Friday, December 16, 2011

Tujisafisheni ndani

Akilini haijakaa, utalii kutokua,
Kila nikifikiria, papo tulipokosea,
Laiti ningelijua, mimi ningegharamia,
Tujisafisheni ndani, utalii utawanda!

Bandari na kupokea, bora kama zingekua,
Na viwanja vya kung'aa, kama Dubai vikawa,
Mamia wangelitua, na ajira kunyanyua,
Tujisafisheni ndani, utalii utawanda!

Mandhari na maua, nchini zingetulia,
Ikawa ni lewalewa, kwa kila anayekaa,
Kwalo wangetusifia, wengine wakaingia,
Tujisafisheni ndani, utalii utawanda!

Nchi ikiwa kinyaa, mtalii hatotua,
Na kama akijatua, haji tena kurejea,
Mbali ataishilia, na wengine kuwang'oa,
Tujisafisheni ndani, utalii utawanda!

Nchi ikijisifia, maskini imekua,
Watu huinyanyapaa, kwingine kukimbilia,
Unanuka nakwambia, ufukara ni balaa,
Tujisafisheni ndani, utalii utawanda!

Lazima kuuondoa, ufakiri Tanzania,
Heshima kujipatia, wengine kutotukataa,
Ndipo tutatembelewa, wenda na yote dunia,
Tujisafisheni ndani, utalii utawanda!

Maji kuyagharamia, mahotelini kujaa,
Mabwawa kuogelea, bure yasijekukaa,
Starehe ni murua, watalii kwao dawa,
Tujisafisheni ndani, utalii utawanda!

Uchafu kutofungulia, choo njiani kikawa,
Na wasiozingatia, si viongozi wa kufaa,
Kazi mbali futilia,na wengine kuchagua,
Tujisafisheni ndani, utalii utawanda!

Barabara bora kua, salama kujisikia,
Watalii kushangaa, kila wanapotembela,
Njiani wasipojikwaa, na kukutwa na balaa,
Tujisafisheni ndani, utalii utawanda!

Pikipiki zahofiwa, njiani zilizojaa,
Humo zinamopitia, daladala kufwatia,
Watu wanamopitia,pasi kushughulikiwa,
Tujisafisheni ndani, utalii utawanda!

Njiani zafa sheria, kwao wanaotembea,
Zinalindwa motokaa, rushwa zinazochangia,
Watalii huambaa, nchi hivyo ikishakua,
Tujisafisheni ndani, utalii utawanda!

Bei kuziangalia, ovyo tunazopangia,
Wengi huwashtua, kwingineko kuhamia,
Itakuwa ni ruia, milioni kufikia,
Tujisafisheni ndani, utalii utawanda!

Uchumi kuunyanyua, vibaka wakapungua,
Zamani kuirudia, Zanzibar ilivyokua,
Vitu walirudishiwa, kila vilipopotea,
Tujisafisheni ndani, utalii utawanda!

Jamii ikichangia, na mapato kupatia,
Nao wakajisikia, ubia wameingia,
Utalii utakua, na nchi kuendelea,
Tujisafisheni ndani, utalii utawanda!

No comments: