Thursday, December 22, 2011

Kuchochea

Uchochezi siujui, leo nataka kujua,
Hao wanaoudai, uchimvi ninawajua,
Ni waanzisha jinai, uovu ukifichua,
Kumwamsha mlalahoi, uchokozi inshakua?

Ni wakubwa wasanii, wanaotushtakia,
Na mfano wangu hai, ni rada tulipofichua,
Viongozi wakadai, watu tunawachochea,
Kumwamsha mlalahoi, uchokozi inshakua?

Wanasheria narai, hili kushughulikia,
Sheria aina hii, wakati zimepitua,
Wakoloni wafurahi,wajinga tulivyokua,
Kumwamsha mlalahoi, uchokozi inshakua?

Sheria tulizotii, yeye alipoingia,
Twaendelea kusihi, huru sasa tumekua,
Kweli anatukinai, uhuru hatujaujua,
Kumwamsha mlalahoi, uchokozi inshakua?

Watu wakiwa nishai, bahau na wasojua,
Nchi hawaiinui, na matatizo hukua,
Na raia hawakui, mawazo wakapanua,
Kumwamsha mlalahoi, uchokozi inshakua?

Mjinga ukimraia, vipi mambo wachochea,
Sheria siielewi, naona yanizingua,
Unafiki haifai, ni bora kuiondoa,
Kumwamsha mlalahoi, uchokozi inshakua?

Ikiwa mtu hajui, kosa kweli kumwambia?
Huyu kuvaa adai, kumbe uchi atembea,
Hivi si kumstahi, ukweli ukimwambia?
Kumwamsha mlalahoi, uchokozi inshakua?

Shetani atusanii, yake tunavyotetea,
Wengine wanazirai, ushetani kuingia,
Nchi yakosa uhai, mauti yakimbilia,
Kumwamsha mlalahoi, uchokozi inshakua?

Wanafiki ni adui, nchi kuwavumilia,
Wanaishi kwa jinai, ukubwa wakitumia,
Katiba iliyo hai, hili utalizuia,
Kumwamsha mlalahoi, uchokozi inshakua?

No comments: