Wednesday, December 14, 2011

Dhahabu kuifasiki

Madini kuyafasiki, lazima chini kumea,
Eneo waliomiliki, ni budi kuwanyanyua,
Leo haifahamiki, hao inaowanyanyua?
Dhahabu kuifasiki, laana mnailea!

Kawajalia milki, muumba aliyekua,
Hugeuka unafiki, mahala kupachukua,
Halafu iwe mikiki, fidia kuja kutoa,
Dhahabu kuifasiki, laana mnailea!

Wanavijiji kindaki, kuamka mwatakiwa,
Madini yenu milki, ni lazima kuwafaa,
Wenzenu Peru waafiki, na hili wapigania,
Dhahabu kuifasiki, laana mnailea!

Harakati washiriki, Aregentina nao pia,
Madini kuyamiliki, na salama kuchimbua,
Hawaitaki hilaki, na visa kujafanyiwa,
Dhahabu kuifasiki, laana mnailea!

Magharibi, mashariki, wanaweza kuchimbua,
Tutafute marafiki,tunaowaaminia,
Hatutaki wanafiki, kibao kutugeuzia,
Dhahabu kuifasiki, laana mnailea!

Katuruzuku Khalaki, ndiye atakayeamua,
Kukomeha ufasiki, madini kutunyanyua,
Mitambo wanaomiliki, rushwa japo wametoa,
Dhahabu kuifasiki, laana mnailea!

No comments: