Friday, January 13, 2012

Siombi kitu zaidi

MIMI ni wako Abdi, yako nayaitikia,
Nakutambua Ahadi, mmoja uliyekua,
Nami daima abadi, budi kukutumikia,
Siombi kitu zaidi, unachonikadiria !

Nkkuze niwe shahidi, siku ya kushuhudia,
Haki nikaifaidi, kwa ulimi wa murua,
Hakika iwe ni jadi, kizazi nikijaliwa,
Siombi kitu zaidi, unachonikadiria !

Nitangulize uradi, hadi siku ya ahadi,
Na nisiwe mkaidi, ikinipasa sajidi,
Na unipande mdadi, kwa jina kulihimidi,
Siombi kitu zaidi, unachonikadiria !

Nipe wepesi wa radi, katika ya tawhidi,
Nijalie niwe badi, mwepesi kutaradadi,
Bidii nayo juhudi, kwa uzuzi na kuakidi,
Siombi kitu zaidi, unachonikadiria !

Nakuhimidi Wadudi, daima si maulidi,
Na siingojei Idi, kwa tabaraki hadidi,
Waniitao gaidi, upofu iwe ahadi,
Siombi kitu zaidi, unachonikadiria !

Niwe katikati budi, ya joto na ubaridi,
Nisiombe la zaidi, ukisha kuniahidi,
Iwe ni ya kwangu sudi, kupata bila idadi,
Siombi kitu zaidi, unachonikadiria !

Nitunze umaridadi, wa nafsi zumaridi,
Uwe kiongozi Hadi, tena rafiki rashidi,
Nikuitapo Swamadi, Malaika waninadi,
Siombi kitu zaidi, unachonikadiria !

Maajidi na Wajidi, niepushe na hasadi,
Na wachawi wa miradi, njiani wanaojinadi,
Na wewe kama Wahidi, kwako niwe ni waridi,

Mitume waso idadi, ibada iwe zawadi,
Inyooshe fuadi, sala ziwe makusudi,
Na masharifu jadidi, uwape yao mihadi,
Siombi kitu zaidi, unachonikadiria !

Waislamu wazidi, shetani kumkaidi,
Uwape yao Mubidi, wapende kwako kurudi,
Iwe ni zao nakidi, mazuri kukuahidi,
Siombi kitu zaidi, unachonikadiria !

Uwape kubwa juhudi, kwa elimu na zaidi,
Na waache kuritadi, kidini kwa ufisadi,
Kuifia ikibidi, hili wapae ahidi,
Siombi kitu zaidi, unachonikadiria !

Patiliza makuwadi, dini wasiiiritadi,
Wenye majina mamedi, wasiwe wenye ugwadi,
Idi wasio idadi, dini wasiikaidi,
Siombi kitu zaidi, unachonikadiria !

No comments: