Sunday, January 1, 2012

Wazee wa Kitaifa, wakowapi Tanzania?

Nchi wazee yataka, mambo yao kufanzika,
Yajepungua mashaka, nao mkubwa wahaka,
Na waliodhulumika, dhahiri kuja fichuka,
Wazee wa Kitaifa, wakowapi Tanzania?

Wazee waliochoka, wananchi kugawanyika,
Na vitu kutofanyika, nchi ikafaidika,
Pasiwe la kueleweka, huku yaenda miaka,
Wazee wa Kitaifa, wakowapi Tanzania?

Wazee wenye hulka, ya uhuru kuutaka,
Na watu wasiotumika, kwa kilemba cha ukoka,
Ila ya kwao kuyashika, na nchi kuneemeka,
Wazee wa Kitaifa, wakowapi Tanzania?

Wazee wasiotaka, uchama wenye mashaka,
Uzalendo kuuweka, nchi ikaimarika,
Na ajenda kuzisuka, serikali kuwajibika,
Wazee wa Kitaifa, wakowapi Tanzania?

Maadili kuyasaka, ya uongozi kushika,
Shinikizo kufanyika, hadi chombo kukiweka,
Nchi ikatawalika, wananchi wanavyotaka,
Wazee wa Kitaifa, wakowapi Tanzania?


© 2011 Sammy Makilla

No comments: