ZIMEKWISHAPITA zama, za timu za wanachama,
Soka sasa linakwama, kucheza kama ni ngoma,
Mdundiko unagoma, hapana cha kurindima,
Vilabu vya wanachama, chakaribia kiama.
Soka sio lelemama, lataka watu wazima,
Waloshiba kwa kuchuma, na akiba yao njema,
Wanaoweza kupima, kuwekeza wakasema,
Vilabu vya wanachama, chakaribia kiama.
Wanaofanya kutuma, pasiwe na wa kugoma,
Watu wote wakahema, kila siku kujituma,
Mazembe mkiwasoma, hapa wameishaegema,
Vilabu vya wanachama, chakaribia kiama.
Bakhresa keshazisoma, nyakaati zake alama,
Mara hima kasimama, panapofaa kinoma,
Biashara atachuma, na matangazo kuvuma,
Vilabu vya wanachama, chakaribia kiama.
Huyu mtu wa hekima, kamjalia Alima,
Ufunuo keshagema, afundisha maamuma,
Hakuna kurudi nyuma, mpira sasa kuchuma,
Vilabu vya wanachama, chakaribia kiama.
Msiishi kwenye zama, zitawasumbua homa,
Ovyoovyo kutetema, kama jua limegoma,
Wakati joto lavuma, jijini Darisalama,
Vilabu vya wanachama, chakaribia kiama.
Fanyeni imafaima, kuwekeza wanachama,
Kisha meneja kutuma, kazi kwenda kuifuma,
Asiguswa kwa uzima, wala akiwa na homa,
Vilabu vya wanachama, chakaribia kiama
Mbumbumbu mnalalama, mpira sasa wasoma,
Ni kampuni adhama, waweza wekeza umma,
Umasikini kuzama, watu wakaja kuchuma,
Vilabu vya wanachama, chakaribia kiama
Mengi alishayema, wengine wakamzoma,
Akawaona wa nyuma, biashara akakoma,
Ulaya sasa yahema, wawekezaji wachuma,
Vilabu vya wanachama, chakaribia kiama
Kiogopeni kiyama, kujipanga ni lazima,
Mpira uwe kisima, uwekezaji kupema,
Nchi ipate heshima, na duniani kuvuma,
Vilabu vya wanachama, chakaribia kiama
Tuesday, January 10, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment