Thursday, January 12, 2012

Shilingi yatuumbua

Shilingi sasa kichaa, ndugu yangu umekua,
Haya unayonambia, nashinwa kukuelewa,
Mwenyewe unakimbia, upepo wafukuzia,
Shilingi yatuumbua, ufukara yatutia!

Ovataimu zaua, na posho tulizovamia,
Tunajua kutumia, hatujui vya kwingia,
Uzalishaji nazaa, na sera zimefubaa,
Shilingi yatuumbua, ufukara yatutia!

Twaachia wanaojua, kumbe ndio wasojua,
Fikra wametengua, ubunifu kupumbaa,
Ugumba tunauzaa, nchi inadidimia,
Shilingi yatuumbua, ufukara yatutia!

Mabaraza yatakiwa, uchumi kuzungumzia,
Akili kuziibua, uzalishaji kuuzua,
Nchi ikaendelea, na shilingi kutulia,
Shilingi yatuumbua, ufukara yatutia!

Ndani wanaojifungia, ndio wazuao waa,
Mambo yakiwa kimya, makosa huja jizaa,
Watu wakahadaiwa, nafuu kutokuijua,
Shilingi yatuumbua, ufukara yatutia!

No comments: