Wednesday, December 14, 2011

Msiache zima taa

UTU mlishaondoa, mwabaki kufakamia,
Mali kulimbikizia, ahera msivyochukua,
Nafusi zimepumbaa,baradhuli zimekua,
Msiache zima taa, nd'o yenu teknolojia!

Kongoza waloachiwa, kazi yao kubomoa,
Na waliotegemewa, ndio wanaotegemea,
Kwacho kilichotembea, sasa kinachechemea,
Umeme wa katakata, hivi sasa ni mradi!

Wajifanzao kujua, uhuuna yule ahua,
Maovu mkijaliwa, wema njiani wajaa,
Ya ovyo mkijaliwa, mazuri yawavizia,
Msiache zima taa, nd'o yenu teknolojia!

Na dubu kukuchekea, hilo halijatokea,
Ruksa waliotoa, wakweza wamendoa,
Kichuguu chatitia, kwa leo hakitatufaa,
Umeme wa washawasha, bongo ilipoishia!

Ucheshi walokua, moyoni wajaa ubaya,
Ndio ya kwetu dunia, na haya tunayajua,
Na kila tunavyozaa, ndivyo yanavyozidia,
Msiache zima taa, nd'o yenu teknolojia!

Ni mradi umekua, hofu teknolojia,
Wajuaji wasojua, mkenge wanaingia,
Magunia kujivunia, wajinga waliokua,
Umeme wa washawasha, bongo ilipoishia!

Kamba ninawaachia, Ulaya naelekea,
Ubalozi nimepewa, kwenda kuwatengezea,
Na kisha nikirejea, juu nitawanyanyua,
Msiache zima taa, nd'o yenu teknolojia!

Msiwashe mishumaa, mkaja kushangilia,
Habari sijaambiwa,nilikuwa naotea,
Ila sintoshangaa, haya kuja kutokea,
Umeme wa katakata, hivi sasa ni mradi!

Wajinga wakikuvaa, mjanja hatasogea,
Hekima usipojua, busara hutotumia,
Uongozi ni ukiwa, ujuayo hujajua,
Msiache zima taa, nd'o yenu teknolojia!

Kiburi kubwa hadaa, mitume walingania,
Unyenyekevu ni dua, watawa wanaijua,
Kwalo nitasujudia, Kwa Muumba alokua,
Umeme wa washawasha, bongo ilipoishia!

Ibada sijakataa, maishani kwangu taa,
Bila kuing'ang'ania, leo nisingebakia,
Na sijui yangu njia, wapi inakoendea,
Msiache zima taa, nd'o yenu teknolojia!

Nitazidi kutumia, kwa dakika na masaa,
Kwa siku kutimia, pia majuma kadhaa,
Na miezi kuishia, miaka hadi ikawa,
Msiache zima taa, nd'o yenu teknolojia!

Bila mifumo kuzaa, hapahapa twabakia,
Ndoto tutajiotea, ila hatutaendelea,
Tutazidi didimia, na watu kununuliwa,
Umeme wa katakata, hivi sasa ni mradi!

Na tusipojiandaa, itarudi mishumaa,
Uranium kuibiwa, wengine kwenda wauaa,
Nasi haitatufaa, ikitufaa balaa,
Msiache zima taa, nd'o yenu teknolojia!

Watakuja na kwishia, mambo kubabaishia,
Ndio walivyozaliwa, kubadilika nazaa,
Nchi pengo ingekua, wakweli tungelikuwa,
Umeme wa washawasha, bongo ilipoishia!

Azim naitikia, wito nimeupokea,
Nimejaribu nokoa, fikra kuzitanzua,
Kwao wanaogundua, waweze kuzitumia,
Msiache zima taa, nd'o yenu teknolojia!

No comments: