Kwa dini au sheria, harusi yenu hufanywa,
Ahadi mtazitoa, mkatae kusengenywa,
Na mafunzo mtapewa, na wazazi mkakanywa,
Ndoa zingine kunyonywa, na huku unadanganywa.

Ukweli hujifichua, wakati mnap0ofinywa,
Maslahi kupungua, kila pembe mnaminywa,
Hali zinapotitia, watu rahisi kugawanywa,
Ndoa zingine kunyonywa, na huku unadanganywa.

Ndugu na hao jamaa, ya uongo hutawanywa,
Hubakia kuvizia, yatangazwa yasiyofanywa,
Na mitego husambaa, wategwe wasiokanywa,
Ndoa zingine kunyonywa, na huku unadanganywa.

Hodari walioamua, milele kutokugawanywa,
Kisha wakajititimua, wasiwe watu wa kunywa,
Fedha kudundulizia, waache tena kunyonywa,
Ndoa zingine kunyonywa, na huku unadanganywa.

Kuwekeza wakitua, vinginevyo wakatonywa,
Mke anapoamua, hataki tena kunyonywa,
Mbele akavichukua, huku mume anasonywa,
Ndoa zingine kunyonywa, na huku unadanganywa.

Mme chumvi hudaiwa, na chake kikamenywa,
Bahili mke akawa, sio wa kumumunywa,
Mme nguvu hulegea, asitake kutekenywa,
Ndoa zingine kunyonywa, na huku unadanganywa.

Ndoa jambo maridhia, ila pasiwe kunyonywa,
Nikahi kitu murua, mtu asiposengenywa,
Nyumba hujititimua, na watu msipogawanywa,
Ndoa zingine kunyonywa, na huku unadanganywa.

Baradhuli awe nje

Awe nje baradhuli, akiwa ndani nazaa,
Hudhoofu yako hali, kwa mashaka na balaa,
Kasema Akilimali, nami ninalitambua,
Baradhuli awe nje, akiwa ndani ni balaa.

Si mme si mwanamali, ni watu wa kuduwaa,
Ukweli hawakabili, uongo wanauvaa,
Hodari kwa ubahili, na wagumu wa kutoa,
Baradhuli awe nje, akiwa ndani ni balaa.

Si watu wa afadhali, nafuu hawajaijua,
Hawana mustakabali, mambo yao ya kuzua,
Hesabu sioi kamili, ni watu wa kupungua,
Baradhuli awe nje, akiwa ndani ni balaa.

Akiwa ndani ajali, hutoacha kuzijua,
Na yake kubwa dalili, uwazi kuukataa,
Mbishi kama kandili, iliyo kwenye mvua,
Baradhuli awe nje, akiwa ndani ni balaa.

Amana hastahili, si mtu wa kuaminiwa,
Hulka yake dhalili, si mtu wa kusikia,
Hujiona kuwa ghali, kumbe bure hatofaa,
Baradhuli awe nje, akiwa ndani ni balaa.

Shairi hili nakili, lafaa kuwaimbia,
Ni mjinga baradhuli, si mtu wa kufikiria,
Aweza kuwa na mali, na ovyo ikapotea,
Baradhuli awe nje, akiwa ndani ni balaa.

Aweza kuwa jamili, mzuri wa kuzuzua,
Kimkaribia kimwili, utataka kukimbia,
Ni haramu si halali, hali yake alokuwa,
Baradhuli awe nje, akiwa ndani ni balaa.

Kaditama sihimili, mbele siwezi endelea,
Nimemvua baradhuli, joho analotumia,
Muulizeni maswali, kama mtamuelewa,
Baradhuli awe nje, akiwa ndani balaa.

Sunday, September 19, 2010

Choo si pipa la taka

Choo lina zake taka, lakini si uchafuzi,
Si mahala pa kuzika, ila pakutaladhahi,
Wengi tunakereheka, yasopaswa matumizi,
Choo si pipa la taka, kikiziba kuna kazi !

Watupaje takataka, na choo hakiyawezi,
Unatupaje viraka, na vipande vya mavazi,
Mnatutia mashaka,na choo hakipendezi,
Choo si pipa la taka, kikiziba kuna kazi !

Kaziye kusetirika, kupunguza uchukuzi,
Pasafi ukaviweka, vilivyo na uchokozi,
Nawe ukapumzika, kuvuta safi pumzi,
Choo si pipa la taka, kikiziba kuna kazi !

Wenzetu wanasifika, choo kwao matanuzi,
Chooni akishafika, huwa hafanyi ajizi,
Hakika hupumzika, akawa kitu hawazi,
Choo si pipa la taka, kikiziba kuna kazi !

Kwingine si Afrika, chooni wanabarizi,
Hekima zikachmbika, vilokuwa hawawazi,
Na ujumbe wakaweka, uende kwa wateuzi,
Choo si pipa la taka, kikiziba kuna kazi !

Yabidi kubadilika, vyoo tupate kuenzi,
Bila'vyo kuheshimika, itakuwa si saizi,
Yapo mengi kufanyika, ili tuipande ngazi,
Choo si pipa la taka, kikiziba kuna kazi !

Kama nyumba ni mashaka, makazi ni kama zizi,
Vipi choo kujengeka, vyenye thamani azizi,
Watu watatosheka, kustawisha mizizi,
Choo si pipa la taka, kikiziba kuna kazi !

Hapa kwetu Afrika, hawawazi viongozi,
Wao wamesharidhika, kwa o vyoo i tailizi,
Sisi kutostaarabika, waona yetu saizi,
Choo si pipa la taka, kikiziba kuna kazi !

Wengi wao wanshafika, mengine hawayawezi,
Wabebwa kuzoeleka, wala hawafanyi kazi,
Wananchi wanateseka, wao kwao wabarizi,
Choo si pipa la taka, kikiziba kuna kazi !

Wachawi saidieni

Sifa zenu naamini, zimeenea mjini,
Kadhalika vijijini, pia kote duniani,
Kwa kweli twawaamini, ila bado kuwathamini,
Wachawi saidieni,tupate maendeleo.

Mtunzi nimebaini, mna mengi kwa yakini,
Mwaweza fanya nchini,uchumi usiwe duni,
Mkaongeza thamani,dunia kututhamini,
Wachawi saidieni,tupate maendeleo.

Tunataka televisheni, zenye bei afueni,
Mwazitengeza nyumbani, hamuuzi madukani,
Tunachotaka mwakani, hizo ziwe mitaani,
Wachawi saidieni,tupate maendeleo.

Mwazungumza hewani, ila simu hatuoni,
Nalo hili twaamini, ni biashara auni,
Zije simu za mkononi, tuwe nasi washindani,
Wachawi saidieni,tupate maendeleo.

Finland na Marekani, kwa Nokia ni makini,
Motorola nayo ndani,Ya kwetu iwe akilini,
Tuuite jina gani,pengine la Majinuni,
Wachawi saidieni,tupate maendeleo.

Mashine kaziundeni, tupeleke viwandani,
Msukule watumieni,hata nishati wabuni,
Ili mradi mwakani,nchi iwe namba wani,
Wachawi saidieni,tupate maendeleo.

Na ungo kageuzeni, tupate ndege angani,
Eitisii ifufueni,iende hadi Japani,
Na mizigo tubebeni,tuiuze kwa jirani,
Wachawi saidieni,tupate maendeleo.

Elimu yenu ya ndani,mwaisaka ugenini,
Kadhalika mashambani, pamwen namo nyikani,
Vilevile vichakani, yote mnayathamini,
Wachawi saidieni,tupate maendeleo.

Majongoo geuzeni, wawe za sasa treni,
Dizeli iachieni, umeme tutumieni,
Uchina shirikianeni,mwokoe zetu laini,
Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

Maji huko maziwani, uchawi utumieni,
Yapande hadi nyikani, tunyweshe mashambani,
Tutumie na mjini,maana hayaonekani,
Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

Mwingie na baharini, madini yatafuteni,
Pia mafuta sakeni, nchi ipate ihwani,
Haya sifanyi utani,wallahi ninawaamini,
Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

Mmeshinda mitihani, wajao uongozini,
Mliita mashetani, mizimu pia majini,
Hiana hawakuwafanyieni, wakawa madarakani,
Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

Hakika nawaamini, nchi yawategemeeni,
Bila ya nyie yakini, tutakuwa mashakani,
Kuendelea yumkini, pasiwe matumaini,
Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

Kama wanawaamini, viongozi duniani,
Basi ni nyie makini, na si wao jamani,
Ustawi uleteni, daima tuwasifuni,
Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

Wewe kwangu kama mfu

Wapo wanaopumua, lakini sawa na mfu,
Wasiokusaidia, bali huwa wanakifu,
Hata tajiri wakiwa, mali yao ni nyamafu,
Wewe kwangu kama mfu, haupo kwenye dunia.

Vibaya kukumbukia, mafao safu kwa safu,
Niliokwisha watendea, watwana na marufu,
Nikashukuru dunia, kunikidhi ukunjufu,
Wewe kwangu kama mfu, haupo kwenye dunia.

Nikashukuru dunia, kunikishi ukunjufu,
Nimesahau mamia, ila wangu udhaifu,
Kwalo ninashangilia, na kumtukuza Afu,
Wewe kwangu kama mfu, haupo kwenye dunia.

Elimu nilowapatia, wakapata utukufu,
Kazi nilowaombea, wakazihodhi tarafu,
Mchango nilochangia, wakapata masurufu,
Wewe kwangu kama mfu, haupo kwenye dunia.

Ni Vero ninayemjua, nyuma aliyerudufu,
Akazileta hidaya, kwangu na mai waifu,
Machozi tuliyaachia, kuipata hii sharafu,
Wewe kwangu kama mfu, haupo kwenye dunia.

Wengi tumesaidia, ila huyu bashrafu,
Ni kazi kumpatia, na kula naye kandafu,
Moyoni katuchukua, masafa yenye urefu,
Wewe kwangu kama mfu, haupo kwenye dunia.

Ni wengi waliokuwa, wafupi pia warefu,
Chetu tuliwamegea, pasipo ya israfu,
Nafasi tukawaachia, masafu kwa masafu,
Wewe kwangu kama mfu, haupo kwenye dunia.

Leo waturingishia, kwa vito na zao sufu,
Kila wakiangalia, wajiona watukufu,
Na sisi watuzomea, masikini wa siafu,
Wewe kwangu kama mfu, haupo kwenye dunia.

Tumeijua dunia, na nyoyo zake hafifu,
Tunashika yetu njia, hatuyataki madufu,
Msije tuparamia, tutawaona uchafu,
Wewe kwangu kama mfu, haupo kwenye dunia.

Ukimya tumechagua, sisi si watu wa rafu,
Wetu usipowaangalia, kwetu wewe kama mfu,
Kuna tunayemtegemea, naye ni wetu Latifu,
Wewe kwangu kama mfu, haupo kwenye dunia.

Saturday, September 18, 2010

EITIEMU

Eitiemu imegoma, fedha sijazichukua,
Mfukoni nimekwama,na shida sijaatatua,
Na mtu wa kuazima,bado sijamfikiria,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Kujiamini nasema, leo kumeniumbua,
Sikuwa nayo tuhuma, ndarahima sintotoa,
Kutoka utu uzima, utotoni nikaloa,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Eitiemu kwa heshima, yote nilikupatia,
Nikidhani kwa nakama, sasa nimezikimbia,
Na hulka ya kuazima, mbali nimetupilia,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Ndugu nilishawahama, mbali nao nikakaa,
Rafiki nikawasema, mbele wakatangulia,
Eitiemu muadhama, wawili tukabakia,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Na kila nikikutuma, haraka ulikimbia,
Ukarejesha uzima, pale ulipopotea,
Ukaniwia karama, kidogo kuabudiwa,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Umbo lako dogo jema, mfukoni waingia,
Mororo ukitazama, na laini ulokuwa,
Ila mkubwa kwa gharama, haja zangu kutimia,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Kwangu ikawa rehema, kwa jua pia mvua,
Kila nikikutazama, nazidi kujiaminia,
Daima nikikusoma, na kukuchungulia,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Haukunikwaza mtima,nikajua wanijua,
Wewe kwangu ni salama, na kweli nimeridhia,
Ukafanya kila hima, mimi kunitumikia,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Ghafla leo nakwama, sijui pakukimbilia,
Imeondoka adhama, mengi natuhumiwa,
Mimi niliyesimama,watu wakashangilia,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Mimi niliyesimama, watu wakafurahia,
Leo nahofu hasama,wasijenishambulia,
Ninaifunga kalima, mafichoni kurejea,
Eitiemu nimekwisha, kwanini wanikatalia ?

Copyright © Sammy Makilla-2010

Ni wewe ukishakufa

Maongozi yetu gea, isiyoelekezeka,
Wapi tunakoelekea, bado hakijaeleweka,
Kila nikiangalia,yananijaa mashaka,
Ni wewe ukishakufa, ndio yatatekelezeka.

Mipango yao nazaa,kwangu haijaeleweka,
Miaka yake mamia,huko mimi nitafika,
Umri ninaoujua,wala nusu haujafika,
Ni wewe ukishakufa, ndio yatatekelezeka.

Yapo ninayoyajua,yanachukua miaka,
Lakini mengi halua,michache yanafanyika,
Ila hatujawastua,wawe watu wa haraka,
Ni wewe ukishakufa, ndio yatatekelezeka.

Ushindani umepoa,kama umehasika,
Hakuna lakuzimua,yachacha na kuchachika,
Daima yao tabia, mambo husahaulika,
Ni wewe ukishakufa, ndio yatatekelezeka.

Uono wao wa pua,vipi mbali watafika,
Husifu moja hatua,hali elfu twataka,
Ni watu waliolowa,na rahisi kuridhika,
Ni wewe ukishakufa, ndio yatatekelezeka.

Haitungoji dunia,mwendo lazima haraka,
Lengo ukijiwekea,kuchelewa si mwafaka,
Ukiweza tangulia,unaondoa mashaka,
Ni wewe ukishakufa, ndio yatatekelezeka.

Afrika yatitia,wengine kwapambazuka,
Magharibi twapotea,Mashariki tunavuka,
Ila kwa wasiojua,kasumba yawafunika,
Ni wewe ukishakufa, ndio yatatekelezeka.

Mengi nayafikiria, yangekwishatekelezeka,
Wakubwa watutania,dhamira yao wahaka,
Nazidi yaangalia,nakumwachia Rabuka,
Ni wewe ukishakufa, ndio yatatekelezeka.

Copyright © Sammy Makilla-2010

Pensheni zinaliwa

Tofauti sijajua, ya hisa na kuchangia,
Makato ninayotoa, ni fungu nawekezea,
Bado mnaniambia, mwanachama nimekuwa,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Kazi najitegemea, changu mnakichukua,
Kasri mwajijengea,kibanda sijakijua,
Nishai mnanitoa,wezi ninawafikiria,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Hata ninapougua, juzi ndo mwagundua,
Huduma nahitajia, na lazima kulipia,
Zama hivyo haikuwa, mwenyewe mliniachia,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Ada zinanisumbua, kunikopa mwakataa,
Uchungu ninaosikia,kama vile ninazaa,
Nataka kuwafunua,kisha nikawafukia,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Kinachostahli kuwa, nilichokinunua,
Vipi mnakiachia, walaji kusimamia,
Meneja sijamchagua,na wala sijamjua,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Ukiritimba mwakaa, yote mnajivutia,
Naona sasa yafaa, unyonywaji kukataa,
Pensheni kuachia,ziwe za waajiriwa,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Serikali inafaa, pembeni kuja kukaa,
Nyingine kufungua, binafsi kwa ridhaa,
Ushindani kuingia,pasiwe anayesinzia,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Pensheni maridhia, mmiliki humfaa,
Hisa anazozitoa, kampuni yake huwa,
Hakuna wa kuingilia,maamuzi anayotoa,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Kwa hali ilivyokuwa, mmiliki atwibia,
Siye wa kumkubalia, huyu anatuingilia,
Maamuzi anayotoa,hayawezi kutufaa,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Amkeni Watanzania, hivi sasa twaibiwa,
Ufukara tutaoa,ndoa isiyokataliwa,
Watukaanga wazawa, samli yetu watumia,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Inabidi kushupaa, cha kwetu kukichukua,
Najua watakataa, nasi tutawakatalia,
Lazima kuwapakua, tupike kinachofaa,
Pensheni zinaliwa, na wasiozichangia.

Copyright © Sammy Makilla-2010

Maziwa

Nyasa kisha Victoria, Tanganyika nalo pia,
Maziwa umejaliwa, mama yetu Tanzania,
Vipi twanyong'onyea, sababu hatujajua,
Maziwa umejaliwa,unashndwa kunyonyesha ?

Usichana waringia, au umekaukiwa,
Kilio tunacholia, bado hujakisikia,
Mikononi twakufia, nawe watuangalia ?
Maziwa umejaliwa,unashndwa kunyonyesha ?

Maziwa yanasifiwa, kwenye ramani watia,
Ulaya wanayajua, walikikwishayafuatilia,
Misri inayatumia,Sudani na wao pia,
Maziwa umejaliwa,unashndwa kunyonyesha ?

Ndio wanayoyakamua, au unawakamulia,
Watoto wao wakua, unyafuzi watuvaa,
Utapiamlo balaa, huruma yatuumbua,
Maziwa umejaliwa,unashndwa kunyonyesha ?

Enyi kizazi kipya, hili budi kushangaa,
Wazazi wamepagawa, hawaijui dunia,
Wewe waweza ifaa,lakini haitokufaa,
Maziwa umejaliwa,unashndwa kunyonyesha ?

Ujanja tumezidiwa,hata na wapita njia,
Virutubisho wavua,wavipeleka Ulaya,
Sisi bado twazubaa,tunazijali sheria,
Maziwa umejaliwa,unashndwa kunyonyesha ?

Palestina yafaa, kwenda kutembelea,
Mitaro waichimbua, kilomita kwa mamia,
si maji tu yapitia,hata zana na vifaa,
Maziwa umejaliwa,unashndwa kunyonyesha ?

Chini kwa chini watua, kwa juu hautojua,
Hutoka wakaingia, na vito kuvinyanyua,
Uhai waendelea, waisanifu dunia,
Maziwa umejaliwa,unashndwa kunyonyesha ?

Ninalia Tanznia, mama usiyetimia,
Wengine waangalia,wanao waangamia,
Maziwa umejaliwa,unashndwa kunyonyesha ?
Maziwa umejaliwa,unashndwa kunyonyesha ?

Copyright © Sammy Makilla-2010

Majivuno Kusadikika

Kila mwabudu Wazungu, kujiamini kahama,
Kila mtegemea ndugu, kusimama keshakwama,
Asiyekitunza chungu, hifadhi hana daima,
'Weupe wa nywele zangu, hauonyeshi hekima:
sikiza kauli yangu, maamuzi na azma!'

Asiyemwogopa Mungu, shetani anamtuma,
Asojali watu wangu, hana ya kwangu heshima,
Achanganyaye mafungu, ni mwizi wa mali ya umma,
'Weupe wa nywele zangu, hauonyeshi hekima:
sikiza kauli yangu, maamuzi na azma!'

Atawalae kwa rungu, kuua kwake lazima,
Asotishika na mbingu,ardhi humsakama,
Hofu ikitiwa pingu,uoga hurudi nyuma,
'Weupe wa nywele zangu, hauonyeshi hekima:
sikiza kauli yangu, maamuzi na azma!'

Dunia ya wanguwangu,huipoteza hekima,
Nje kukiwa ukungu, huoni kwa kutazama,
Na utamu wake dengu, si utamu wa mtama,
'Weupe wa nywele zangu, hauonyeshi hekima:
sikiza kauli yangu, maamuzi na azma!'

Copyright © Sammy Makilla-2010

Friday, September 17, 2010

Akili kama vyoo

Ndio wetu viongozi, na hizi akili zao,
Wafurahia ushuzi, ukiwa kwa wengineo,
Wao yao matanuzi,kilo bora ndicho chao,
Ubovu wa vyetu vyoo, sawa na zetu akili !

Onyesha wao ushenzi,huja mbogo watu wao,
Mtu akitoa chozi, acheka hudai wao,
Mwananchi kwao masinzi, bora si yamfaayo,
Ubovu wa vyetu vyoo, sawa na zetu akili !

Hutuiita wachochezi, nchi twataka pindua,
Kumbe wao wachokozi, kazi si wanaojua,
Ila kawapa Mwenyezi, uwezo sasa ni wao,
Ubovu wa vyetu vyoo, sawa na zetu akili !

Nchi imekosa wajenzi,tapeli watawalao,
Hawa ni wengi wa ajizi, heri sio waletao,
Umejaa ubazazi, ndio matunda yao,
Ubovu wa vyetu vyoo, sawa na zetu akili !

Tunataka mapinduzi, wa viongozi wajuao,
Wanaoheshimu kazi, za wananchi wenzao,
Wasotia pingamizi,habari wazitoao,
Ubovu wa vyetu vyoo, sawa na zetu akili !

Hatutaki mashauzi,majuha tulionao,
Wadhanio uongozi,ni kunyanyasa wenzao,
Tunataka chapakazi,popote wajitumao,
Ubovu wa vyetu vyoo, sawa na zetu akili !

Mahakama za wajuzi, sikia chetu kilio,
Waandishi na watunzi,kwa sasa tukitoao,
Tutashndwa fanya kazi, kwa vitishi na matao,
Ubovu wa vyetu vyoo, sawa na zetu akili !

Yafanyeni maamuzi, hawa si watufaao,
Nchi wapaka masinzi,kwa wote watujuao,
Twaonekana washenzi,na sheria si tujuao,
Ubovu wa vyetu vyoo, sawa na zetu akili !

Uongozi kubwa kazi, waulize wajuao,
Usidhani ni viyoyozi,maslahi na mafao,
Cheo ni usimamizi,uletao mafanikio,
Ubovu wa vyetu vyoo, sawa na zetu akili !

Cheo ni uangalizi, wa wale uongozao,
Na ukubwa ni malezi, yaje bora matokeo,
Ukuu si maonezi, kwa cheo uwazidio,
Ubovu wa vyetu vyoo, sawa na zetu akili !

Utumwa hatuuwezi, miaka hii iwayo,
Wafalme si majazi, wala si tuwatakao,
Hatutaki viongozi, watu wanyanyasao,
Ubovu wa vyetu vyoo, sawa na zetu akili !

Thursday, September 16, 2010

Ndio ukubwa wa pua

1.
Laiti ingelikuwa, pua kubwa damisi,
Watoto wasingekuwa, wanatoka makamasi,
Udogo ungezidia, katu wasitanafusi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
2.
Humkuta babu pua,michirizi yamuasi,
Kila akilipengua,maji yanamdadisi,
Huugua akalia,sikuzote wasiwasi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
3.
Pua ndogo hutulia,na mabonge kuanisi,
Mtoko hukushtua,kama skadi ya Mrussi,
Na ubongo hupagawa, kwa raha unavyohisi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
4.
Kama hili watambua,mja umeshadurusi,
Dunia kweli wajua,ma ukweli wake kiasi,
Kiumbe hajatimia,bila hii fahirisi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
5.
Upepo ukipepea,kifua mara huasi,
Na nusura ni mafua,mirija yake kamasi,
Uchafu huuchukua,kuupitisha kwa kasi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
6.
Kamasi ukilitoa,huburudika nafsi,
Kitu kidogo twajua,lakini yote Qudusi,
Rehema zake zatua,japo tuna Ibilisi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
7.
Pua yangu nilidhania, imeshapita kiasi,
Ukubwa imezidia, itajakuwa nuksi,
Wazungu nikashangaa, zao kwao kama basi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
8.
Ndipo nikang'amua,pua kubwa si mkosi,
Ukitaka kuendelea,uwe yake majilisi,
Mashine utavumbua,na madawa kuasisi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
9.
Pua iliyodumaa,zinaleta uyabisi,
Hawana wanachojua,akili zao muflisi,
Ni watu wa kununua,kutengeneza hadithi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
10.
Hata waitwao mapua,hili kwao si nemsi,
Ovyo wameshakuwa,fikra zao najisi,
Kila wakijifaragua,wawashinda ubinafsi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
11.
Kila nikifikiria, baridi ninaihisi,
Mwafrika sijamjua, kuitaliki nafusi,
Lake ndilo maridhia, ya wengine si mfuasi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
12.
Msaada tungegawiwa, tena ulo mahsusi,
Pua tungezawadiwa, tupunguze ubinafsi,
Na wengine kuangalia, maisha yawe harusi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
13.
Ni kazi kuendelea, budi utoe kamasi,
Sie tunadidimia,pua zimekosa jasi,
Uongo tunapumua,na mipango ya nuksi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.
14.
Lipi tumeshikilia,si sanaa si sayansi ?
Ni watu wa kusaidiwa,kwa viatu na libasi,
Watu wa kuhurumiwa,kwa haramu na najisi,
Ndio ukubwa wa pua, uhimilio kamasi.

Utaombwa ukiomba

1.
Si ubwabwa wala pamba, kinachokosa nyongeza,
Kama wewe uliumbwa, kuumbuka unaweza,
Na mchamba huchambwa, na nuru haiwi giza,
Utaombwa ukiomba , je, hayo utayaweza ?
2.
Dunia kome la mimba, yalopita hurejeza,
Yazaliwe kama ndumba, nakala ziloigiza,
Hakuna anayetamba, kaziye kama kucheza,
Utaombwa ukiomba , je, hayo utayaweza ?
3.
Nakukanya Mwanakamba,ajizi hulegeza,
Uikaze hino kamba, ulimwengu kukufunza,
Na katu kutojigamba,ushujaa hutoweza,
Utaombwa ukiomba , je, hayo utayaweza ?
4.
Tosheka na wako mtumba, mpya waachie wenza,
Kama hauna uvumba, udi poa utafukiza,
Komba kama wanalamba, usitafute nyongeza,
Utaombwa ukiomba , je, hayo utayaweza ?
5.
Usimwombe mwana gumba,hauwezi muujiza,
Usipeleke kilemba, Pemba hautokiuza,
Huna chumba, vipi nyumba, hunayo unajikweza ?
Utaombwa ukiomba , je, hayo utayaweza ?
6.
Warembo wana kasumba, na wengine zimeiza,
Usitafute mchumba, kwa sura ya kupendeza,
Huyo aliyemuumba, vingine kamlemaza,
Utaombwa ukiomba , je, hayo utayaweza ?
7.
Usitake lima shamba, maji yasikopitiza,
Na ukifuga mtamba, mila jike kuagiza,
Na mchele wenye pumba, bila kupeta hukwaza,
Utaombwa ukiomba , je, hayo utayaweza ?
8.
Usiombe utaombwa, hili mwali nakukataza,
Tosheka nacho kibamba, usitamani mkuza,
Dunia ni komba komba, wengi huwapatiliza,
Utaombwa ukiomba , je, hayo utayaweza ?
9.
Utaombwa ukiomba, je, hayo utayaweza ?
Sio wimbo wa kuimba, mjuzi nakukataza,
Mtoka choo kuchamba, desturi yaagiza,
Utaombwa ukiomba , je, hayo utayaweza ?

Tumbo likiuma….

1.
Muone akitembea, utadhani ni maswezi,
Guu ashindilia, utafikiri mjenzi,
Kiuno kashupalia, mithili yake mkwezi,
Mbwembwe kwa kutembea, tumbo likiuma huwezi.
2.
Mja si yako dunia,tabia chako kitanzi,
Nini unachoringia,wengine hawakimalizi ?
Wajitakia ukiwa, siku yenye fumanizi,
Mbwembwe kwa kutembea, tumbo likiuma huwezi.
3.
Leo unavyotembea, iweje kesho huwezi,
Tumbo likivimbiwa,mbona itakuwa kazi,
Hubaki unalialia,na vishindo vya ushuzi,
Mbwembwe kwa kutembea, tumbo likiuma huwezi.
4.
Tembea bila umbeya,kama mtu wa zoezi,
Nenda waihurumia,dunia yake Mwenyezi,
Na wale wanaojua,ni amri ya Azizi,
Mbwembwe kwa kutembea, tumbo likiuma huwezi.
5.
Nenda unafikiria, na Manani kumuenzi,
Zipige zako hatua,dunia hauimalizi,
Kwa staha kutembea,na kusifu hii enzi,
Mbwembwe kwa kutembea, tumbo likiuma huwezi.
6.
Wanangu nawausia,dunia siyo ya machizi,
Elimu kuzisomea,mema yalo matembezi,
Mwenyezi nikumjua,njia hugeuka majazi,
Mbwembwe kwa kutembea, tumbo likiuma huwezi.
7.
Kuvimba haijakuwa,jambo lililo na radhi,
Ni bure kujitanua,bahari hauiwezi,
Yanini kujisifia,msifu wako Muizzi,
Mbwembwe kwa kutembea, tumbo likiuma huwezi.
8.
Watazame walokuwa,wakitamba na mabenzi,
Waliovimbisha vifua,walifunzwa hawafunzi,
Kimya wameshatulia,wameiafiki dozi,
Mbwembwe kwa kutembea, tumbo likiuma huwezi.

Dhahabu anachukua

1.
Sijui weusi baa, kama sio mgahawa,
Mjanja kumtania, hajui asiyejua,
Na nchi ikivamiwa, mamluki mwamjua,
Dhahabu anachukua, anigawia mkaa !
2.
Kunyonga aliyezoea, kuchinja anachelea,
Mwizi ukimchagua,jua atakuibia,
Mbwa ukimzoea,msikitini huingia,
Dhahabu anachukua, anigawia mkaa !
3.
Anayedharau wazawa,mwenyewe hajajijua,
Utuwe hununuliwa, mateka kisha akawa,
Kiongozi msifiwa, heri zezeta ya kuwa,
Dhahabu anachukua, anigawia mkaa !
4.
Vibaka tunawajua, walio kwenye mitaa,
Ila hatujawajua,ukubwa wanaouvaa,
Hazipishani tabia, kama hujui tambua,
Dhahabu anachukua, anigawia mkaa !
5.
Ujinga hautokufaa, mwizi kumng'amua,
Tende hukutupia,nawe ukanogewa,
Basi utamuachia,vya maana kuchukua,
Dhahabu anachukua, anigawia mkaa !
6.
Mwafrika kalaaniwa,au kachanganyikiwa,
Nduguze kuwakataa,kuona wasiofaa,
Wageni kushikilia,nasaba wasiokuwa,
Dhahabu anachukua, anigawia mkaa !
7.
Mikosi inashupaa, na maafa yatanua,
Nchi zinaangamia, waroho wachekelea,
Viongozi twachagua,wenyewe wanaojifaa,
Dhahabu anachukua, anigawia mkaa !
8.
Andiko hili radhia, lisome kizazi kipya,
Hao ndio watajua,ni nani wetu majuha,
Na kisha kuwazomea,kuzika hai wakiwa,
Dhahabu anachukua, anigawia mkaa !
9.
Waifute historia, yote waliochafua,
Walo wema kubakia, hadi siku ya kiyama,
Na Mola kushuhuhudia, Afu aliyetimia,
Dhahabu anachukua, anigawia mkaa !
10.
Hamsini yatimia, miaka ya kupotea,
Jangwani tulipagawa,na njia hatukuijua,
Leo Rabi twamlilia,nyota itaangazia,
Dhahabu anachukua, anigawia mkaa !
11.
Sisi katu hatujawa, ndio jaa la dunia,
Vya wengine kununua, nasi kutowauzia,
Akili zingepungua, uwizi tusingejua,
Dhahabu anachukua, anigawia mkaa !
12.
Muda umekaribia, eon kuja kutimia,
Mwokozi mkimlilia,Mungu huwazawadia,
Wezi mking’ang’ania,naye atawaachia,
Dhahabu anachukua, anigawia mkaa !

Mweupe Kisha Mweusi

1.
China na Malaysia, wameshaoneysha njia,
Himaya wamejijengea, wananchi kutangulia,
Viranja wakabakia,wa mwisho kuangaliwa,
Mkoloni rangi nyeupe, kamuachia Mweusi.
2.
Kwao wamemuondoa, mkoloni kakimbia,
Na wao hawakuchagua,kuwarithi walokuwa,
Taifa kutumikia,hilo ndilo waloamua,
Mkoloni rangi nyeupe, kamuachia Mweusi.
3.
Viongozi wetu baa,wajua wanalokimbia,
Ikulu wakiingia,kazi kujishaua,
Matanuzi kuyakwaa,hata yasiyowafaa,
Mkoloni rangi nyeupe, kamuachia Mweusi.
4.
Kitendawili kimekua,hamsini yatimia,
Wanavaa wanavua,wengine wanaingia,
Sala inatabiriwa,mwananchi ataumia,
Mkoloni rangi nyeupe, kamuachia Mweusi.
5.
Mweupe amwemwachia, mweusi tunayemjua,
Naye ashilindilia, shindilia dona kawa,
Viumbe wanatitia,ardhini wadidimia,
Mkoloni rangi nyeupe, kamuachia Mweusi.
6.
Mweusi kashikilia,ufalme katangazia,
Gabon wameamua,Misri wanafuatia,
Na pengine yatatokea, huko tulikozaliwa,
Mkoloni rangi nyeupe, kamuachia Mweusi.
7.
Hili haliwi ni baya, kama hai tungekuwa,
Kwa maana ya kuchanua, ustawi
tukakwea,Kilele kukifikia,cha waliokwishajaliwa,
Mkoloni rangi nyeupe, kamuachia Mweusi.
8.
Hawa wanalolijua, ni kula na kutumia,
Shilingi yadidimia, wao wanazidi jaa,
Nchi imeshafulia,twaambiwa yaendelea,
Mkoloni rangi nyeupe, kamuachia Mweusi.
9.
Bure ukiviachia, ni wapi utajazilia,
Benki ukizipakua, nani wa kukufidia,
Utapiamlo ukijaa, akili nani kujaliwa ?
Mkoloni rangi nyeupe, kamuachia Mweusi.
10.
Akili zimeshavia, nani analo jipya,Mazezeta
tunshakuwa, kaburi latungojea,
Kasi imeshahasiwa, kipi kitakachozaliwa ?
Mkoloni rangi nyeupe, kamuachia Mweusi.
11.
Hoi tumekwishakuwa,wapi nguvu kupatia,
Ari imeyoyomea,ni wapi pa kuanzia,
Ni budi upya kuzaliwa,mambo ndio kutangamaa,
Mkoloni rangi nyeupe, kamuachia Mweusi.
12.
Kama miji yasinzia,vijiji vimeishilia,
Usingizini vyarudia,Kuamka shida imekuwa,
Miujiza yangojewa,hali kujanusuriwa,
Mkoloni rangi nyeupe, kamuachia Mweusi.
13.
Kizazi changu chalia, nchi tumeibambua,
Hakuna kilichobakia,gogo lote laishia,
Na wanaotufatia,lazima kushtakia,
Mkoloni rangi nyeupe, kamuachia Mweusi.

Wednesday, September 15, 2010

Ni mimi na wewe

Awali tulishakutana, sijui mahala gani ?
Ukanigea amana, kuniingiza peponi,
Na niliposhtukia, ikawa hauonekani,
Ni siku nyingine tena,mimi na wewe peponi!

Leo nakuona tena, macho yangu hayaamini,
Kitu gani nitanena, uwe mwangu mikononi,
Pembe gani nitabana,niwe nawe faraghani,
Ni siku nyingine tena,mimi na wewe peponi!

Wewe kwangu ni hazina,chemchemi ya imani,
Hawa yako sijaona,mwangu tena maishani,
Afya yangu hunona,ukiwa mwangu moyoni,
Ni siku nyingine tena,mimi na wewe peponi!

Imeitikiwa amina,dunia niliyoghani,
Mtima siwezi kana,njia hii naiamini,
Si mtu wa danadana,mashuti yangu makini,
Ni siku nyingine tena,mimi na wewe peponi!

Nimeuona mwamana,nipe ya kwako yamini,
Waisikia adhana,elekea ibadani,
Kuwa radhi Maulana,mja huitwa peponi,
Ni siku nyingine tena,mimi na wewe peponi!

Yangu hayana laana,namuogopa Manani,
Nasihi yake dhamana,kukutia mikononi,
Uwe shuka kwa bayana, pia nami yumkini,
Ni siku nyingine tena,mimi na wewe peponi!

Furaha yangu kufana,tena hapa duniani,
Kwalo hilo kukazana,uelewe ihwani,
Hakika nitajiiona, hai zaidi natona,
Ni siku nyingine tena,mimi na wewe peponi!

Kwanini nipige kona,hali kuna ushindani,
Nikijageuka tena,uwe hauonekani,
kutakana kukamatana,ukiwachia hatiani,
Ni siku nyingine tena,mimi na wewe peponi!

Hili sasa ninavuna,vaa pete kidoleni,
Itunze yangu amana,niweke mwako moyoni,
Dunia ni pana sana,isije kutuhadaa,
Ni siku nyingine tena,mimi na wewe peponi!

sagesage hasira

Moyo wazidi kufura, kwa unayonitendeya,
Imetawala hasira,na kutoweka sheria,
Pasipokuwa nusura,mtu ataangamia,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Umenifanya ni chura,bwawa ni yangu dunia,
Na mimi ninakuchora,wewe mjanja wajua,
Tarehi ikisowera,tajiju na kujijua,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Kila nikikupa kura,ndiyo wazidi udhia,
Mnaniuzia sura,mnaniachia njaa,
Mwanipamba kwa bendera,shuka siwezi nunua,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Mali asili mwapora,wageni mwawatunukia,
Ardhi mwaisakura,wakuja mnawaachia,
Na hii mbaya bishara,kizazi kinachofatia,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Madini mmechakura,hongo mkazipokea,
Tunachokipata hasara,na mashimo kubakia,
Mabepari wanafura,nazidi kujikondea,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Weupe kama sungura,ujanja wamezidia,
Wasiosoma majura,nao mnawapokea,
Mashirika yadorora,kisa hamjakijua,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Kuendelea ibura,mzawa mkimuonea,
Kama hanayo tijara,nchi itadidimia,
Mkiikosa busara,tutazidi kuumia,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Kunazo sheria bora,na sheria za mabaa,
Nuksi zenye kukera,hutupa wanaojua,
Ndizo zizuazo hasira,tena na kubwa balaa,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Benki mnazipora,na hifadhi nazo pia,
Uchumi unadorora,wafana mnatwambia,
Zinakwisha barabara,mwanena tunaendelea,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Kwa ukubwa nchi mkwara,mikoa mwang'ang'ania,
Madaraka yamegura,hakuna wa kusimamia,
RC ni hasara, watu hawajamchagua,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

RC si busara, gavana twahitajia,
Mipango wataochora, mikoa kuendelea,
Nchi kubadilika sura, itutambue dunia,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Kenya sio masihara, wana katiba mpya,
Sisi tunaodorora,wa kwanza tulishakuwa,
Kuwa na watu kachara, matende yakazuia,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Lugha yetu yadorora,zingine twazitumia,
Japo twajua fikra,mizizi zimekataa,
Mataifa yalo bora,lugha zao yatumia,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Kwa kila kitu twadorora, hatuna tunalong'aa,
Ila tu kwa kujipara,nje wanatushangaa,
Mwendo nyuma zetu sera, masikini twabakia,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.


Ninaomba maghufira, Jalali kutuhurumia,
Tunshaipoteza dira,hatujui yetu njia,
Unapotea msafara,jangwani tulipokua,
Isagesage hasira,moyoni iliyojaa.

Mabruki

Nikidhani mamluki, ni watu tu wa vitani,
Hadi nilipohakiki, kama vile ya utani,
Na kuona halaiki, wapo pia mitaani,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Wengi hawaaminiki,watumiwa na sultani,
Mambo yao unafiki,wengine huwa shakani,
Yafaa mtaharuki,watawatia matatani,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Binadamu hapendeki,hata ukimthamini,
Dhamira yamshtaki,kwa kile anachothamini,
Na daima hatosheki,hadi kwenda kaburini,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Utampa ustahiki,vitendoye uzaini,
Mkubwa haheshimiki,pindi awapo gizani,
Na mdogo haaminiki,utapomweka dukani,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Wabaya ni marafiki,na wala sio wageni,
Na ndugu hawabebeki,huvunja zote mizani,
Na jirani huwashiki, husuda yawazaini,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Mke kwa mme fasiki,si mkweli nje na ndani,
Mme kwa mke fataki,hatosheki na hisani,
Maisha kama hilaki,na nuksi majumbani,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Sio kama nahamaki,sina ninachothamini,
Na wanaonidhihaki,si mizizi duniani,
Njia yangu mashariki,magharibi sijabaini,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Ayajuaye Khaliki,ya pamba au katani,
Historia kamiliki,kahifadhi ya zamani,
Naye hana mshiriki,ajua ya akheirini,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Nafusi haiamaki,yaendayo duniani,
Mimi sio mhakiki,badala siitamani,
Machache nimeafiki,kuyatia matendoni,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Husema sieleweki,na hilo naliamini,
Wajua sitingishiki,chini nashika makini,
Huona sitabiriki,wanalijua yakini,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Nyota yangu Mabruki,ahadi sina moyoni,
Hamnao wa laiki,nao hawajabaini,
Hadi azuke Buraki,kunipeleka peponi,
Iyeyushe hii chuki,ilonijaa moyoni !

Yafute haya machozi

Umeshanipa simanzi, tena kwa mingi miaka,
Hali hata huulizi,kwako nimekwishazikika,
Kwa hii yako ajizi,vibaya nimeathirika,
Yafute haya machozi,yaliyokwishatiririka.

Sijayajua mapenzi, ila ni kuhangaika,
Ingelikuwa maradhi, kwa kweli ningeponyeka,
Ila hili la faradhi, kulikosa nateseka,
Yafute haya machozi,yaliyokwishatiririka.

Si elimu sio kazi,sioni kinachofanyika,
Maisha sasa upuuzi,natamani kuondoka,
Ningelipata jahazi,nami ningejumuika,
Yafute haya machozi,yaliyokwishatiririka.

Hayanitoshi makazi,hapana panapokalika,
Lanijia jinamizi,usiku ninateseka,
Nachelea kuwa chizi,usiposhughulika,
Yafute haya machozi,yaliyokwishatiririka.

Yanalowana malazi, kitanda kinafurika,
Na mto huu siuwezi,umekwishasambaratika,
Na godoro hili uzuzi,ja kikojozi katwika,
Yafute haya machozi,yaliyokwishatiririka.

Wanaofutwa machozi,walahi wafarajika,
Hawanacho kizuizi,kupendwa watapendeka,
Ila mie sinakazi, ila ni kulalamika,
Yafute haya machozi,yaliyokwishatiririka.

Hadithi siimalizi, kwiki imeshanishika,
Jamani tena siwezi, sijui wapi pa kushika,
Natamani kwenye ardhi, sasa ningelimezeka,
Yafute haya machozi,yaliyokwishatiririka.


Yamenifika mtunzi, kumtaka asokutaka,
Nimejikuta bazazi, watoto wananicheka,
Mgonjwa sina muuguzi, nazidi kusononeka,
Yafute haya machozi,yaliyokwishatiririka.

Uponyeshe moyo huu

Kurudiana wataka, ombi sintolikataa,
Nafsi haina wahaka, ila moyo waugua,
Ni lazima kutibika, kabla sijauambia,
Uponyeshe moyo huu uliokwisha kuuvunja !

Kisa chake kuvunjika, wewe chote wakijua,
Ni pale ulipokiuka, za kwetu wenyewe sheria,
Na ukubwa kujivika, kujifanya unajua,
Uponyeshe moyo huu uliokwisha kuuvunja !

Kwa hasira kuropoka, na mambo kuuzulia,
Vibaya kukereheka, na kuchukia dunia,
Asubuhi kuamka, ukawa umekukataa,
Uponyeshe moyo huu uliokwisha kuuvunja !

Ukaapa na kuapika, hutoweza kurudia,
Utawa ukautaka,na misheni kuingia,
Na upweke kujivika,hadi mwisho wa dunia,
Uponyeshe moyo huu uliokwisha kuuvunja !

Ulikufa ukakuzika, na matanga kuanua,
Mara wazuka mzuka, huko ulikotokea,
Bado makubwa mashaka, hakika haujaijua,
Uponyeshe moyo huu uliokwisha kuuvunja !

Vipi nitaeleweka, moyo kuuangukia,
Nini kilichofanyika, hadi wewe kukuridhia ?
Mbona wanipa mashaka,ya balaa kulizua ?
Uponyeshe moyo huu uliokwisha kuuvunja !

Wengi tumedanganyika, kwa hao viruka njia,
Na tukijakugutuka, hakifai kitumbua,
Mchanga kimeudaka, kula hakitokufaa,
Uponyeshe moyo huu uliokwisha kuuvunja !

Nilikupenda hakika, nawe hili walijua,
Nikakushika kikaka, ndugu kukuchukulia,
Uhaini kukuteka, hilo sikulidhania,
Uponyeshe moyo huu uliokwisha kuuvunja !

Nierevushe Rabuka, hatua ya kuchukua,
Moyo wako umechoka, haupendi kuumia,
Upweke unautaka, kuachana na dunia,
Uponyeshe moyo huu uliokwisha kuuvunja !

Mnavyowapenda wenu

Laiti sisi wakata,tungelikuwa na chetu.
Tuwe wa kunatanata,zinawiri hali zetu,
Wenetu tungepakata,tuwalishe kila kitu,
Mnavyowapenda wenu, ndivyo tungependa wetu.

Malaika nakuita,mpendwa wetu mwenetu,
Njoo machozi kukufuta,hao tena si wenzetu,
Kipato chao chatweta,hatujaweza kufutu,
Mnavyowapenda wenu, ndivyo tungependa wetu.

Elimu tutajiburuta, uwe na watoto wa watu,
Zaidi tukikipata, hilo lisiwe deni kwetu,
Tungali tunatafuta, benki tena hatuna kitu,
Mnavyowapenda wenu, ndivyo tungependa wetu.

Wakubwa wameukata, jamaa sio wenzetu,
Azimio walifuta,ili tusipate kitu,
Ujamaa kuuchota,mazingaombwe kwetu,
Mnavyowapenda wenu, ndivyo tungependa wetu.

Zao turufu karata,geresha zote ni zetu,
Na sasa wanyatanyata,usultani jadi yetu,
Hatosana mwana mkata,ila utumwa ni wetu,
Mnavyowapenda wenu, ndivyo tungependa wetu.

Miaka itawasuta, ngoja nikwambie kitu,
Itajazusha utata, mvi zikaota kutu,
Migongo kuwakong'ota, akili zikawa butu,
Mnavyowapenda wenu, ndivyo tungependa wetu.

Kwa njaa mtajapeta,muukamate wenu utu,
Hapo hakuna kuteta,ila fukia sepetu,
Mguu tupu kuuwata,uje kuvaa viatu,
Mnavyowapenda wenu, ndivyo tungependa wetu.

Zama nilishakuita, uje ulimwengu wetu,
Miaka mingi kupita, ukawa kwenye msitu,
Sauti hukuipata, kwa dhiki za mtutu,
Mnavyowapenda wenu, ndivyo tungependa wetu.

Rwanda nilikwishapita, kuwasalimu Wahuru,
Watutsi wakaniponda, eti wale si wenzetu,
Kumbe kiyama waita,jinsi walivyothubutu,
Mnavyowapenda wenu, ndivyo tungependa wetu.

Kenya nilishawasuta, wakaniona si mtu,
Kuondoka kwa Kenyatta,kamwachia mtukutu,
Vilio anayeviita,maana si mtu wa watu,
Mnavyowapenda wenu, ndivyo tungependa wetu.

Kibaki alipogota, Mungiki akawa chatu,
Odinga naye kanyata, akiyakwepa matatu,
Kisumu hadi Mvita, ikatembea mitutu,
Mnavyowapenda wenu, ndivyo tungependa wetu.

Ndoto hatujaiota, hapa kisiwani kwetu,
Amani tumeichota, hauvuji mtungi wetu,
Ila mizimu yaita, kila msiba na tatu,
Mnavyowapenda wenu, ndivyo tungependa wetu.

Kwa haki au dhuluma

Kiogopeni kiyama, kwa zenu hizo amri,
Mwatenda yenye dhuluma, utadhani makafiri,
Kupunja sasa azma, si mkaaji si msafiri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Nusura imeshahama, imebaki tahariri,
Zaja mbegu za nakama, kuzipanda si hiari,
Ni nani wa kulalama, eti ndani kuna kheri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Pastahilipo heshima, pabakia makaburi,
Kwingine kote zahama,kwa kiburi na jeuri,
Ni nani mwenye huruma,watawala waso kheri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Ubinafsi wavuma, wavuja sio kadri,
Watoto na wao mama, baba naye adhikiri,
Kabaki peke yatima, maisha yamuathiri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Ukabila wa kichama, wapashwa kwenye tanuri,
Nchi kuja kuichoma, kama ilivyodhihiri,
Wataimba usalama, huku hali ni hatari,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Na mahala pa heshima, kinyume kinadhihiri,
Pema si tena pema, pameingia ya shari,
Mnyonge sasa agoma,kwake hakunayo kheri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Ni nani asiyekwama,katika yake kadiri,
Nafsi zinatuhama,twamuachia Ghaffuri,
Twafunga zetu kalima,twaila yetu shubiri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Eneo utalihama, ikishatoka amri,
Fidia hutoifuma, ukipata ni sifuri,
Twenda mbele twenda nyuma, nashindwa hili kariri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Maombi utayatuma, mikopo kutafsiri,
Zitakukweza gharama,na riba bila urari,
Ujenzi utasimama,na benki kukuadhiri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Na ukienda kulima, hukukwaza usafiri,
Ukivuna utadema,hasara kukuhasiri,
Utajihisi yatima,kitanzi kukitabiri,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Ajira sasa hujuma,utabakia fakiri,
Zimekimbia neema,madhara yameshamiri,
Tabaka zinakunjama,madaraja si hodari,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Mdhibiti yuko nyuma, jina laalika shari,
Wazibebao tuhuma, mbona hawatiwi kabari,
Nani abebe gharama,maisha kuwa kamari,
Ni amri ya Ikulu, kwa haki au dhuluma.

Mipango mji

Mji mipango wataka, kila hali kuvutia,
Si nyumba tu kujengeka, bali pia na majaa,
Misingi bugi kuweka, iwe misafi mitaa,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Kazi kustaarabika, ni vita kupigania,
Hujui wanakotoka, watu wanaoingia,
Tofauti ya hulka, pia nayo mazoea,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Sheria budi kuweka, watu kuwasimamia,
Yawe yanayofanyika, kote yanakubaliwa,
Na yasiyokubalika, watenzi kuadhibiwa,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Haiwezi kujengeka, miji isiyotulia,
Mabomu yatalipuka, watu wabaki walia,
Uchafu utatukuka, uozo ukaenea,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Na maji yatamwagika, hakuna wa kuyazoa,
Mioto italipuka, maafa yakaingia,
Magonjwa yatalipuka, watu wengi kupotea
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Mwenyeji hufurahika, mji msafi ukiwa,
Huacha kulalamika, sifa nyingi kuzitoa,
Watoto hushereheka, mji wao kujivunia,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Wageni humiminika, kuja kuwasalimia,
Miezi hadi miaka, wakawa wanaoingia,
Mji hugeuka Makka, Hija watu kuhijia,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Watalii watafika, na sifa nyingi kutoa,
Wengine huwaalika, kuja kututembelea,
Kipato kikaongezeka, shida zetu kupungua,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Diwani mnuka taka, hafai kuvumilia,
Mtaa huaibika, naye kadhalika pia,
Mtupe kwenye kichaka, kisha na moto kutia,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Meya kama takataka, nini awasaidia ?
Harufu mbaya huweka, na nyie mwapendezewa?
Uoza mkiutaka, magonjwa huwatembelea,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Mbunge mwenye kunuka, huleta harufu mbaya,
Jimbo halitokalika, ushuzi unaonukia,
Vipi huyu mwamuweka, au nyie zimepungua?
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Wakuu wanahusika, wa mikoa na wilaya,
Kukosa kustaarabika, nao wanavumilia,
Hawa watu wa mashaka, mbele hatutasogea,
Mipango mji lazima, kuvutia watalii.

Tofauti ya mjanja

Trekta moja latosha, mjanja kutengeza mengi,
Gari moja humuwezesha, kuleta yake shangingi,
Kompyuta mbili tosha, kuziunda zake nyingi,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Simu chache zinatosha, kuunda chake kiwanda,
Mtambo uliokwisha, wa mgodi huko Rwanda,
Mjanja humuwezesha, mitambo yake kuunda,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja huona nje, hatafuni tu vya ndani,
Ili watu asipunje, ajua kwenda ugenini,
Yeye sio mwana njenje,ufukara sio chanda,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja hampi kazi, mgeni mwenyeji afe,
Hana jana wala juzi,halisimami lake tufe,
Na mjomba na shangazi,kwa hili moyo wasife,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja si mnunuzi, bali mtengenezaji,
Kama sivyo mchuuzi,huu ndio wake mtaji,
Kuelea ndio hadhi,mjinga aenda na maji,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja mali yake watu, mjinga maliye vitu,
Pakizuka utukutu, hujikuta ni kiatu,
Mwenye mbili si tatu,na jembe haliwi ratu,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja huishi pacha, kama hai kama mfu,
Nalo kwake si Alinacha,bali wingi wa sharafu,
Mcha Mungu hatoacha,hali hii kuiafu,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja hayahujumu, kamwe yake mazingira,
Na kwalo akikutuhumu,kali yake hasira,
Huwa wakati mgumu, kwako kupata maughufira,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja hawaajiri, fala na wasiojua,
Huwa hachezi kamari, na mradi wenye ulua,
Malengo yake kadiri,ujinga hakuzoea,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja hawi kipofu, mkataba akisaini,
Kwake hili la wakfu,hakubali uzaini,
Hucheza yake turufu,nchi yake huthamini,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja sio fisadi, wananchi kuwaibia,
Wala sio mkaidi, nchi kuwaharibia,
wala sio mritadi, ukoloni kurudia,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Mjanja hawi mfumo, kila kitu kutawala,
Ajua chake kikomo, desturi pia mila,
Na huzuni na nderemo, kwake hayana kabila,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Kila mtu ana zake, wahenga wasema nywele,
Waume na wanawake, wazima na wenye ndwele,
Mwanzo, mwisho ni mwnenzake, na chini ina kilele,
Tofauti ya mjanja, na asiye mjanja.

Ujauzito wa moyo

Usiombe kuwa nao, ujazito wa moyo,
Omba uepushwe huo, usife kwa jakamoyo,
Ni pepo wa vipepeo, viumbe wapepeao,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Ujauzito wa hila, wa mengi tuyatakayo,
Fikira na masuala, wakubwa wapuuzayo,
Ni jumla kwenye sala, na sadaka watoayo,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Hutesa ukiwa macho, fikra kuwa kaziyo,
Kwa dhahiri na kificho, huwaza yale yasiyo,
Husaga kama pikicho, ya chini juu yawayo,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Mimba ya maendeleo, mashujaa wabebayo,
Haina katu uzio, kutesa nyoofu nyoyo,
Mema wawatakiao, wenzao bila uchoyo,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Si uongo ninenayo, ni wengi wawajuayo,
Roho mbaya wakataao, na washindao choyo,
Mitihani wavukao, na ng'ambo wasogeao,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Ni chini warudiao, wakapafanya makao,
Wanyonge wanyanyuao, ili kuja juu nao,
Na ukubwa wacheleao, usio katu mafao,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Si bendera wapepeao, wananchi wawavungao,
Ni jasiri wa matao, na uchumi wajengao,
Ni amiri wa mgao, haki waisambazao,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Si kwa sifa watembeao, ila mbegu waletao,
Si mashabiki wa bao, bali waletao ngao,
Wanyonge lao kimbilio, ndio kubwa tegemeo,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Watu wa matarajio, ndoto watafsirio,
Na mwanga wauletao, si gizani wakaao,
Pia na wazungukao, mwangani wawachukuao,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Ujauzito wa moyo, ndoto zake za kioo,
Muhali urejeshao, maono ya matokeo,
Na wa nje wajuao, ni wachache wapatao,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Ujauzito wa moyo, ni simanzi ubebao,
Kwa yote uonayo, na hayo usikiayo,
Na yake matamanio, kuwa nao kifananio,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Ujauzito wa moyo, washinda ule wa tumbo,
Ni mengi myasemayo, siyajali majigambo,
Ni walevi mlewao, kila aina ya tembo,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Machache myajuayo, ila ndio mjionao,
Waibaji vidakao, hupora vyetu na vyao,
Ukubwa wautakao, japo sio wajengao,
Ujauzito wa moyo, hakika mgumu mno.

Nyumba kwa kila kaya

Ndoto zingine uchizi, ota kinachowezekana,
Sitaki kupiga mluzi, waelewa waungwana,
Zimepita fumanizi, na ahadi za laana,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Msusi sio kinyozi, hili si la kubishana,
Na viazi sio ndizi, ijapo vinalingana,
Mmoja juu hawezi, na mwingine chini huchina,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Baradhuli na bazazi, hawajui la maana,
Saa zote kinywa wazi,japo mambo si bayana,
Kwao fikra si kazi, kwa hewala ni watwana,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Nchi haipandi ngazi, hadi makazi kusana,
Wananchi wawe wakazi, si wakimbizi aina,
Hayahitaji mjuzi, haya yako wazi sana,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Haugharimu ujenzi, twamiliki zote zana,
Vifaa havina kazi, rahisi kupatikana,
Fundi wako kwa majozi, kila fani waoana,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Nchi yetu pandikizi, viotani twabanana,
Magenge yetu makazi, na hamna muamana,
Roho mbaya twatarizi, choyo na nyingi hiana,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Nchi yetu bado wazi, mbona tunaumbuana,
Wanazuka majambazi, tuliowapa dhamana,
Wauza viwanja wazi, kisa twataka banana,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Vyauzwa viwanja wazi, huku twavumiliana,
Watoto wakosa malezi, bado tunachekeana,
Wehu twawapa hifadhi, nchi yazidi gongana,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Twasemwa ni wapuuzi, wala akili hatuna,
Mambo yetu ya kishenzi, wala sio waungwana,
Hili wala hatuwazi, ni kama sawa twaona,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Ufukkara sikuhizi, ni sifa yenye laana,
Hukuhama wanunuzi, mbaki kuangaliana,
Nao pia watembezi, wakawa hawaji tena,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Umasikini kitanzi, wenyewe tunanyongana,
Nchi yataka wajenzi, sio vitu vya Wachina,
Nchi yataka makuzi, na sio kuchomoana,
Nyumba kwa kila jamaa, hii inawezekana.

Washikeni watu hao

Washikeni watu hao, na mzidi kuwapenda,
Ila ndoto moyo wao, hapa kwetu kuupanda,
Si chungwa ni malimaokwao hawaachi kudanda,
Mwisho ndege watapanda, kusanzuka kwenda kwao.

Wapi mti uoatao,kwenye yetu miji kenda,
Mmea uchanuao, bila mizizi kutanda,
Na matunda wachumao, kwenye mgongo wa nunda,
Mwisho ndege watapanda, kusanzuka kwenda kwao.

Ni wahenga wasemao, kizazi kujakifunda,
Ulimwengu mtukwao, ndio ufalme huundwa,
Vigumu waponda chao, kokote kuja kupanda,
Mwisho ndege watapanda, kusanzuka kwenda kwao.

Mbwani hawa watokwao, tena na mwingi udenda,
Kwa wageni waingiao,na pasenti zawaganda,
Mithili neema yao,ni cha mauti kitanda,
Mwisho ndege watapanda, kusanzuka kwenda kwao.

Hesabu kila wajao, tunajivalisha sanda,
Ila kwa wachache wao,utu wanaoulinda,
Wengine wahamishao,hawa watu wa kuwinda,
Mwisho ndege watapanda, kusanzuka kwenda kwao.

Ni mfupi wetu upeo, si wa nyumba bali banda,
Na hao watembeao, macho yao yajipanda,
Waonalo si kioo,bali hali kama chanda,
Mwisho ndege watapanda, kusanzuka kwenda kwao.

Hawajui wajuao, japo wavaa magwamda,
Mchina kwake salioumeshindwa unda Honda,
Mtabaki mnunuao,wala si watu wa viwanda,
Mwisho ndege watapanda, kusanzuka kwenda kwao.

Hawa wamchunguao, kwanini haruki kinda,
Si wajua wajuayo, kama kweli hajapinda,
Waso mbawa warukao,chini lazima kudunda,
Mwisho ndege watapanda, kusanzuka kwenda kwao.

Ndio wajulikanao, wapiganao kwa munda,
Hao hao wachechemeao,kwa shukrani za punda,
Ninasema mtukwao,japo kote mtaranda,
Mwisho ndege watapanda, kusanzuka kwenda kwao.

Tanzania nipendayo, maskini wangu nyonda,
Laana yako kilio,kwa fikra za mgando,
Liwapi lako kimbilio,wanapotawala nunda,
Mwisho ndege watapanda, kusanzuka kwenda kwao.

MCHWA

Siku ya kuangamia, mchwa huifurahia,
Mbawa atazawadiwa,na angani akakwea,
Huku na huku kupaa, aranderande na njia,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Mwenyewe hufurahia,mbumbumbu bila kujua,
Mauti yamngojea, njiani asikojua,
Ghafla hushtukia, Ziraili amchukua,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Haya ndiyo ya dunia, na jinsi inavyokua,
Uombacho utapewa, ovyo au cha kukufaa,
Na vingine mwajaliwa, ajali kuwaletea,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Laiti ungelijua, gari usingepokea,
Kwamba laja kukuua, na siku hazijafikia,
Na nyumba usingekaa, kama waja kuvamia,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Mafuu hufurahia, pasipo kuomba dua,
Mwenyewe akiaminia, uwezo wake wazua,
Neema hujichotea,shukrani kuzuia,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Muumba yote ajua,na riziki huzigawa,
Hachagui kama mbaya,au anayemnyenyekea,
Wote atawapatia,mbaya kumzidishia,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Viumbe huwashangaa,kumnyima japo dua,
Ila hatopungukiwa,hata bilioni mkiwa,
Wangali wanaojua,wao wamhitajia,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Heri wasiojaliwa, hawana la kulijutia,
Mwepesi wauchukuam mzigo walokabidhiwa,
Na deni lao walijua, sio la kuwashadidia,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Wale wanaojaliwa, hisani kutotambua,
Gogo watalichukua, chini likawashindilia,
Hapana wa kuwanyanyua, siku itakapoingia,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Cha heri kilichokuwa, motoni huja watia,
Duniani huanzia,masahibu kuwavaa,
Wengi huchanganyikiwa,baadhi kuwa vichaa,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Katu sintoajabia, wazuzukao jamaa,
Kwingine hawajajua,na hawajaangalia,
Pepo zinakoendea,na misimu tarajiwa,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Siku ya kuangamia, mchwa hushangilia,
Mabawa anayopewa,hayeshi kumzuzua,
Huruka na kuingia,kwenye taa kujifia,
Siku ya kuangamizwa,mchwa huzawadiwa mbawa.

Mbuyu uangukapo

Ardhi hutikisika,mbuyu ukianguka,
Hadi mbali husikika, watu kote wakastuka,
Huuliza na kumaka, ni nini kimefanyika,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.


Mbuyu mti wa hakika, umbo lake lasifika,
Hudhani umegeuka, matawi juu kuwekwa,
Majani yake ya shaka,mizizi huhadaika,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Mti umerehemeka, kwa kina umejengeka,
Na wengi huogopeka, eti mizimu waweka,
Watu huwa na wahaka, usiku unapofika,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Mti unaabudika, kwa wale wenye shirika,
Matambiko hufanyika, mizimu kubembelezeka,
Kwa kafara na sadaka,madhabahu hujengeka,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Ukishika umeshika, katu hautaterereka,
Hana vuli na masika, kote unaneemeka,
Na mabuyu huzalika, watoto wanayoyataka,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Upepo huamanika,kuangusha ukitaka,
Kiuno utajishika,na kwenda kupumzika,
Na pumzi zitaushuka,nguvu bure kuharibika,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Amejalia Rabuka, na watu ni kadhalika,
Wajao kurehemeka, kwa nguvu kuneemeka,
Au mali kujashika, kwa hali kutakatika,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Kama mbuyu hujazuka, wakawa na patashika,
Hawataki kushindika,wala kuja kukwazika,
Watazua hekaheka,tufani nazo gharika,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Ukubwa watautaka, wengine kunyanyasika,
Viumbe kudhalilika, wao ndio hufurahika,
Jeuri watapeleka,hata kwaye mtukuka,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Ujibari hujivika, wasiwe nao wahaka,
Vioja huibuka, kama Amin mtajika,
Na siku inapofika, mbuyu utaanguka,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Jibari atadondoka, wasifu kuporomoka,
Hakuna atalodaka, ila wingi wa mashaka,
Dunia humgeuka, na kujiona kichaka,
Mbuyu uangukapo,ardhi hutikisika.

Somo lipo vijijini

Nchi yetu kuendelea, vijiji budi kukua,
Haya tunayoyalea, tunakokwenda kubaya,
Vijiji vinadumaa, huku miji inakua,
Somo lipo vijijini,wala sio ugenini.

Mtume hajatokea, vijijini kwenda kaa,
Darasani kuingia,maisha yanavyokua,
Kisha atapoelewa,vitani kuja ingia,
Somo lipo vijijini,wala sio ugenini.

Mengi akiyagundua, shahada ataikwaa,
Utafiri kuzindua,tatizo lilipokuwa,
Na majibu maridhia,kichwani yakatulia,
Somo lipo vijijini,wala sio ugenini.

Barabara zapotea,kusikokuwa na njia,
Nyoka walikojaa,sumu wanaotupia,
Pasipo pakutokea,vipi soko kufikia,
Somo lipo vijijini,wala sio ugenini.

Maji ni ya kuchimbua,kama madini watoa,
Kote tope yamejaa,wahofu kuyatumia,
Wao wanywa, kufulia,ndicho walichojaliwa,
Somo lipo vijijini,wala sio ugenini.

Nchi yazidi kukua,huku maji yapotea,
Bomba zinang'olewa,mifumo imechakaa,
Sasa kazi imekua,maji kujitafutia,
Somo lipo vijijini,wala sio ugenini.

Umwajiliaji hadaa,wahandisi ruia,
Ni vipi utajiundia,kitu bila fundi kua,
Nchi bado imezubaa,twashindwa kujitegemea,
Somo lipo vijijini,wala sio ugenini.

Shule zimetapakaa,walimu wamepotea,
Ujinga tunaulea,karne inayoingia,
Huko nje twajivunia,tumeshapiga hatua,
Somo lipo vijijini,wala sio ugenini.

Watu bado kujijua,ni nani wa kuwaokoa,
Pipi wakishapatiwa,waona wamefikiriwa,
Vyama vingi wadhania,damu vitakujawatoa,
Somo lipo vijijini,wala sio ugenini.

Hawajui demokrasia,kazi ni kuwapigania,
Ukiritimba kukataa,chama kinachowalemea,
Katiba mpya kutwaa,viongozi kuwafua,
Somo lipo vijijini,wala sio ugenini.

Umeme haujaingia,kama waja hatujajua,
Giza linapoingia,ndio mwisho wa dunia,
Sayansi inaviambaa,vijiji vinasinyaa,
Somo lipo vijijini,wala sio ugenini.

Wenzetu wanaelewa, sola wanazitumia,
Miradi wameamua, nyumba zote kuwa na taa,
Sisi gizani twabakia,porojo twashangilia,
Somo lipo vijijini,wala sio ugenini.


Misaada inatolewa,juu kwa juu yaliwa,
Siasa zatapakaa,na ushirikina pia,
Watu mengi wachelea,vigumu kujikomboa,
Somo lipo vijijini,wala sio ugenini.

Kwanini ni masikini

Sisi sio masikini, ila uongozi duni,
Fikra za walakini, ndizo tunazothamini,
Na twawaona wageni, eti ndio wenye thamani,
Wenyewe hatujithamini, vipi tuwe na thamani ?
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Hawamjui Auni, na fikra Muhayamini,
Nadra kwa afueni, kwenda kwa watu wahuni,
Unyama na uhayawani, sio ya kwetu amini,
Uungwana duniani, huanzia kwako nchini,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Mbele sana hatuoni, njaa yetu twabaini,
Kaumu haina ihsani,na mifumo walakini,
Dira yetu ni maoni,na wala sio ramani,
Tatizo hatulibaini,vipi uishe umaskini ?
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Nafsi zetu lawamani,si watu wenye imani,
Vitabu hatuvioni,Kuvisoma si yamkini,
Vitakatifu shakani,vya kawaida kapuni,
Wamezuka wajuwani,kila kitu wabaini,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Vinara hukaa ndani, nje kwenda si yakini,
Hawatafiti asilani,wajue vyote viini,
Kwa mtu kutathmini,na taasisi nchini,
Twabahatisha mizani,vipimo viso razini,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Asiyeelewa ni nani, nchi ina ukubwa gani,
Kuitawala kitini,au pawe ni mezani,
Huwezi mwana yamini,ni usanii na utani,
Mkoa sio zamani,ni nchi kwa humu ndani,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Wenyewe jifundisheni, wakuu elimikeni,
Lugha yetu ni auni, tuanze kuithamini,
Dhana zote za thamani, tuziongelee kwa undani,
KIswahili kwa yakini, ndio dawa ya umaskini,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Nani lugha za kigeni, zawa kwao fikrani,
Zinasinyaa na fani, vipaji vyawa laini,
Mawazo ni mgandoni,hatuyajui ya mbeleni,
watu ni shairi guni,haifai kulighani,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Rasilimali nuksani,zinawafaa wageni,
Mwenyeji si afueni,atajali kitu gani,
Twazidi mjaza madeni,Kichwani na miguuni,
Atembee namna gani, atoke humu jangwani,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Mifumo kitu makini, nafasi sasa ipeni,
Nani hapa duniani,haondoki madarakani,
Mmoja tukimuaminitutaingia mashakani,
Vichaa watatuahini, wakija uongozini,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Hii ni yangu imani,na msingi wa amani,
Watu wawezesheni, waukimbie umaskini,
Raia wa kuamini,aliye na kitu tumbuni,
Vinginevyo mwajizaini,yatawatokea puani,
Masikini wa fikra, si masikini wa mali.

Kilicho'za kimeoza

Kilicho'za kimeoza, hakiwezi acha nuka,
Kunukia miujiza,hata marashi 'kipaka,
Huzuii la kuoza,hili lataka kuzika,
Hata upake marashi,kilicho'za kimeoza.

Hata marashi puliza,harufu haitotoka,
Cha kuoza cha kuoza,tabia yke kunuka,
Chongo halwi kengeza,ndivyo ilivyo dunia,
Hata upake marashi,kilicho'za kimeoza.

Cha kuoza kimeoza,acha kuhangaika,
Japo alikuwa mwenza,hutoweza kumshika,
Kwa nisai na ajuza,desturi ni kuzika,
Hata upake marashi,kilicho'za kimeoza.

Kwangu kinachotatiza,hali ilivyobadilika,
Wangali hai waoza,kwa tabia na hulka,
Hali hii yawaponza,watu hai wananuka,
Hata upake marashi,kilicho'za kimeoza.

Uchu wa cheo waiza,macho wengi hupofuka,
Mwenyewe hujilemaza,kuvaa kustahika,
Siachi kujiuliza,vipi atasetirika ?
Hata upake marashi,kilicho'za kimeoza.

Waungu wajitangaza, na hali wananuka,
Kaumu wanaibeza,eti wanatamanika,
Maiti sasa ni wenza,kitandani twashereheka,
Hata upake marashi,kilicho'za kimeoza.

Fisadi twapatiliza,huku tunajumuika,
Tena twazidi wakuza,daraja wanazovuka,
Likija ingia giza,sijui nani atatoka,
Hata upake marashi,kilicho'za kimeoza.

Wavivu tunawaoza,kwa vyeo kuwajibika,
Ajizi zinapoanza,jukwaani twalalamika,
Malezi yetu yakwaza,jamii kutajirika,
Hata upake marashi,kilicho'za kimeoza.

Vigumu nawaeleza,nchi kuweza jengeka,
Huku tunafuga funza,madaraka kuja shika,
Vidole kuviongoza,twende tunapopataka,
Hata upake marashi,kilicho'za kimeoza.


Kuzoza nilikizoza,si mtu wa kusikika,
Hodari waliojifanza,waona wameelimika,
nini utachowafunza,waweze tena kushika,
Hata upake marashi,kilicho'za kimeoza.

Yangu sasa namaliza,cheo sitaki kushika,
Najificha na ajuza,shaibu nimetosheka,
Anijalie Muweza,hatima kurehemeka,
Hata upake marashi,kilicho'za kimeoza.

Tumbo

Tamaa mama wa baa, na baba yake msiba,
Tumbo ujazo twajua, vipi zaidi wabeba,
Au hayo mazoea,ya kuhodhi si kushiba,
Tumbo kushiba kiroba, mbona wahodhi gunia?

Mboba wahodhi gunia, hali kushiba kiroba,
Tumnbo unafakamia, huoni hiyo ghiliba,
Huwezi ukachukua,zaidi ya unachobeba,
Tumbo kushiba kiroba, mbona wahodhi gunia?

Au sasa ni ngamia, huweza weka akiba,
Nundu utaikwaa,mgongoni kuibeba,
Jangwani usife njaa,japo wabeba mikoba,
Tumbo kushiba kiroba, mbona wahodhi gunia?

Kula madai ya njaa,hauli kama wakwiba,
Tumbo lataka chukua,kiasi linachokibeba,
Mashine kukokotoa,unaofaa mraba,
Tumbo kushiba kiroba, mbona wahodhi gunia?

Mwili wataka kujaa,kadhalika na haiba,
Kitambi chaoghofya,Kikizidi kwa ukbwa,
Mimba waweza mdhania,yule anayekibeba,
Tumbo kushiba kiroba, mbona wahodhi gunia?

Uungwana ni kinaya,japo waweza kushiba,
Zaidi ya inavyotakiwa,hali wengine washiba,
Tosheka cha kutumia,uache pia jazba,
Tumbo kushiba kiroba, mbona wahodhi gunia?

Kula utakacho pia, kasma haba na haba,
Mradi kinavutia,na unapata kibaba,
Maisha kushangilia,wala si kama msiba,
Tumbo kushiba kiroba, mbona wahodhi gunia?

Acha wenzko kutwaa, kiasi cha wao kushiba,
Usifiche cha kuliwa, uvundo kisije beba,
Ndani huja kukuozea,hili halinayo toba,
Tumbo kushiba kiroba, mbona wahodhi gunia?

Choyo daima kimbia, hili huvunja nasaba,
Waliotutangulia,kama vile masahaba,
Hili walilikimbia,hawakukubali ghiliba,
Tumbo kushiba kiroba, mbona wahodhi gunia?

Chonyo ni mwana izaya,inda mkaza mjomba,
Jamaa hupelekea,wasitoe marahaba,
Na shikamoo kukataa,japo ni yao swahiba,
Tumbo kushiba kiroba, mbona wahodhi gunia?

Israfu nayo kataa,japo una kabakaba,
Wenye shida angalia,uwape chao kibaba,
Na yatima kuwalea,wausahau msiba,
Tumbo kushiba kiroba, mbona wahodhi gunia?

Mwogope mwenye kutoa,kwa mtaji pia riba,
Talanta kuzitumia,kama ilivyo akraba,
Na siku ya kushuhudia,wakiri hata bawaba,
Tumbo kushiba kiroba, mbona wahodhi gunia?

Bawabu

Bawabu ninaumia, lakini navumilia,
Kazi yangu kuning'inia,mlango nikishikilia,
Sitoki ninapokaa,wala sijui kutembea,
Bawabu ninangojea, siku ya kwenda tembea.

Nala nilipojengewa,nalala ninapokaa,
Chini siwezi kukaa,Kusimama nimezoea,
Mchana hunizingua,kufunga na kufungua,
Bawabu ninangojea, siku ya kwenda tembea.

Usiku ninaugua, ninashindwa kupumua,
Zinafungwa zangu mbawa,siwezi kujiachia,
Na nyimbo huniishia,ninabaki nasinzia,
Bawabu ninangojea, siku ya kwenda tembea.

Umbo langu ni sawia,mdogo wala sijakomaa,
Ila nabeba dhiraa,wengine zaweza ua,
Kulalama sijajua,utumwa nimezoea,
Bawabu ninangojea, siku ya kwenda tembea.

Ila ninaingojea, siku ya kwenda tembea,
Kwingine nikakujua, mageni kujionea,
Mathalani Tanzania,mikoa na zake wilaya,
Bawabu ninangojea, siku ya kwenda tembea.

Nataka pia dunia, kusafiri na kujua,
Nifike huko Ulaya,barafu kujionea,
pia na huko Asia,maendeleo kujua,
Bawabu ninangojea, siku ya kwenda tembea.

Magharibi kuwachia,mashariki nikajua,
Pepo zenye manufaa,niweze kusafiria,
Niabiri abiria,hata nisikokujua,
Bawabu ninangojea, siku ya kwenda tembea.

Niione na Russia, na China ya kijamaa,
Kwanini waliukimbia,na sisi twautamia,
Nako kusini Korea,Kaskazini nako pia,
Bawabu ninangojea, siku ya kwenda tembea.

Na Mashariki Ulaya,hali sasa kuijua,
Majengo yaliyojaa,lakini bado kuna njaa,
Na Cuba alikozaliwa,Castro mwana mjamaa,
Bawabu ninangojea, siku ya kwenda tembea.

Niende nako India,pamwe nako Malaysia,
Siri yao kugundua,ufukara kuung'oa,
Na sayansi kuivaa,kuileta nyota ya jaha,
Bawabu ninangojea, siku ya kwenda tembea.

Brazili nako pia,mitambo kuitambua,
Na akili ya kuvumbua,Afrika kujinasua,
Tuache tu kununua,vingine kuvivumbua,
Bawabu ninangojea, siku ya kwenda tembea.

Na askari wa dunia,ninataka kumjua,
Marekani mwenye waa,mtata wa jema kujua,
Nafsi inayemsumbua,mguu anapotia,
Bawabu ninangojea, siku ya kwenda tembea.

Nijue Australia, na kangaroo pia,
Aidha Scandinavia,theluji ilikojaa,
Weupe wa kweli kujua, nazo mosi familia,
Bawabu ninangojea, siku ya kwenda tembea.

Vuvuzela si mmbeya

Si wanawake wambeya, bali wenye mambo mia,
Pumzi wasiotua, habari kukushushia,
Na kuroroma tabia, na hasa ukiishiwa,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Vuvuzela domokaya, hajui la kuchagua,
Na atazungumzia, hata asiolijua,
Na ubishi huvamia, bila asili kujua,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Maneno kama mvua, isiyokubali jua,
Kisima chake hujaa, japo siyo yanayofaa,
Mdomo kuufunua, kama saluti kutoa,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Hakuna asilojua, Vuvuzela nakwambia,
Na mengine huyazua,matope akakupakaa,
Ni mtu wa kuhurumia,kwa maneno ni kichaa,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Haachi kuyarukia, kila analosikia,
Nguo aweza kuvua, hadharani kwa butwaa,
Ni mwenye kujisifia, japo hajajiangalia,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Vuvuzela litalia, hata usipokosea,
Lawama huwa lazua, wakati lafadhiliwa,
Ushindi kuuchukua, muhali haijatokea,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Vuvuzela linalia, kipato kikipungua,
Kitu aking'ang'ania,kama usipompatia,
Utakesha waimbiwa,lepe hutolitambua,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Umbeya akiletewa, hawezi akachungua,
Vuvuzela litalia, jirani wakalisikia,
Na machozi litatoa, eti kwamba laonewa,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Vuvuzela ni mkia, kichwa ni nadra kuwa,
Sapoti huweza toa,pale pasipotegemewa,
Matatani ukaingia,usijue pakutokea,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Vuvuzela hutimua, ndugu na pia jamaa,
Kwa kelele kuzidia,hadi wakachanganyikiwa,
Hamna wa kulisifia, "Arsenal' walikataa,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Mpira ukiangalia, kulala litakwambia,
Ukitaka kutembea,sababu litaizua,
Kwanini leo yafaa,nyumbani ukabakia,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Kama ulishachagua, Vuvuzela kununua,
Na nyumbani limejaa,basi ndugu vumilia,
Hatima yako ngojea,ya taabu na udhia,
Vuvuzela si wambeya, ila wake domokaya.

Diwani fungua macho

1.
Waweza boresha kata, si kama ilivyokua,
Yaweza isha matata, kata ikajitanua,
Wawza maliza ukata, kampuni mkikwaa,
Diwani fungua macho,waweza boresha kata!
2.
Diwani ni kama nta, umoja ukatokea,
Hamasisha wana kata, vikao wapate kaa,
Maamuzi kuyakata, mengi yenye manufaa,
Diwani fungua macho,waweza boresha kata!
3.
Maendeleo ni vita, katika yetu dunia,
La sivyo mtapakata, umaskini sawia,
Neema hamtoipata, hadi mwisho wa dunia,
Diwani fungua macho,waweza boresha kata!
4.
Kata lazima kuota, ndoto zenye majaliwa,
Msikubali kusota, wengine wanakimbia,
Boresheni Mkukuta, muweze kuja kupaa,
Diwani fungua macho,waweza boresha kata!
5.
Wenngine wanawasuta, na pia kuwanyanyapaa,
Neema hamjatafuta, vijiweni mnakaa,
Za mchana mnaota, ndoto zisizowafaa,
Diwani fungua macho,waweza boresha kata!
6.
Fikra hamjapepeta, rai kuzichanganua,
Yapo mambo mia sita, chache mwaweza chagua,
Na hapo mkajikita, mazuri kukokotoa,
Diwani fungua macho,waweza boresha kata!
7.
Ubinafsi wawasuta, madalali wa mitaa,
Mwauza hata viota, wapi ndege watakaa?
Historia mtadata, itawachora vibaya,
Diwani fungua macho,waweza boresha kata!
8.
Diwani acha kuteta, neema budi kuzua,
Na wala usije ota, utakuja kuizoa,
Haipati maji kata, bila mtungini kwingia,
Diwani fungua macho,waweza boresha kata!
9.
Usiwe wa kupitapita, majilisi hujakaa,
Wakazi nao kuteta, ndio njia ya kuanzia,
Mawazo mkayavuta, matatizo kugundua,
Diwani fungua macho,waweza boresha kata!
10.
Ufumbuzi kutafuta, kero zilizoenea,
Diwani kavae ngata, mtungi kichwani tia,
Na kama kucheza kwata, gwardi kuparamia,
Diwani fungua macho,waweza boresha kata!
11.
Diwani usiwe mtata, mtu wa watu jua,
Madhambi yote kufuta, wewe yakutegemea,
Itakate yenu kata, ing'are kuliko sinia,
Diwani fungua macho,waweza boresha kata!
12.
Diwani rai tafuta, na elimu kimbilia,
Usijefanye dokata, la saba halijatimia,
Watakuona kiputa, nundu kuja kukulemea,
Diwani fungua macho,waweza boresha kata!
13.
Natupa yangu karata, geresha halijanifaa,
Ukiona unatota, bafuni hujainigia,
Basi tambua mafuta, mwilini yamezidia,
Diwani fungua macho,waweza boresha kata!

Mbunge jimbo ni lako

1.
Mbunge umepotea, mwenzetu hatukuoni,
Siku tulipokuchagua, ulitupa nyingi imani,
Wewe kukutegemea, kutuondoa mashakani,
Mbunge jimbo ni letu, usije ukaturusha!
2.
Mwisho kututembelea, hatukumbuki ni lini,
Ahadi ukazitoa,zote kwishia mitini,
Kinyongo chaning'inia,nyongo watu tumbueni,
Mbunge jimbo ni letu, usije ukaturusha!
3.
Habari zimeenea, waishi ughaibuni,
Umukua milionea, tena wa matrilioni,
Umaskini wachukia, utakutumbua ini,
Mbunge jimbo ni letu, usije ukaturusha!
4.
Hewa utakuchafulia, wanuka umasikini,
Huwezi kuvumilia, kuona waso thamani,
Na waziri umekua, sikuzote safarini,
Mbunge jimbo ni letu, usije ukaturusha!
5.
Hakuna tulilopangua, mipango hukubaini,
Halipo lililopotea, kwetu hukuwa na thamani,
Hapana kilichochipua, vilifia ardhini,
Mbunge jimbo ni letu, usije ukaturusha!
6.
Hapo ndipo pa kuanzia, kisha tufike mwishoni,
Tulikupa twachukua, wangung'unika nini ?
Vipi utamwamkua,asiye mwako machoni ?
Mbunge jimbo ni letu, usije ukaturusha!
7.
Wananchi watachukua, kilicho mwako mkononi,
Na hili sintowaambia, sioni lina walakini,
Kichochoro 'kitumia, kumejaa barabarani,
Mbunge jimbo ni letu, usije ukaturusha!
8.
Mvuvi anapovua, samaki huwa kapuni,
Wewe umeshakwapua, vyako viko makwapani,
Usiotee kurejea, hiyo ndoto ya mbeleni,
Mbunge jimbo ni letu, usije ukaturusha!
9.
Wazee mmeshupaa, mmetufanyia nini,
Magenge mmeyazua,kung'atuka mwahaini,
Juu tutawasanzua,vijana fursa wapeni,
Mbunge jimbo ni letu, usije ukaturusha!
10.
Wanawake wameamua, kazi kuja waonyesheni,
Haraka pisheni njia, midume msio makini,
Nchi twataka komboa, umalizike uzaini,
Mbunge jimbo ni letu, usije ukaturusha!
11.
Vijana wameamua, kuingia madarakani,
Filamu kutuchezea, si ile ya umaskini,
Ya kuukata kwa sanaa, tushangaze duniani,
Mbunge jimbo ni letu, usije ukaturusha!

Mkuu wa wilaya mambo ?

1.
Wilaya inaugua, hili ndugu walijua,
Tabibu anatakiwa, wilaya kupata dawa,
Wote mnajifungia, ofisini mnasinzia,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
2.
Maendeleo vitendo, lazima kuyapangia,
Mengine wekeni kando, kwanza muonyeshe njia,
Hayo mawazo ya mgando, zamani tumeshakataa,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
3.
Wilaya ina ardhi, tupange cha kuzalisha,
Na jinsi ya kuhifadhi, tija tukaizungusha,
Wilaya ipande hadhi, na kujitofautisha,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
4.
Wilaya ina madini, vipi lije tumaini,
Utoke umaskini, watu kukosa thamani,
Tuipate afuteni, vijijini na mjini,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
5.
Wilaya ina maziwa, vipi tuyapate maji,
Ili yaweze kutumiwa, na kuwa ni wetu mtaji,
Mashamba kunyeshea, tukafanya uvunaji,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
6.
Wilaya ina mifugo, tuwafuge namna gani,
Wasiwe kwetu mzigo, bali amana makini,
Na sisi tuwe vigogo, Mbeya na umasaini,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
7.
Wilaya ina asali, vipi mbaya yetu hali,
Tunazo na pilipili, mbona maisha shubili,
Twala na kusaza wali, ila hatuna afadhali,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
8.
Nini chanzo cha tatizo, lazima tupate jua,
Utafiti mzomzo, lazima kujifanyia,
Tupate maelekezo, njia ipi kutumia,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
9.
Wengi wasema nchini, sisi mbona matajiri,
Hatunao tu umakini, ndio twawa mafakiri,
Ili tuwe sio duni, tuianze mpya ari,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
10.
Wilaya sio ngomani, wilaya ni kampuni,
Meneja watafuteni, miradi waje baini,
Mipango nayo wabuni, kwa mkubwa umakini,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
11.
Wialay ni kampuni, viranja badilikeni,
Urari uwe juani,wala sio mafichoni,
Nini wilaya thamani, na wapi mlipo duni,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
12.
Amali zenu jueni, hizo ni hisa yakini,
Watu waelimisheni, kwa KIswahili laini,
Wasoenda darasani, nao pia watamani,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
13.
Ukuu sio masuti, wala fashioni mpya,
Huo ni uzumbukuti, mafiga hayana chafya,
Wananchi ndio yakuti, wataka moyo kulea,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?
14.
Ukubwa sio ofisi, fenicha nalo gari,
Ukuu si kutanafusi, wala njaa ya fahari,
Uongozi uasisi, heri ya wote si shari,
Mkuu wa wilaya mambo, au yote kwako sawa ?

Mkuu wa mkoa vipi ?

1.
Kiongozi kazi yake, kutatua matatizo,
Ukijenga uezeke, tena utumie nguzo,
Madaraka usishike, kama fikra hamnazo,
Mkuu wa mkoa vipi, au huoni tatizo?
2.
Au huoni tatizo, wakati yakuzunguka,
Ofisi ni kipoozo, toka nje kugutuka,
Teremka ngazi hizo, hadi chini ukafika,
Mkuu wa mkoa vipi, au huoni tatizo?
3.
Wewe Waziri mkuu, mkoa yako milki,
Acha tu ya kunukuu, ingia katika mikiki,
Silaha yako mguu, kwalo haudanganyiki,
Mkuu wa mkoa vipi, au huoni tatizo?
4.
Wewe mkubwa gavana, milioni wako chini,
Hili na lile hawana, wakungoja mitaani,
Hatua iwe amana, njoo nawe mstarini,
Mkuu wa mkoa vipi, au huoni tatizo?
5.
Mkuu onyesha njia, watu wataifuata,
Ikiwa wanapotea, basi wewe ni matata,
Panga kisha kupangua, hatuutaki ukata,
Mkuu wa mkoa vipi, au huoni tatizo?
6.
Jamii iwe na nyumba, wameyachoka manyatta,
Pambanueni vihamba,watu wapate karata,
Siasa zile za kuimba,hazina wa kufuata,
Mkuu wa mkoa vipi, au huoni tatizo?
7.
Barabara kazi yako, zijengwe ima fa ima,
Juu wako nyuma yako, wewe sema waja hima,
Wala msikae kitako, hadi iishe zahama,
Mkuu wa mkoa vipi, au huoni tatizo?
8.
Miradi anzisheni, kama vile kampuni,
Watu wajumuisheni, hisa ziwe maishani,
Na pasiwe na utani, lazima mle yamini,
Mkuu wa mkoa vipi, au huoni tatizo?
9.
Miundombinu anzeni, juu nao wamalize,
Kusubiriana acheni, wenyewe sasa mjikaze,
China kajifunzeni, wanavyofanya seuze,
Mkuu wa mkoa vipi, au huoni tatizo?
10.
Juzi wamejenga treni, iendayo sana kasi,
Wameiga kwa Wajapani, ufundi pia asasi,
Kama vile ni utani, safari zao fususi,
Mkuu wa mkoa vipi, au huoni tatizo?
11.
Nendeni India muone, watengeza kila kitu,
Ni mikoa ya wajane, walakini watukutu,
Wanakua mara nane, sisi kwao hatufutu,
Mkuu wa mkoa vipi, au huoni tatizo?
12.
Paeni nako Brazili, mashine wakokotoa,
Kila kitu ni sahili, wazalisha kwa mamia,
Hawanao ujahili, milango wamefungua,
Mkuu wa mkoa vipi, au huoni tatizo?

Mashairi yanasema

1.
Mashairi yanasema, mengi yanatuambia,
Kwa watu wenye hekima, kauli huzizingatia,
Na palipo waadhama, waidha huzingatia,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
2.
Yashangaza hizi zama, kuipuuza sanaa,
Zunguka nchi nzima, ushairi unapwaya,
Nai zinazorindima, adili zadidimia,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
3.
Shuleni wameshakwama, nani kutunga ajua,
Afundishaye ni ndama, ng'ombe wameshapotea,
Kukamua wamekwama, upepo wawapepea,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
4.
Redioni wamehama, watunzi waliokua,
Sasa zimebaki ngoma, na makelele kufua,
Halfani hana hema, baridi augulia,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
5.
Andanenga kasimama, gumzoni kaingia,
Utunzi kaona noma, maslahi yasinyaa,
Wala hapana heshima, wala wa kutuangalia,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
6.
Ninatweta, ninahema, hili sikulitegemea,
Nchi yenye takrima, utunzi isiyowafaa,
Watu wafunga kalima, busara kuyoyomea?
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
7.
Kitu gani anasema, Shaaban alipokua,
Mnyampala muadhama, hili hakulifikiria,
Shehe Abedi daima, asingelitegemea,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
8.
Mochiwa kabaki nyuma, hadi anajiondokea,
Mla mbovu kainama, hili hakulisikia,
Abdulatifu kahama, Uingereza kaselea,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
9.
Kiswahili kitazama, bila utunzi kukua,
Wasiokitakia mema, hawataki kukitumia,
Vyuoni wanakilima, eti sio maridhia,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
10.
Elimu imesimama, tena yazidi sinyaa,
Kiswahili kukinyima, ruksa kufundishia,
Ni kweli mkataa pema, panakomwita pabaya,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
11.
Mitume wametuhama, lugha yetu kuiua,
Tambiko zimegangama, hakuna wa kutusikia,
Na midomo imeachama, twadhani twaomba dua,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
12.
Mushawari kagoma, uzuri umepotea,
Sasa twaicheza ngoma, asili tusioijua,
Akili zimetuhama, tumebaki kubabia,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
13.
Mashairi yanasema, viziwi watasikia,
Makilla akilalama, wengi watamsaidia,
Ni tamu lugha ya mama, utumwa nyingine kua,
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!
14.
Semeni mliosoma, Mlokozi chokonoa,
Kahigi tia kalima,na vijana mlioingia,
Nchi yataka neema, ije vipi bila lugha?
Mashairi yanasema, asosikia kiziwi!