Saturday, January 28, 2012

Huijui saa yako

Laiti tungelijua, wadanganya uhakika,
Mengi tungelitambua, yanaweza badilika,
Na safari ilokuwa, huenda hatutafika,
Huijui saa yako, huenda bila kwaheri!

Ahadi hatujapewa, hakuna kuyumkinika,
Twaingia kwenye njia, ramani hatujashika,
Hatuijui hatua, wapi itatupeleka,
Huijui saa yako, huenda bila kwaheri!

Mengi tunadhamiria, yasiyo na muafaka,
Ndoto nyingi hupotea, tupewalo tukashika,
Ikabidi kutulia, na kidogo kutosheka,
Huijui saa yako, huenda bila kwaheri!

Ila wapo wasojua, ilani nayo mipaka,
Kwingine hupindukia, nafsi ikawashika,
Wakajiona wajua, lolote kwa kufanyika,
Huijui saa yako, huenda bila kwaheri!

Manani huwainua, hadi juu wakafika,
Kisha hujawaachia, wabaki wanajiweka,
Ila hawatachelewa, kuyagundua mashaka,
Huijui saa yako, huenda bila kwaheri!

Kila akiachiliwa, mtu aja kuanguka,
Hawezi kujinyanyua, wala hatanyanyulika,
Mwisho umeshafikia, ndicho kilicho hakika,
Huijui saa yako, huenda bila kwaheri!

Usiifuate dunia, kwani utadanganyika,
Yafaa kujitambua, wewe sio kadhalika,
Uhai uliopewa, majukumu unataka,
Huijui saa yako, huenda bila kwaheri!

Nilinde katika njia, ninakusihi Rabuka,
Naogopa kupotea, si wakweli washirika,
Nisiwe wa kulaniwa, nikaikosa hakika,
Huijui saa yako, huenda bila kwaheri!


Januari 28, 2012
Kibaha,
Mkoa wa Pwani

No comments: