Sunday, January 29, 2012

Mtunzi hana thamani

WENZETU wamejaliwa, nchi kuwaridhia,
Mshairi kwa sanaa, kazi muhimu kupewa,
Na ofisi kuingia, ushairi kuandaa,
Hathaminiwi mtunzi, hapa kwetu Tanzania !

Mtunzi huteuliwa, nafasi akachukua,
Mshairi namba moya, nchi ikamchagua,
Akatunga na kusia, nchi yanayosisimua,
Hathaminiwi mtunzi, hapa kwetu Tanzania !

Taifa humtambua, mashairi kuyalea,
Jamii yakaifaa, kwenye shibe na njaa,
Na watu kuwausia, yote yenye manufaa,
Hathaminiwi mtunzi, hapa kwetu Tanzania !

Uongo huushushua, na kweli kuing'amua,
Watu akawaongoa, na nchi kutengenea,
Amani ikaenea, na umoja kukomaa,
Hathaminiwi mtunzi, hapa kwetu Tanzania !

Mshairi Tanzania, ni kichafu kitambaa,
Kamasi cha kutolea, kuishia kwenye jaa,
Hakuna anayemjua, walal kumsaidia,
Hathaminiwi mtunzi, hapa kwetu Tanzania !

Vyuo vinaugua, kwa homa ya malaria,
Maruerue kujaa, jinamizi kaingia,
Nao watindikiwa, ushairi unavia,
Hathaminiwi mtunzi, hapa kwetu Tanzania !

Vyuo vatindikiwa, ushairi umepwaya,
Washindwa kuitumia, sanaa kufundishia,
Wakawasha mshumaa, na fikra kuzagaa,
Hathaminiwi mtunzi, hapa kwetu Tanzania !

Mengi wakayaibua, tungo na fikra pia,
Mawazo wakachimbua, nchi kujaa kufaa,
Chemchemi ikajaa, hekima kutopotea,
Hathaminiwi mtunzi, hapa kwetu Tanzania !

Vyombo vya habari baa, sanaa yanyanyapaa,
Ila vichache radhia, Radio tunazojua,
Vipindi huviandaa, malenga tukasikia,
Hathaminiwi mtunzi, hapa kwetu Tanzania !

Magazeti nayo pia, ushairi yaonea,
Ukurasa yakataa, tungo kuzikubalia,
Machache hutokea, nafasi inapokuwa,
Hathaminiwi mtunzi, hapa kwetu Tanzania !

Hakuna Mtanzania, wa kuhariri sheria,
Mashairi kuyajua, msasa akayatia,
Yeyote huchaguliwa, kazi hii akapewa,
Hathaminiwi mtunzi, hapa kwetu Tanzania !

Televisheni balaa, sanaa hazijajua,
Muziki washikilia, hata tuchoke sikia,
Sasa ni kama kinyaa, kelele zinavyojaa,
Hathaminiwi mtunzi, hapa kwetu Tanzania !

Watunzi tuombe dua, watu macho kufungua,
Sanaa kuangalia, vizazi ikavifaa,
Isije ikajifia, na hazina kupotea,
Hathaminiwi mtunzi, hapa kwetu Tanzania !

Januari 29, 2012,

Dar es salaam.

No comments: