Sunday, January 8, 2012

Yaliyopita si ndwele

LAWAMA mama wa njaa, na baba wa kuchelewa,
Yalopita yaambaa, yafaa kuyaachia,
Yafaayo kufatia, leo yanayotokea,
Yaliyopita si ndwele, tujigange kwa yajayo:
Yaliyomo si tu yao,
tuweke na yetu pia.

Na anayekutumia, huja nawe kumtumia,
Shamba alokuvunia, kuvuna humsaidia,
Mwana aliyemchukua, mjukuu utamlea,
Yaliyopita si ndwele, tujigange kwa yajayo:
Yaliyomo si tu yao,
tuweke na yetu pia.

Kelele anayelia, na huku anatumiwa,
Hawezi kukusaidia, mfukoni atatwia,
Ni vyema ukajijua, mkakati kutumia,
Yaliyopita si ndwele, tujigange kwa yajayo:
Yaliyomo si tu yao,
tuweke na yetu pia.

Tunao maharamia, kwetu wameparamia,
Ni vigumu kuwajua, na kisha kuwaondoa,
Hilo lisipotokea, daima tutaonewa,
Yaliyopita si ndwele, tujigange kwa yajayo:
Yaliyomo si tu yao,
tuweke na yetu pia.

Mipango isipokuwa, hamna pa kusimamia,
Huanguka mkatua, hata msipopajua,
Yafaa kupangilia, ni mwanzo wa kwendelea,
Yaliyopita si ndwele, tujigange kwa yajayo:
Yaliyomo si tu yao,
tuweke na yetu pia.

Udhibiti watakiwa, kupata na kutumia,
Daftari asokuwa, mali yake hupotea,
Ni mjinga hukataa, idhibati kufanziwa,
Yaliyopita si ndwele, tujigange kwa yajayo:
Yaliyomo si tu yao,
tuweke na yetu pia.

Hasidi haitofaa, ni bure utaumia,
Wivu unaotakiwa, ni kushindana kwa nia,
Makubwa kujifanyia, na mengi kujijazia,
Yaliyopita si ndwele, tujigange kwa yajayo:
Yaliyomo si tu yao,
tuweke na yetu pia.

Katika panga pangua, biashara zatakiwa,
Na ardhi nayo pia, lazima kujazilia,
Haya ukiachia, wengine wanachukua,
Yaliyopita si ndwele, tujigange kwa yajayo:
Yaliyomo si tu yao,
tuweke na yetu pia.

Midia zinatakiwa, watu kuwashtua,
Yale wanayotakiwa, wapaswe kuyatambua,
Na kamba kushikilia, juu itakayowanyanyua,
Yaliyopita si ndwele, tujigange kwa yajayo:
Yaliyomo si tu yao,
tuweke na yetu pia.

Waumini kuwaibia, wenyewe tunajiua,
Katu hatutaendelea, njiani tutaishia,
Taasisi zitavia, tuzidi kuzainiwa,
Yaliyopita si ndwele, tujigange kwa yajayo:
Yaliyomo si tu yao,
tuweke na yetu pia.

Uchamungu twatakiwa, na kesho kuyahofia,
Waumini wakiumia, sisi tutakuja lia,
Kamwe hatutaangaliwa, wala kuja hurumiwa,
Yaliyopita si ndwele, tujigange kwa yajayo:
Yaliyomo si tu yao,
tuweke na yetu pia.

Meneja wanatakiwa, vitu kuvisimamia,
Uswahili ni balaa, kaburi twajichmbia,
Ardhini kulaniwa, na motoni kuingia,
Yaliyopita si ndwele, tujigange kwa yajayo:
Yaliyomo si tu yao,
tuweke na yetu pia.

No comments: