Thursday, January 12, 2012

Hizi ni dunia mbili

Kati yao wanawali, hili naliona kweli,
Tofauti ni thakili, kuwa nyingine kabuli,
Hii si yetu asili, na tena sio fasili,
Huwa ni dunia mbili, sura nzuri na akili.

Kaumba Mutawakali, Mushawari kwa adili,
Kayagawa ilhali, kidogo kupewa feli,
Ikisadifu jamili, huzipunguza akili,
Hizi ni dunia mbili, sura nzuri na akili!

Hii ni yangu kauli, hujabadili Muzzli,
Akajalia akili, yakini nayo jamali,
Yeye ndiye mbadili, na muweza wa akili,
Hizi ni dunia mbili, sura nzuri na akili!

Hizi ni zake dalili, utukufu ahimili,
Na wanaomkabili, humsifu kulhali,
Huwapa watu akili, wengine asifadhili,
Hizi ni dunia mbili, sura nzuri na akili!

Huwaacha baradhuli, akawajaza jamili,
Pasiwe nao mithili, kama Yusufu ahali,
Haya ni ya Murtaali, mwenye wingi wa amali,
Hizi ni dunia mbili, sura nzuri na akili!

Dua anazikubali, ikiwa kama halali,
Huinua madhalili, akazika majabali,
Na wasio na akili, akazidi wapa mali,
Hizi ni dunia mbili, sura nzuri na akili!

Ni Razaki bilkuli, wote anatufadhili,
Si Chama cha Waswahili, kubagua kiakili,
Wao wanapowajali, kwa wengine mabahili,
Hizi ni dunia mbili, sura nzuri na akili!

No comments: