Friday, January 13, 2012

Ahadi za mja kunena

Mja ahadi hutoa, na hatendi akinena,
Kuropoka majaliwa, hathamini uungwana,
Ahadi anazotoa, ajua uwezo hana,
Ahadi za mja kunena, muungwana ni vitendo!

Imani huitania, na amri ya Rabana,
Fukara kuwahadaa, na tamaa kuwabana,
Yao yakkshakujaa, ya wengine ni utwana,
Ahadi za mja kunena, muungwana ni vitendo!

Juu wanaangalia, chini washindwa kuona,
Na Jalali huridhia, awangoje kwenye kona,
Hedaya kuwapatia, alizokwishazitabana,
Ahadi za mja kunena, muungwana ni vitendo!

Ahadi huikataa, ajuaye mimi sina,
Achelea kuyalea, watu watakayoguna,
Kipimo hukipimia, cha uwezo mimi sina,
Ahadi za mja kunena, muungwana ni vitendo!

Nafsi huichungua, hali inayofanana,
Ahadi inapotoa, hujua haitakana,
Aliamini ikawa, kwa watu ni muungwana,
Ahadi za mja kunena, muungwana ni vitendo!

Fuadi isochanua, vigumu kuelezana,
Utakua, nilikua, njia zetu hupishana,
Haujui, sintojua, akili zitalingana,
Ahadi za mja kunena, muungwana ni vitendo!

No comments: