Friday, December 16, 2011

Ni kitanda chenye dhiki

Kitanda chenye hasira, hasidi na roho mbaya,
Kinafaa kukigura, hakiwezi tengeneya,
Kiumbe akiwa sira, kukuuma hutokea,
Ni kitanda chenye dhiki, usingizi hutopata.

Lalo bila maghufira, malaika husanzua,
Na bwana aliye bora, kusamehe atwambia,
Hili tukiwa majura, nini tunakitegemea?
Ni kitanda chenye dhiki, usingizi hutopata.

Kitanda kilicho ghera, usingizi hukataa,
Nafsi wanaofura, hata nyoka hukimbia,
Heri kulala na chura, nyimbo mbaya kukwimbia,
Ni kitanda chenye dhiki, usingizi hutopata.

Ulevi kama chakara, kitanda chote hupwaya,
Hufanyika masihara, hapana la kufurahia,
Kisirani huzurura, hadi kesho kuingia,
Ni kitanda chenye dhiki, usingizi hutopata.

© 2011 Sammy Makilla

No comments: