VITABU twashikilia, na dua tunazitoa,
Nchi ipate jaliwa, kuepuka mabalaa,
Miongoni kumtia, tunayemuangukia,
Mungu awe kati yetu, wenye dini, waso dini!
Ya kwao waliyotia, wenyewe kujifikiria,
Na ya kwetu kuambaa, mithili tusiokua,
Haki akasimamia, na hukumu kuitoa,
Mungu awe kati yetu,wenye yao, wenye yetu!
Maneno wanaoua, na mwili roho kutoa,
Ili kujitimizia, waliyokwishaazimia,
Na watetezi raia, bure wanaojitolea,
Mungu awe kati yetu, wauaji, watetezi!
Na wale tunaoliwa, Wahab kusimamia,
Chetu akatupimia, na chao kuwagawiwa,
Walao kuambulia, kile kinachowafaa,
Mungu awe kati yetu, walao na waliwao!
Nchi waliochukua, ukubwa wakajipea,
Na tuliodhulumiwa, tukaonekana kinyaa,
Yabidi kutuagua, na dawa kutupatia,
Mungu awe kati yetu, wenye nchi, waso nchi!
Walalahoi twalia, walalahai ni baa,
Hukumu twakuachia, wewe ndiye unayejua,
Sisi tutaingojea, hadi utakapoamua,
Mungu awe wetu, walalahoi, walalahai
Nchi wanaosimamia, na umaskini kujaa,
Matumbo wanaovimbiwa, hali sisi tuna njaa,
Afu twakugeukia, huruma twategemea,
Mungu awe kati yetu, wamanchi na viongozi.
Neema wasiopewa, na hao wanaopewa,
Miongoni kwetu jaa, nafsi kuangazia,
Pengine tutakujajijua, na utu kuutambua,
Mungu awe kati yetu, wanyimwa na wapewao.
Pagani waliokua, Mungu wasiokujua,
Haki na usawa pia, miongoni kwetu kua,
Utukufu walopewa, sisi utumwa twatwaa,
Mungu awe kati yetu, wachaMungu na pagani.
Mungu awe kati yetu, wasafi na wahaini.
Waongo tunaoambiwa, pembeni tumeshakaa,
Hukumu twakuachia, haki unayetengenea,
Subira tunailea, kungoja ya kutokea,
Mungu awe kati yetu, wakweli nao waongo.
Wale wanaotumiwa, na wageni kuwafaa,
Waliokwishakununuliwa, wakageuka bidhaa,
Na sisi tulobakia, njiani tunazubaa,
Mungu awe kati yetu, wazawa na mamluki.
Nchi tunaoililia, na amani kuhofia,
Chama wanaopepea, na nafusi kukomaa,
Hukumu twaingojea, kusiche bila kutoa,
Mungu awe kati yetu, wenye nchi, wenye chama !
Udini wanaozushiwa, na miradi ilokua,
Wapepeao vitambaa, vya uzaini na hadaa,
Na wanaojisifia, na tunaojikosoa,
Mungu awe kati yetu, wasio na wenye udini.
Na wanaotuibia, nchi kufanya bidhaa,
Hali wasiotujua, twazidi kudidimia,
Kwa haya wanaopwaya, aibu wasiojua,
Mungu awe kati yetu, wezi na waaminifu.
Akili waliopewa, na sisi tusiojaliwa,
Ujinga tuliogaiwa, na maradhi kulaniwa,
Maafa tuliopangiwa, na fedheha kutujaa,
Mungu awe kati yetu, matabaka Tanzania!!!
Masikini tulokuwa, na neema kukatiwa,
Mashaka tuliopewa, mikosi na kila baa,
Yetu tumeshayajua, je, yao wanatambua?
Mungu awe kati yetu, matabaka Tanzania!!!
© 2011 Sammy Makilla
Friday, December 16, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment