Kazi hii sijataka, akili ni mazoea,
Ukwasi ningelishika, mengine ningejifnyia,
Na haya kupumzika, nikaabiri dunia,
Nitaacha nikilipwa, niwaachie wengine.
Kazi ninayoitaka, ibada na nyingi dua,
Dini nikatakasika, kwa undani kuijua,
Haya kutoshawishika,wenzangu kuwaachia,
Nitaacha nikilipwa, niwaachie wengine.
Hili ninalo hakika, kung'atuka nawania,
Mtaji nikishaushika, shamba naenda hamia,
Wakiwa nikawashika, na macho kuwafungua
Nitaacha nikilipwa, niwaachie wengine.
Majirani nawataka, kiuchumi kuwafaa,
Mengi yameshapangika, kutenda nakusudia,
Na hao wakiibuka, jina watanijengea,
Nitaacha nikilipwa, niwaachie wengine.
Kilimo ninakitaka, ufugaji nao pia,
Msingi nikishaweka, shule nitaifungua,
Kizazi kukiezeka, imara kuwa lake paa,
Nitaacha nikilipwa, niwaachie wengine.
Msaada nautaka, ya kwenu kuwaachia,
Moyo wangu kusumbuka, umekwishajichokea,
Nautoroka wahaka, shamba kwenda jikalia,
Nitaacha nikilipwa, niwaachie wengine.
© 2011 Sammy Makilla
Friday, December 16, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment