Bado mnapewa shanga, nanyi mnazikubali,
Mnahongwa pia kanga, mnaona nazo mali?
Hakika nyinyi wajinga, kubali msikubali,
Bado unapewa shanga, almasi mwaitoa?
Wakoloni waliganga, weupe wenye kandili,
Na nyimbo zao kutunga, ukawaona rijali,
Hata na yao kuringa, mwishowe ulikubali,
Bado unapewa shanga, almasi mwaitoa?
Mweusi anakufunga, na shari kuikabili,
Ataka wake ushanga, hivi leo ukubali,
Akataa kumpinga, umpe na zako mali,
Bado unapewa shanga, almasi mwaitoa?
Uongo atautunga, uonekane jahili,
Na hao wake wajinga, wakudhihaki kwa hali,
Na kamasi kukupenga, kama vile baradhuli,
Bado unapewa shanga, almasi mwaitoa?
Kawahadaa mganga, sisi hatuna akili,
Wazidi njama kupanga, kwa kutuona dhalili,
Na mifupa watapanga, wajenge zao akili,
Bado unapewa shanga, almasi mwaitoa?
Watatuuzia shanga, nazo pia kandambili,
Wao wakakate anga, yetu ni ardhilhali,
Tunajua kupuyanga, kuwa wao madalali,
Bado unapewa shanga, almasi mwaitoa?
Kwa vitenge pia khanga, hereni na mihimili,
Fulana zenye upanga, na rangi ziso rijali,
Yote watabananga, pasiwe na mushkeli,
Bado unapewa shanga, almasi mwaitoa?
Kificho watacharanga, ukweli wakkubali,
Kazi hii kujivunga, ndio wake uhalali,
Mti wake ni mgunga, shoka kazi hakubali,
Bado unapewa shanga, almasi mwaitoa?
Mioyoni wanavyokonga, malaika tajamali,
Kumbe ni makarandinga, mizigo yote kuhimili,
Ahadi zao mizinga, radi haitaikabili,
Bado unapewa shanga, almasi mwaitoa?
Wednesday, December 14, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment