Wednesday, December 14, 2011

Watuibiao

Kizazi na kiwe tasa, dhahabu watuibiao,
Wasiipate fursa, ila kwa watuambao,
Tukawapa yetu ruksa, vijijini tukaao
Watuibiao dhahabu, kizazi kiwe ni tasa!

Umetupata mkasa, sisi huku tukaao,
Kisha wapewa anasa, mijini hao wakaao,
Machozi yakibubusa, ni wengi tuyatoayo,
Watuibiao dhahabu, kizazi kiwe ni tasa!

Maisha yetu mkasa, wanaofaidi wao,
Nyusi twashindwa pepesa, ujanja watumiao,
Viongozi wamenasa, kujitoa kazi kwao,
Watuibiao dhahabu, kizazi kiwe ni tasa!

Linawashinda darasa, ubabe ni kazi yao,
Wataishindwa anasa, kwa mengi waulizwayo,
Na majibu wakikosa, iwe ni hamaki kwao,
Watuibiao dhahabu, kizazi kiwe ni tasa!

Wanaziua fursa, za yetu maendeleo,
Haki yao ni utasa, kwao nao wake zao,
Na wakipata makasa, wasiwe na marejeo,
Watuibiao dhahabu, kizazi kiwe ni tasa!

Heri hawakuinusa, zimekufa pua zao,
Waachie yenye hisa, za moto ububujikao,
Kesho iwe kisa na mkasa, mbele ya Muumba wao,
Watuibiao dhahabu, kizazi kiwe ni tasa!

No comments: