Thursday, January 12, 2012

Obama bado afaa

Ni nani kama Obama, Marekani kuokoa,
Uchumi wanza simama, kwapungua kulegea,
Kwa yake kubwa hekima, maajabu yatokea,
Obama bado afaa, wengine wajizuzua!



Nchi imeishamtuma, matunda wanangojea,
Tumuombeeni mema, aweze kufanikiwa,
Kile atakachokichuma, chaweza kutusaidia,
Obama bado afaa, wengine wajizuzua!

Mipaka imemzima, kwingi amefifia,
Sio yake madaraka, nini atajifanyia,
Ila wenye la hakika, bado wamtumainia,
Obama bado afaa, wengine wajizuzua!

Afata zake kalima, anaitafuta dawa,
Aweze kutibu homa, isumbuayo dunia,
Ona anavyojituma, ushindi hatochukua?
Obama bado afaa, wengine wajizuzua!

Wanafiki wazizima, matajiri walokua,
Vyao wameshavichuma, vya wengine wanadakia,
Wamiliki wenye njama, dunia wanaohadaa,
Obama bado afaa, wengine wajizuzua!

Imeshaisha kasama, waliyoikusudiwa,
Sasa kwao iwe noma, shimoni wanaingia,
Wanatafuta zahama, na mali kuwapotea,
Obama bado afaa, wengine wajizuzua!

Upande wanaoegema, kuti bovu wakalia,
Kuanguka ni lazima, chini wakaja kutua,
Wakaikosa heshima, waliyokwishaizowea,
Obama bado afaa, wengine wajizuzua!

Kwa hadhi na taadhima, heri ninakutakia,
Rais tena Obama, uweze ukajaliwa,
Dunia ipate hema, kwa muda tukatulia,
Obama bado afaa, wengine wajizuzua!

No comments: