Mtendwa akifanziwa, nukta ataitia,
Alama ikajang'aa, kesho ikashuhudiwa,
Wajue wasiojua, na ya haki kuamua,
Mtendwa akitendewa, mwisho huacha puuza!
Uoga humpotea, ukajaa ushujaa,
Haki kusimamia, waongo kuwaumbua,
Kila mtu akajua, ni wapi pakusimamia,
Mtendwa akitendewa, mwisho huacha uoga!
Hudharau yalokua, madogo yakitukia,
Husepa akaelea, na kazi kuendelea,
Ila yanapomzidia, pumzi huzinyanyua
Mtendwa akitendewa, mwisho huacha puuza!
Na akishakugundua, mtenda anatendewa,
Kupuuza hupwaliwa, hasira zikamjaa,
Mikono akinyanyua, ataibeba dunia,
Mtendwa akitendewa, mwisho huacha uoga!
Si mtu wa kuchezewa, mtendwa aking'amua,
Huruka juu ya paa, shetani akambinua,
Na angani kutembea, hadi akamkomalia,
Mtendwa akitendewa, mwisho huacha puuza!
Hata chini huchimbua, ardhini kuingia,
Mambo akayapindua, juu chini yote kuwa,
Na kisha kuchanganua, la ukweli akajua,
Mtenda akitendewa, mwisho huacha uoga!
Hakuna chakubakia, siku inapowadia,
Mwenye kucheka hulia, mdogo mkubwa kua,
Wanaovaa huvua, waimbao kunyamaa,
Mtenda akitendewa, mwisho huacha puuza!
Manyunyu hunyunyukia, na nyuki wakaugua,
Mzinga huzinguliwa, akatekwa malkia,
Miliki huja sambaa, shaghalabaghala kua,
Mtenda akitendewa, mwisho huacha uoga!
Wednesday, December 14, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment