Hujuaje mwenye njaa, mlaji akivimbiwa,
Nani kukusaidia, wao wajisaidia,
Mlaji hatokunyanyua, ataka wake wale pia,
Mlaji akishakula, hujuaje mwenye ndaa ?
Waongoza wenye njaa, kula mnategemea?
Matumbo yamewajaa, hewa tupu kumbe yawa?
Mioyo ganzi yeshakua, huruma watasikiya?
Mlaji akishakula, hujuaje mwenye ndaa ?
Hawa wajilimbikia, nini watawaachia,
Kazi yao kuopoa, mwadhani ni wa kuvua,
Nyavu kujawapatia, hiyo kweli ruiya,
Mlaji akishakula, hujuaje mwenye ndaa ?
Nchi itaendelea, bila mtu kuendelea,
Hii ni kubwa sanaa, mwanzo wake sijajua,
Lakini inapoishia, tayari ninapajua,
Mlaji akishakula, hujuaje mwenye ndaa ?
Ustawi motokaa, na njia zinafatia,
Sijapata kusikia, ila sasa naambiwa,
Kwa mguu natembea, najua nitapofikia,
Mlaji akishakula, hujuaje mwenye ndaa ?
Nyumba wanazikataa, si msingi wa kufaa,
Fedha wanajirushia, vigumu chini kutua,
Kile kisichotufaa, kwao dili imekua,
Mlaji akishakula, hujuaje mwenye ndaa ?
Kazi watuimbia, maneno usiokua,
Ala hazijatimia, burudani yazubaa,
Na kula anayejua, huhofu kuzinguliwa,
Mlaji akishakula, hujuaje mwenye ndaa ?
Fumbo wawafumbia, wajanja wasiokua,
Mjinga aking'anua, ataondoa udhia,
Na juu kinachokua, lazima chini kutua,
Mlaji akishakula, hujuaje mwenye ndaa ?
© 2011 Sammy Makilla
Friday, December 16, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment