Friday, December 16, 2011

Huwarusha mamlaka

Lazima kuwaondoa viongozi wasofaa,
Ila kazi kuwatoa, kwa wanavyong'ang'ania,
Na sheria watumia, halali zisizokua,
Huwarusha mamlaka, watu wao serikali.


Ujibari wajitia, mno tumewaachia,
Mimi kweli nashangaa, tajiri na muajiriwa,
Ang'aka muajiriwa, tajiri kumtimua,
Huwarusha mamlaka, watu wao serikali.


Kinyume ingelikuwa, kufukuzwa mwajiriwa,
Kazi akiitibua, wengine wakachukua,
Afrika yazubaa, wazidi kutuonea,
Huwarusha mamlaka, watu wao serikali.

Wananchi hawajajua, nguvu waliyojaliwa,
Wabaya wavumilia, na wezi waliokua,
Dhima wanaotumia, kwa ya kwao manufaa,
Huwarusha mamlaka, watu wao serikali.

Katiba kuifumua, vipengele vikajaa,
Hili kusimulia, jinsi ya kuwaongoa,
Viongozi wasiofaa, hata wakichaguliwa,
Huwarusha mamlaka, watu wao serikali.

Amgaza wamasheria, katiba kujatufaa,
Sio tena kuchezewa, na kazi wasiojua,
Muda kutupotezea, hatukuja kutembea,
Huwarusha mamlaka, watu wao serikali.

Mamlaka kuchukua, madaraka kuachia,
Na mifumo ya kufaa, viongozi kukataa,
Huu wakati radhia, tusije kuuachia,
Huwarusha mamlaka, watu wao serikali.

Allah twakusujudia, Maliki uliyekua,
Uiongozayo dunia, iongoze Tanzania,
Viongozi kutufaa, watakaotunyanyua,
Huwarusha mamlaka, watu wao serikali.

© 2011 Sammy Makilla

No comments: